Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuweza kusimama katika Bunge hili la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara yao hii ya TAMISEMI, kipekee kabisa nimpongeze Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri aliyoifanya katika suala zima la kuongeza bajeti ya TARURA. Ukiangalia Rais alipoingia madarakani bajeti ya TARURA ilikuwa bilioni 275 lakini mwaka wa kwanza wa bajeti ya Rais wa Awamu ya Sita bajeti ya TARURA iliongezeka kwa zaidi ya asilimia mia moja na hivi leo tunavyozungumza bajeti hii ya TARURA imeongezeka hadi kufika bilioni 778, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana ndani ya muda mfupi wa miaka miwili. (Makofi)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwita Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hili neno mnyonge huwa linatumiwa vibaya, haijawahi kutokea duniani Rais akawa mnyonge. Ahsante. (Kicheko)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Neema taarifa unaipokea?

MHE. NEEMA W. MGAYA: Naomba niendelee. Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya TARURA imeongezeka mpaka kufikia hiyo bilioni 7,78 lakini bado kuna changamoto katika utekelezaji kwa baadhi ya maeneo katika suala zima la Wakandarasi. Kuna baadhi ya Wakandarasi wanapewa kazi maeneo mengi lakini ili hali uwezo wao wakufanya kazi unakuwa mdogo, hivyo ufanisi wa kazi unakuwa hauonekani lakini vilevile kunakuwa hakuna tija kwa wananchi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba tuwape Wakandarasi kazi kutokana na uwezo waliokuwa nao, mwenye uwezo mdogo apewe kazi ndogo, mwenye uwezo mkubwa apewe kazi kubwa, isiwe mtu anafanya kazi kijanjajanja akisikia Songea wanalalamika anahamisha mitambo kutoka Lindi anapeleka Songea, hapo hatutafika kwakweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nichukue nafasi hii sasa kuomba maombi katika Halmashauri zetu za Mkoa wa Njombe. Nikianzia na Halmashauri ya Wilaya ya Makete, naiomba Serikali ituongezee pesa katika barabara inayotoka Kipengele kwenda Lupila barabara ya zaidi ya kilomita 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu mvua inanyesha miezi nane theluthi mbili ya mwaka mvua zinanyesha tu, ukizingatia kule Lupila ndiyo wazalishaji wakubwa wa viazi pamoja na mbao. Kuboreshwa kwa barabara hii kutasaidia mlaji wa mwisho wa kule Dar es Salaam ninyi mnaopenda kula chips Dar es Salaam watapata kwa bei nafuu. Kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha kwamba barabara hii inaboreshwa kwa maslahi ya Watanzania kwa ujumla pamoja na wananchi wa Makete. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, nilikuwa naiomba pia Serikali ituongezee pesa katika kuboresha barabara ya Makete – Isaplano kilometa 12 kule Halmashauri ya Makete, vilevile katika Halmashauri ya Wanging’ombe naiomba Serikali ituongezee pesa kama milioni 870 hivi kwa ajili ya kuboresha barabara inayotoka Malangali kwenda Wangama kilometa 15 kwenye mradi mkubwa wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile TARURA wasisahau Waziri Mkuu alikaa na Watendaji wote wa TARURA Tanzania nakuwapa maelekezo kwamba namna ya kuboresha barabara za Vijijini Nyanda za Juu Kusini, ichukuliwe kwa namna ya kipekee kutokana na wingi wa mvua katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini. Napenda niwakumbushe hilo na wazingatie hayo maelekezo ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye afya msingi. Nimpongeze Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kujenga Vituo vya Afya, Hospitali za Mikoa, Hospitali za Wilaya, Zahati zetu lakini naomba nitoe ushauri kutokana na changamoto hii Wauguzi na wafanyakazi wa Kada ya Afya ambao kila Mbunge anaesimama anaizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa Wizari hii ya TAMISEMI ikae pamoja na Wizara ya Utumishi waone namna ya kuongeza wafanyakazi, watumishi wa Kada hii ya Afya katika vituo vyetu vya afya, zahanati zetu, hospitali zetu ili kuweza kuleta tija katika suala zima la majengo haya ambayo tayari tumeishayajenga katika maeneo mbalimbali ya Kata zetu, Wilaya zetu na Mikoa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Wanging’ombe mahitaji ya watumishi wa Kada ya Afya ni 1,051, mpaka sasa hivi waliokuwepo ni watumishi 342 sawa na asilimia 32.6 kupungufu ya watumishi 709 ambayo ni sawa na asilimia 67.4. Tunaiomba Serikali ituangalie Halmashauri hii ya Wanging’ombe kwa jicho la huruma tuweze kupata watumishi hawa hili tuweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi wetu, sambamba na katika Halmashauri ya Makete kuna upungufu, Halmashauri ya Njombe Mji, Njombe Vijijini, Halmashauri ya Ludewa pamoja na kule Makambako. Kwa ujumla Mkoa wetu wa Njombe tuna upungufu mkubwa wa watumishi wa Kada ya Afya, tungeiomba Serikali ituongezee watumishi hawa wa Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye elimu msingi. Niseme tu kazi kubwa imefanyika katika Awamu hii ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mtakumbuka ndani ya mwaka mmoja alijenga madarasa karibia 15,000, madarasa 12,000 kwa shule za sekondari, madarasa 3,000 kwa shule za msingi na hii ilitusaidia hata watoto wetu kutokwenda second selection kwa wale wa sekondari lakini vilevile kwa wale wa elimu ya msingi ule umbali wa kutembea kwenda kutafuta shule umbali mrefu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amejitahidi sana kupunguza umbali kwa watoto wetu kutembea kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto, changamoto inarudi palepale kwenye wafanyakazi. Walimu hatuna wa kutosha ndani ya Mkoa wetu wa Njombe, Halmashauri zote Sita, hasa changamoto ya walimu wa sayansi imekuwa kubwa sana katika Mkoa wetu wa Njombe katika Halmashauri zetu zote Sita kwa maana Halmashauri ya Wanging’ombe, Makete, Ludewa, Njombe Mjini, Njombe Mji na Makambako. Kama unavyojua ulimwengu wa sasa hivi ni ulimwengu wa sayansi ni vyema tukawandaa watoto wetu waweze kukabiliana na ulimwengu huu wa sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie katika suala la mikopo ya asilimia kumi. Nampongeza Mheshimiwa Rais…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Amar.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba upungufu wa walimu wa sayansi siyo wapi huko anakosema Njombe, ni kwa nchi nzima upungufu huu upo ikiwemo pia na Nyang’hwale.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Neema, muda umeisha basi malizia sekunde mbili.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Kwa kumalizia napokea taarifa yake na naunga mkono hoja. (Makofi)