Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia mchango wangu katika Wizara ya TAMISEMI. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na kutembelea katika majimbo yetu kuja kufanya ziara kwa ajili ya kuangalia changamoto ambazo ziko katika majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Mkoa wa Dar es Salaam na ninatoka Wilaya ya Ilala ambapo majimbo yetu majimbo mawili, Jimbo la Segerea pamoja na Jimbo la Ukonga yako pembezoni mwa mji. Katika majimbo yetu haya mawili kuanzia juzi na jana hali sio nzuri na kwa sababu Mheshimiwa Waziri anaijua vizuri Dar es Salaam na yeye mwenyewe ametokea Dar es Salaam kwa kweli anakielewa ninachokiongea. Nimekuwa nikichangia hapa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2020, 2021, 2022 na leo 2023 kuulizia mradi wa DMDP ambao ulikuwa utekelezwe 2021 na haya matatizo yote yanayoendelea Mkoa wa Dar es Salaam na mpaka sasa hivi unamwona Mbunge mwenzangu Jerry Slaa hayupo hapa, si kwa sababu hayuko anatembea, yuko katika Jimbo lake kuna mafuriko makubwa sana, na pia Mheshimiwa Zungu naye hayupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam hata mvua ikinyesha Kisarawe maji wa Kisarawe yote yabakuja katika Wilaya ya Ilala especially kwenye Majimbo ya Segerea, Ukonga pamoja na Jimbo la Ilala. Na ni kwa nini haya maji yanakuja pale? ni kwa sababu kuna miundombinu mibovu; ukianzia mifereji mpaka barabara zetu ni mbovu. Kwa hiyo tulikuwa tunautegemea sana sana Mradi wa DMDP ambao tumeambiwa kila mwaka unatekelezwa, kila mwaka unatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaongea hapa, tumeshampeleka Mheshimiwa Waziri tumemwonesha sehemu tunazotoka, hali ni mbaya sana. Kwa mfano katika Jimbo la Segerea Kata ya Buguruni, Kata ya Bunyokwa, Kata ya Vingunguti; na kwa Kata ya Vingunguti juzi wananchi pamoja na Mnyamani wananchi wameshindwa kutoka ndani, imebidi tuombe usaidizi kutoka kwa kampuni ya SGR ambao wanatengeneza barabara ili waweze kutusaidia kutoa yale maji. Hali ni mbaya; na yote hiyo sio kwa sababu yoyote ni sababu ya mifereji mibovu na michakavu ambapo kila wakati mmesema kwamba mnakuja kuturekebishia hii mifereji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana wewe ulikuja katika Jimbo letu la Segerea pia ukaenda mpaka Jimbo la Ukonga kuangalia hali ilivyo. Wananchi wetu wa Mkoa wa Dar es Salaam hakuna biashara yoyote wanayoifanya kama mvua ikinyesha. Mvua ikinyesha siku mbili, mfano kama jana na juzi, pamoja na leo nimesikia mvua inanyesha, hakuna watu wanaoenda kufanya kazi, hakuna mama ntilie anayepika chakula, hakuna bodaboda wanaofanya biashara na hawa wote wanaingiza kipato pia wanaiingizia kipato Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mkoa wa Dar es Salaam ni mji maarufu pamoja na kwamba si makao makuu. Watu wote wanaoishi Dar es Salaam wanategemea kufanya biashara lakini pia kuna wawekezaji wanatoka sehemu mbalimbali. Kwa jana na leo mwekezaji yeyote akija pale hawezi kufanya biashara yoyote wala hawezi kutamani kuwekeza, maana yake mazingira ya miundombinu hayamvutii. Maji ni machafu, mirundikano, mifereji michafu, barabara mbovu, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana sana, sisi tunaomba sana sana na kwa niaba ya Wabunge wenzangu hawa ambao hawapo tunaomba Mradi wa DMDP uanze, ambao ndio mmekuwa mnatuahidi kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama huu mradi ungekuwa umeanza na Mto wetu wa Msimbazi umetengenezwa basi haya mafuriko yangekuwa hayapo. Kwa hiyo tunaomba, umetuahidi kwamba huu mradi utaanza mwezi wa sita tunaomba uanze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka niongelee ni jambo la fidia. Katika Jimbo la Segerea kuna wananchi ambao walipisha airport, ninamshukukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Mkurugenzi wa TAA wamelisimamia hili jambo limefikia sasa sehemu nzuri, nilichokuwa ninaomba hawa wananchi wameishafanyiwa tathmini pia pamoja na biashara zao ambazo zilikuwa zinaendelea katika hilo eneo, kama walikuwa wana wapangaji, kama walikuwa wana nini, hao watu wote wameishaondoka, tunaomba sasa Mheshimiwa Waziri hawa watu walipwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea hapa na Mheshimiwa Waziri kasema kwamba wameishamaliza wanachukua sasa daftari kulipeleka Wizara ya Fedha, sasa tunaomba litakapofika huko Wizara ya Fedha lisije tena likakaa, likakaa tena miezi Sita, kwa sababu sheria inasema baada ya miezi sita tunaanza upya na mtakuwa Serikali mmepata hasara kwa sababu kwenda kufanya tathimini mnawalipa watu wa ardhi, nasi ikifika baada ya miezi sita tunafuta, tunaanza upya kwa sababu vitu vinapanda na sheria inasema kila baada ya miezi sita.

Kwa hiyo, niwaombe kwamba hawa wananchi sasa wamevumilia vya kutosha, tathmini tayari mmeishafanya na imeishamalizika tunaomba ikichelewa sana mwezi ujao wawe wameishapata hela zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni kuhusiana na Walimu especially ambao wanatoka Jimbo la Segerea. Kuna walimu wengi sana Mheshimiwa Waziri ambao wanapata likizo lakini hawalipwi malipo yao. Mfano, katika Jimbo langu la Segerea kuna karibu Walimu 150 wanadai pesa zao za likizo tangu 2015 mpaka sasa hivi hawajazipata. Sasa walimu wetu wanafanya kazi kubwa sana tunawavunja moyo, tunaomba hawa watu wapewe pesa zao za likizo ili waweze kufanya kazi zao vizuri. Kwa sababu kumuacha Mwalimu anaendelea kufanya kazi hii halafu akipata likizo hapewi pesa siyo jambo zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri, nawapongeza sana watu wa TARURA kwa kazi kubwa wanayoifanya, lakini sasa TARURA bajeti yao imekuwa ni ndogo sana. Kwa mfano, katika Wilaya yetu ya Ilala tunaomba kabisa kwamba TARURA waongezewe bajeti, bajeti ni ndogo sana na ndiyo maana barabara zao nyingi hawawezi kutekeleza. Kwa hiyo tunaomba katika mambo ambayo yatafurahisha Mheshimiwa Waziri ni kuiongezea bajeti TARURA, tumeishasema hatuitaji barabara za changalawe tena Mjini, tunahitaji tupate barabara za lami, kwa hiyo mtakapo waongezea itakuwa ni vizuri hata kwetu sisi ili tuweze kuangalia sehemu ambazo, kama ulivyopita Mheshimiwa Waziri, kwenye Jimbo langu jiografia ya Jimbo langu ina Kata…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umeisha.

BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninaomba nimalizie suala moja. Mheshimiwa Waziri jambo lingine tunaomba mthibitishe Mkurugenzi wetu ili aweze kufanya kazi akiwa comfortable. (Makofi)