Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Dunia kwa kutujalia uhai, leo hii tuko hapa Bungeni tunachangia hoja ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya kuwatumikia Watanzania. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Angellah Kairuki na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Festo Dugange na Naibu wake Mheshimiwa Deo Ndejembi. Wote kwa pamoja nawapongeza kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuzungumzia kazi alizozifanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miaka miwili katika upande wa TAMISEMI. Mheshimiwa Rais kwa upande wa TAMISEMI ameshughulikia sana masuala ya afya ya binadamu kwa maana anawapenda Watanzania. Mheshimiwa Rais amehakikisha zahanati 1,066 zinajegwa nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha Hospitali za Wilaya 135 zinajengwa nchini Tanzania. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha vituo vya afya 713 vinajengwa. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha majengo ya dharura (EMD) 80 yanajengwa nchini Tanzania. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha vyumba vya dharura (ICU) 28 vinajengwa nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hakuishia hapo, ameweza kuhakikisha kwamba nyumba za watumishi 450 zinajengwa nchini Tanzania. Mheshimiwa Rais kwenye suala la afya hajaishia hapo, ameweza kutoa vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi bilioni 250. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, ameweza kuhakikisha kuna ajira 10,324 nchini Tanzania. Makofi kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo imefanya jumla ya Shilingi bilioni 600 kutumika kwenye masuala ya afya nchini Tanzania. Hili ni jambo kubwa, Mheshimiwa Rais amejali afya za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu vitu hizi Mheshimiwa Rais amevifanya kwa muda wa miaka miwili tu tangu alipoingia madarakani. Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, kwenye suala la elimu nchini Tanzania amehakikisha kwamba zinajengwa Shule maalum mpya za Sekondari za wasichana kwenye mikoa yote, na kila mkoa umepewa shilingi bilioni nne na shilingi bilioni 10 zimeshatolewa, na shule nyingine zinaendelea kupata fedha hizo, kwa maana ya kwamba, kila mkoa utapata shilingi bilioni nne kujenga shule hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hajaishia hapo, kumekuwa na ujenzi wa vyumba vya madarasa 23,000 nchini Tanzania. Hili ni jambo la kumpongeza Mheshimiwa Rais. Pia kumekuwa na ujenzi wa shule za sekondari na msingi ambazo zinaendelea nchini Tanzania chini ya juhudi za Mheshimiwa Rais. Ni obvious lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kasi hii ya miaka miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, kwenye suala la miundombinu tumeona barabara za vijijini zikijengwa na zikiimarishwa kwa maana kwamba tumeona TARURA wakipewa pesa kuimarisha barabara za vijijini na mijini. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba akina mama kutoka vijijini wataweza kufika mjini kupata huduma zao za afya au kama wana mahitaji zaidi.

Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, sasa naomba niende kwenye Mkoa wangu wa Katavi. Kwenye suala la elimu, naiomba Serikali… (Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Restituta, mimi ni Mwenyekiti sio Makamu Mwenyekiti.

MHE. TASKA R. MBOGO: Samahani Mwenyekiti. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la elimu kwa Mkoa wangu wa Katavi tunaipongeza Serikali, madarasa yanaendelea kujengwa. Nina ombi kwa Serikali. Ombi langu ni moja, ninaiomba Serikali iangalie suala la madawati. Nitoe mfano, pale Mpanda Mjini tuna Shule ya Msakila, ina upungufu wa madawati 400. Watoto wa darasa la kwanza wanakaa chini, chekechea wanakaa chini, darasa la tatu wanakaa chini na darasa la nne wanakaa chini. Pia wana Mwalimu wao Mkuu; Mwalimu Didas anajitahidi kuwafundisha watoto hawa, mpaka hii shule ni miongoni mwa shule bora kwenye Mkoa wetu wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo Shule ya Shanwe ina upungufu wa madawati 447. Naiomba Serikali, inapotupatia vyumba vya madarasa iangalie utaratibu wa kuziambia Halmashauri ziweze kuchonga madawati. Napenda kusema kwamba, niliwahi kumwuliza Makamu Katibu Mkuu Mheshimiwa Musonda, alisema kwamba suala la madawati ni suala la Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba basi Halmashauri zipewe Waraka ziweze kuchonga hayo madawati kwa sababu ukichukua mfano Shule ya Shanwe ni shule ya miaka mingi, imeanza toka mwaka 1961 lakini ina miundombinu mibovu, madawati hamna, na ina vyumba vitano. Ina uhitaji wa vyumba 12 vya madarasa, lakini sasa hivi ina vyumba vitano tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia pia, ni suala la matundu ya vyoo. Shule zetu nichukulie mfano, Shule hii ya Msakila, ambayo ni shule nzuri sana pale Mpanda Mjini, ina wanafunzi 2,300, lakini shule hii ina matundu ya vyoo 10 tu. Unaweza ukafikiria mwenyewe uhitaji wa wanafunzi 2,300 kwenda kwenye matundu ya vyoo 10, hali inakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, wakati tunakwenda kupata majengo mazuri ambayo tunajengewa sasa hivi, na Mheshimiwa Rais wetu amejitahidi kupata fedha za kujenga majengo hayo, tunaomba pia miundombinu ya vyoo izingatiwe. Darasa linapokwisha, madarasa yanapoongezeka, tunaomba pia masuala ya vyoo, maana ndio afya ya msingi ya shule, yazingatiwe. Pia masuala ya madawati yazingatiwe.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, muda wako umeisha Mhehsimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.