Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara ya TAMISEMI.
Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Manaibu wake wawili, Katibu Mkuu na Viongozi wote wa TAMISEMI wanafanya kazi nzuri, tunajua kwamba wengi wao ni wageni kwenye Wizara hiyo na ninaamini kwamba wanatafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa utekelezaji wa bajeti kwa kutupa hela nyingi Wabunge wengi likiwemo Jimbo la Bunda ambapo tumepata bilioni 1.650 kwa miradi mbalimbali ya barabara ya Nyamswa – Bunda, barabara ya Sanzati – Nata, barabara ya Makutano – Sanzati na miradi ya afya na miradi ya zahanati. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu ukienda pale mitaani au ukiwa nje ya Bunge wanakuuliza mbona Wabunge, masaa yote mnampongeza Rais? Nadhani elimu iende kwa wananchi, tuwaambie kwamba Wabunge kazi yetu ni kupitisha bajeti, anayetekeleza bajeti na kuamua akusanye fedha ziende kwenye Majimbo yetu ni Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, yeye ndiye ana tekeleza bajeti, kwa hiyo tunamshukuru kwa sababu anatekeleza bajeti vizuri, anakusanya fedha na zinakuja kwenye Majimbo yetu. Kwa hiyo, lazima tufike hapa tuseme huyu tumekupa kazi ya kufanya na hiyo kazi unaifanya vizuri lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kazi anayoifanya nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba sasa tuna Wizara ya TAMISEM) ina Viongozi wengi wapya lakini nawaomba watazame Jimbo la Bunda. Halmashauri ya
Wilaya ya Bunda inajengwa hospitali ya Halmashauri ya Bunda – Nyamswa – Ikizu pale Bukama, tumepewa Bilioni Tatu na Milioni Mia Sita Hamsini toka 2018 mpaka leo hospitali ile ni gofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza maswali mengi sana, huwa nasema hivi Rais anapochaguliwa na wananchi, Rais anaetokana na Chama cha Mapinduzi na Wabunge wa CCM ndiyo wengi humu ndani, halafu akateua Mawaziri ni wa kwake, akateua Wakuu wa Mikoa ni wa kwake, akateua Wakuu wa Wilaya ni wa kwake, Wakurugenzi na Idara mbalimbali ni wa kwake, sasa anapowateuwa wanakwenda na analeta hela kwenye Halmashauri zetu na hela azisimamiwi hivi wanamjengea kura au wana mharibia kura? Najiuliza maswali mengi sana, nasema kama mtu amemteuwa kwenda kusimamia Idara fulani maana yake aliyeniteua anataka nijenge, nifanye kazi nzuri ya ufanisi ili kazi yake na yeye mwisho wa kuomba kura watu wampe kura vizuri. Niwaombe Mawaziri, niwaombe Wateule wa Rais, watekeleze kile walichopewa na Mheshimiwa Rais, kuwateuwa kwa madhumuni hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi yanayolalamikiwa na wananchi ni maeneo yanayotekelezwa na Serikali. Chama cha Mapinduzi kipo vizuri sana na tunaamini kipo vizuri masaa yote na muda wowote na miaka yote, lakini utekelezaji wa CCM kwenye upande wa Serikali kuna matatizo yake 3,650,000,000 zipo pale zimelala, amekwenda pale Waziri Ndugange nakushukuru ulikuja pale, umeyatazama pale ilivyo, hali ni mbaya. Juzi wananchi wa Nyamswa – Ikizu, vifaa vimeletwa vimefungwa na Halmashauri wenyewe wamefunga usiku, baada ya siku tatu vimeibiwa! Aliyekuja kufunga ni mwenyewe, aliyetoa taarifa ya wizi ni mwenyewe. Hizo taarifa tumewapa najua mtazifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe sana, Jimbo la Bunda Kituo cha Afya Mgeta, Kituo cha Afya Onyari, Sekondari ya Vilina na Halmashauri ya Bunda Hospitali naomba mtazame sana. Mheshimiwa Angellah Kairuki wewe unafanya kazi vizuri naomba uende utazame, lakini najiuliza swali moja hivi amezungumza hapa Mheshimiwa Kishimba, anasema tuunde Wizara ya Kero, mi najiuliza kwani Mheshimiwa Waziri na ofisi yako ukisema ukaleta hapa tathimini ukaleta karatasi humu ndani fomu, ukasema Wabunge wote wenye kero jazeni fomu halafu ukatukutanisha kama ulivyofanya Mkoa wa Mara juzi juzi hapa, kwani kuna ubaya gani? Si Waziri wa Kero ni wewe huyo huyo unataka nini sasa? Ni wewe huyo huyo Waziri wa Kero. Kwa hiyo, nikuombe kwamba sasa hili nalo ulitazame vizuri ili uweze kulitazama.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maombi haya sasa naingia kwenye maombi maana naweza nikaanza nikasahau haya yaliyotokea hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba Halmashauri ya Wilaya Bunda. Mheshimiwa Waziri na Mawaziri wengi wamepita pale sana, Wabunge nataka niwaeleze Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ni kama vile mtu anakaa Mkoa wa Morogoro halafu katika hapa Mkoa wa Dodoma halafu mbele yake ni Mkoa wa Singida, Halmashauri ya Bunda iko Jimbo la Mwibara iko Singida, Bunda wako Morogoro, wakitoka Morogoro wafike Dodoma wafike wachukue nauli waende Singida warudi tena Morogoro. Mazingira machafu sana, kelele nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko nchi zimeundwa kutokana na Jiografia yao. Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, iliundwa kutokana na Jiografia yake, tunaomba Halmashauri ya Bunda majengo tunayo iliyokuwa Halmashauri ya Bunda ya zamani ya Mzee Wasira, iko pale ina majengo yale tumeyaacha yanateketea, majengo mazuri sana tusaidieni sisi hatuhitaji majengo tunahitaji Halmashauri na Mkurugenzi awepo pale tuweze kupata Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi mengine niliyonayo ni Zahanati ya Kijiji cha Bigegu sasa naomba haya viongozi wote mnao husika msilikilize vizuri. Hali ya hewa hapo ni mbaya sana, Zahanati ya Kijiji cha Bigegu, Zahanati ya Salakwa, Zahanati ya Mawanga, Zahanati ya Nyaguzume haya ni maeneo hatarashi sana wananchi wa pale watoto wanakufa na malaria umbali wa kituo ni mrefu sana, naomba hilo nalo mlichukue. Naomba Kituo cha Afya Mihingo, Kituo cha Afya Nyamang’uta, Kituo cha Afya Kitale na Salama. Hali ya hewa hapo siyo nzuri kwa upande wa Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba barabara ya Kambugu – Nyabuzume – Vigutu – Butiama tumeishaiomba sana na Mheshimiwa Sagini, tuunganishe hizo barabara iweze kupita wananchi wa maeneo hayo ambayo wanafanya kilimo cha alizeti. Barabara ya Mikomarilo – Mirwa – Buhemba kule soko la Butiama barabara hiyo inahitajika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara ya Mavunga – Mtaro kwenda Jimbo la Bunda Mjini, barabara ya Mgeta – Salakwa – Maliwanda – Kilawila. Sisi tunazungukwa na Hifadhi ya Serengeti, Grumeti imetuzunguka pale lakini wananchi hawana uwezo wa kwenda kuuza mazao yao kwenye hoteli zile mle ndani, kwa hiyo tunaomba hiyo barabara tuipate ili wananchi waweze kufanya biashara kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije suala nyeti sana, Waheshimiwa Wabunge wenzangu tusijifanye vichaa, tunaomba tuelewane hali ya madawati kwenye shule zetu za msingi ni mbaya sana, Bunda peke yake madawati 11,840 hayapo! Jimbo la Bunda la kwangu 4,815 hayapo, hata ningetengeneza madawati kwa Mfuko wa Jimbo Milioni 51 nitakaa miaka 11 ambayo wananchi hawawezi kusema kwamba wanakubali au hawakubali, kwa hiyo hali ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya madawati kwenye nchi yetu siyo kwamba imeanza leo, Awamu ya Tatu ilikuwepo, Waziri Sumaye alitangaza kila mwananchi alitengeneza, wananchi waliungana wakatengeza dawati moja, 2018, 2019 nadhani humu humu Bungeni hata Bunge letu lilichanga tukatengeneza madawati mengi sana kwenye shule, haiwezekani watoto wakakaa chini, haiwezekani watoto wa nchi hii huru wanakaa chini haiwezekana! Tunaomba Serikali mtuunganishe mnaweza mkafanya mambo mawili:
Jambo la kwanza tangazeni kwamba wananchi watengeneze madawati tushirikiane nao tutengeneze; Pili tutumie Taasisi zetu na maeneo ya Serikali kutengeneza madawati. Naomba sana Waziri haiwezekani tukawa Wabunge, humu ndani watoto wa maskini wanakaa chini, haiwezekani! Kwa hiyo, tuangalie hali ya madawati siyo nzuri sana kwenye maeneo yetu. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere ahsante sana muda wako umeisha, nakushukuru sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)