Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye Wizara yetu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Mimi mchango wangu nitauelekeza kwenye maeneo makubwa mawili. La kwanza ni kwenye mapitio ya bajeti kwa sababu ni utaratibu kabla ya kuchangia bajeti mpya kuangalia bajeti ya mwaka uliopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jiji letu la Arusha tuna changamoto kubwa sana ya ubadhirifu na usimamizi mbovu wa fedha za halmashauri. Hapa nitapenda nitoe mifano michache kabla sijaenda kwenye uhalisia. La kwanza tunajenga jengo la utawala la ghorofa zaidi ya sita, lakini bado wametafuta fundi mjenzi bila kutangaza tender, taratibu za manunuzi hazijafuatwa, wamemtafuta rafiki yao wamweka pale wamesaini mkataba wakampa kazi kwa kiasi cha shilingi 199,750,000. Lakini bado pia wamenunua vifaa vya shilingi 132,000,000, ambavyo havijadhibitika kufika eneo la site. Ukiangalia pia bado wameenda kuongeza nondo ziada ya tani 6.48 yenye thamani ya shilingi 17,000,000 ambazo ni kutokana na uzembe wa wataalamu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameweza pia kuongeza malipo ya 21,000,000 kwa fundi kutokana na uzembe pia wa watalaam wetu. Wameweza pia kuanza ujenzi huo bila kuwa na mtalaam mshauri katika ujenzi huo ambao ninaouzungumzia wa jengo la utawala. Pia bado kumekuwa na malipo fake, kumekuwa na risiti fake za EFD za kiasi cha shilingi 699,945,471, hela zimetoka wamefoji risiti wamepeleka halmashauri na tumekosa kupata huduma. Bado pia wameenda kutengeneza quotation za kughushi za shilingi 580,545,900 kwa kutumia kampuni ya Pedna Limited ambayo ni shilingi 543,000,000 na kampuni ya Arusha Hotel Ltd kiasi cha shilingi 36,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia wamefanya malipo ya shilingi 36,580,000 kwa wazabuni ambao hawakutoa huduma yoyote katika Jiji la Arusha na Mbunge akizungumza unasema huyu Mbunge anagombana na watu. Kwenye mambo kama haya lazima tugombane mpaka mambo yaweze kueleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na manunuzi ya shilingi 12,822,400 kupitia dokezo ambalo wanasema liliandikwa na mtu anaitwa Optat Ismail; lakini baada ya kuitwa amekana dokezo hilo, kwa hiyo hilo dokezo linaonekana ni fake lakini mchakato uliendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia kumekuwa na matumizi ya fedha za masurufu ya kiasi cha shilingi 62,000,000 ambayo yana viashiria vya ubadhirifu na kutokana na matumizi pia mengine ya shilingi 132,000,000 ambazo gharama zake hazina support yoyote ya matumizi. Wanachukua hela wanatumia na wala hawajali kwa sababu wanajua ngazi ya mkoa na wilaya wala hawana cha kuwafanya na pengine inawezekana ikawa ni sehemu ya changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na matumizi ya fedha taslimu kwa manunuzi ya bidhaa mbalimbali kiasi cha shilingi 2,000,000,000 ambayo hayana udhibitisho na wala matumizi yake hayaelezeki. Sasa haya masuala ni makubwa sana nadhani ni vizuri Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na timu yake wakafanya utaratibu wa kwenda kuweka jicho la ziada kwenye Jiji letu ili mwisho wa siku tuweze kuokoa hizi fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matumizi pia akaunti ya amana, yaliyokosa udhibitisho ya shilingi 92,692,714. Nimesema nianze na utangulizi huo kwa sababu Jiji letu limekuwa ni shamba la bibi, watu wameungana Serikali Kuu pamoja na Serikali ya Mtaa kuimaliza Halmashauri yetu. Mimi nimejitoa kafara kuhangaika na msuala haya ili kulinda maslahi mapana ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo suala langu la pili, nimesoma Hotuba ya Waziri wa TAMISEMI yenye page zaidi ya 281 lakini sijaona kama wamachinga wamepewa uzito unaostahili. Ukiangalia tu kwenye page ya tisa amezungumzia kwenye (viii) kwamba kuratibu shughuli za wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara wadogo basi, ukitoa hapo hakuna sehemu nyingine yeyote ambayo wamachinga wamezungumziwa na wamachinga ni kundi kubwa. Ukiangalia sisi tulitenga fedha mwaka jana kiasi cha 1,000,000,000 kwa ajili ya kuboresha maeneo yao, lakini zile fedha asilimia kubwa zimeliwa, wameenda kujenga eneo moja linaitwa Ulezi, ukiwaambia kule hakuna biashara watu hawawezi kwenda wakapeleka shilingi 86,000,000 baadaye wamebomoa hasara imepatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameenda kujenga jengo namba 68 baada ya kujenga bati yenye gauge 28 wametumia bati za gauge 30. Ukienda pale mvua ikinyesha tope tupu wananchi wanapata tabu, hata nia na lengo la Mheshimiwa Rais inakwenda kuwa kero kwa watu wakati dhamira ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kuwawekea watu mazingira mazuri ili waweze kufanya shughuli zao vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye upande wa machinga sisi pale tuna machinga namba 68, tuna eneo la Machame, tuna eneo la Ulezi na eneo la Mbauda. Ukienda maeneo yote changamoto ni kubwa sana; hakuna mitaro ya kupokelea maji, hakuna mataa ya uhakika. Ukiangalia wenzetu wa Dodoma hapa wamejenga jengo zuri sana ambalo linawapa fursa wafanyabiashara na maeneo mazuri zaidi. Ukienda kule Arusha ni utani na masihara ya hali ya juu. Nikuombe tumwombe na Waziri wetu na timu yake wakaongeze jicho ili wale wamachinga wapate mahali pazuri pa kufanya shughuli zao na mwisho wa siku dhamira na nia njema ya Rais wetu iweze kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna changamoto pia ya wenzetu wa mgambo; mgambo wanawasumbua sana wafanyabiashara wanawanyanganya vitu vyao, mama wengine hata wakifunga ushungi wanavuliwa ushungi wao, wanafanyiwa vurugu kila mahali kiasi ambacho inaongeza kero na manung’uniko kwa watu wetu. Mimi niombe mgambo hawa, kwa sababu wao hawana hatia, wao wanatumwa na Serikali katika ngazi ya mkoa na ngazi ya wilaya na wanamshinikiza Mkurugenzi ili kupambana na hawa watu. Naishukuru Halmashauri kwa namna moja au nyingine tukizungumza nao wakati wanapowanyanyasa wale watu wamekuwa wanawarudishia baadhi ya vitu vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe hawa mgambo wawekewe utaratibu maalum, hawa machinga pia wawekewe utaratibu maalum ili pasiwe na sintofahamu na vurugu kwenye jiji letu. Ukienda soko kuu wanaonewa pale, wafanyabiashara wamachinga, ukienda namba 68, ukienda Kilombero, ukienda kila mahali vurugu kila mahali. Kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri pia aongeze jicho kubwa kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulikuwa tuna ushauri, kama kama kuna baadhi ya masoko ya Machinga yanafungwa saa kumi na mbili na yanafungwa saa moja, tutafute baadhi ya barabara jioni ambazo hazitumiki sana na watu tuzifunge zile barabara, wale wafanyabiashara wadogo wadogo kuanzia saa kumi na mbili waruhusiwe kufanya biashara pale wapate riziki zao; maana mgambo wanawanyanganya vitu mpaka saa tano usiku. Hebu mniambie ukimnyanganya mtu muda huo unavipeleka wapi ilhali mtu anatafuta riziki kwenye maeneo yale?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna watu wanahusika na masuala ya parking. Wako wanaofanya biashara ya parking na kila mwananchi analipia parking kila siku, lakini wanashindwa kulipwa mishahara yao mwezi mmoja miezi miwili. Ukiangalia leo tangu Februari na Machi hawajalipwa ilhali ukiangalia fedha imeshaingia Serikalini. Kwa hiyo tuwaombe Serikali mkae na yule mzabuni kila mwisho wa mwezi wale wafanyakazi Watanzania wenzetu wa Arusha maskini wapate haki yao ya ujira wao kama wakati unavyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kumalizia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Gambo, muda wako umeisha.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sekunde chache kumalizia.
MWENYEKITI: Sekunde moja malizia Mheshimiwa Gambo.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwanza wewe binafsi, pia naishukuru Serikali yetu kwa kutenga shilingi 1,000,000,000 kwa ajili ya kukarabati Soko la Samunge, shilingi 1,000,000,000 kukarabati soko kuu na shilingi 1,000,000,000 kukarabati soko letu la Kilombero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana na namtakia Mheshimiwa Waziri…
MWENYEKITI: Ahsante sana.