Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami nishiriki na Wabunge wenzangu kuanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha anatupatia fedha nyingi za miradi ya maendeleo. Sisi Wabunge kama Wabunge pamoja na Madiwani na wananchi kwa ujumla angalau sasa tunasimama kifua mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote wa TAMISEMI kwa kazi kubwa wanayoifanya kusimamia fedha hizi na kuhakikisha angalau yale makusudio na matamanio ya wananchi ya Mheshimiwa Rais yanafikiwa kwa wakati wake. Nachukua nafasi kukushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa fedha ulizonipa hasa kwenye upande wa elimu na TARURA. Mwezi uliopita nilikuwa naadhimisha uzinduzi wa madaraja ya kihistoria ndani ya Wilaya yangu, ni kwa sababu ya utendaji mzuri wa Mheshimiwa Rais, pia na Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu walionitangulia kukuomba Mheshimiwa Waziri uone namna ya kuongeza fedha kwa watu wa TARURA hasa kwenye miradi ya kimaendeleo. Fedha hizi Mheshimiwa Waziri, TARURA ndiyo msingi wa kila kitu kwa wananchi, inatusaidia kutuunganisha kati ya Kijiji na Kijiji, Kata na Kata, na pia inasaidia sana wananchi wanyonge pale wanapotaka kusafirisha na kufanya shughuli zao za kiuchumi. Naomba ulione hili na namna ya kuwaongezea fedha hasa kwenye miradi ya kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia hapa Mheshimiwa Waziri, kwangu kwa Mkoa wa Mara wote ukiacha Wilaya ya Rorya tu peke yake, sijaona fedha yoyote iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa upande wa TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninayo madaraja mawili pale yanaunganisha kati ya Kata na Kata kwa maana Nyakorogo, kuna Komaswa na pia inaunganisha Kata ya Kigunga na Kata ya Nyaburongo. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, haya madaraja mawili tuliyoyaomba sisi watu wa TARURA, na watu wa TARURA tukayaweka kwenye file la miradi ya kimaendeleo, unipe fedha ili niweze kutimiza haya madaraja mwishoni niunganishe na yale madaraja ambayo umeshanipa fedha ili tuweze kutekeleza yale ambayo yanatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anatimiza wajibu wake. Kazi yetu sisi kama Wabunge, viongozi wa kisiasa pamoja na watumishi, katika wajibu wa Mheshimiwa Rais wa kupeleka fedha ni kuhakikisha fedha inapokwenda kwenye miradi inasimamiwa ipasavyo na inazaa matunda. Tutakuwa Bunge ambalo halitakuwa lina matunda mazuri kama itakuwa kila tukisimama tunamsifia Mheshimiwa Rais kwa kupeleka fedha, lakini kule inapokwenda, usimamizi wa miradi ya maendeleo; moja, haikamiliki lakini mbili, inapigwa na inaliwa hadharani na watumishi ambao kimsingi wameamua kutoendana na kasi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kupitia Bunge hili kama viongozi wa kisiasa, pamoja na kusifia fedha nyingi zinazopelekwa na Mheshimiwa Rais, tutimize wajibu wetu kwa kuhakikisha angalau zile fdha zinazaa matunda. Kabla hata ya kusubiri taarifa ya CAG, Sisi tuwe ni watu wa kwanza kuhakikisha zile fedha angalau zinazaa matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Profesa, Mbunge wa Kahama, alisema neno zuri sana. Mbwa mzuri ni yule anayebweka kabla mwizi hajaiba, lakini mbwa ambaye anabweka baada ya mwizi kuwa ameiba, yule anakuwa sio mbwa. Kwa kifupi ni kama wale mbwa tunaowaita mbwa koko. Sisi hatutaki kwenda kwenye masuala ya mbwa, tunataka twende kwenye udhibiti wa fedha za umma zinavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Mheshimiwa Waziri unisikilize vizuri. Tunayo Hospitali ya Wilaya pale, imejengwa toka mwaka 2017. Awamu zote hizi, fedha imekuwa ikienda tumepelekewa jumla ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya kujenga majengo 14 na ile Hospitali iweze kufanya kazi. Mheshimiwa Rais, Mama Samia kwa awamu yake peke yake, ametupatia shilingi milioni 500 na akatupatia tena shilingi milioni 800 kwa nia njema kabisa kuhakikisha yale majengo yanakamilika na yanawasaidia wananchi. Leo ninavyozungumza na wewe, majengo yote 14 hakuna jengo hata moja lililokamilika kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukajiuliza, hizi fedha zinakwenda kwa ajili ya kutimiza, na hii ni bajeti ambayo inapangwa kwenye maeneo mengine ya Halmashauri nyingine; kwa nini Halmashauri nyingine wakipewa shilingi milioni 500 wana uwezo wa kukamilisha majengo matatu, lakini Wilaya ya Rorya haiwezi kukamilisha majengo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili Mhehsimiwa Waziri alitizame kwa jicho la upana. Umemsikia Mbunge Mheshimiwa Getere anazungumza hapa; ukimsikiliza Mkuu wa Mkoa na nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Mara, toka amefika ni miongoni wa Wakuu wa Mkoa ambao wamekuwa wakisema miradi ya maendeleo kwa Mkoa mzima wa Mara haikamiliki. Fedha zinakuja lakini hazikamilishi miradi. Moja ni hiyo Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, alikuja akaona. Katika sehemu ambazo zina vichekesho ukifika Mkoa wa Mara, ni Hospitali ya Wilaya ya Rorya. Inakuja fedha, shilingi milioni 500 ya kujenga madarasa matatu, mtu hajaanza kuchimba msingi, amenunua bati, na ananunua bati over estimation inayotakiwa. Kama bati zinatakiwa 100, anaomba bati 200. Anajenga shilingi milioni 500 inakuja; unamletea shilingi milioni 800, vile vilivyobaki stoo, hahami navyo kwenda kujenga kwenye miradi mingine, anakwenda kununua kwingine ili kupata 10%. Vitu vinabaki stoo, vinaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba mpaka mwisho fedha zinakwenda, miradi haikamiliki. Tunasubiri taarifa ya CAG ili aje aseme, ndiyo tuanze kuzungumza ndani ya Bunge wakati tuna uwezo wa kwenda na kudhibiti na kuchukua hatua kwa mtu yeyote ambaye anaharibu na anaharibu jina la Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri na nimekuwa nikikuomba sana, kwanza ufanye ziara ya kutembelea Hospitali ya Wilaya ili uweze kuona haya yanayofanyika pale, kwa nini Hospitali za Wilaya hazifanyi kazi? Kwa nini tumepewa zaidi ya shilingi bilioni tatu, maeneo mengine Hospitali za Wilaya zimezinduliwa, kwa nini Mkoa wa Mara na Rorya Hospitali hizi hazifanyi kazi? Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri hili aweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwenye kichekesho hicho hicho, sisi tulikaa na Baraza la Madiwani. Tumeanzia Kamati ya Fedha, tumekaa Baraza la Madiwani, tumepitisha Bajeti ya makadirio na makusanyo ya mapato ya ndani. Sisi ndio tumedhamiria kwamba kiasi hiki tunakusanya kama fedha za mapato ya ndani. Tumejiwekea shilingi bilioni 1.7, inakuja huku kwenu, inapunguzwa, mnasema hawawezi kukusanya 1.7, wakusanye 1.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, kwa hiyo, tunamfurahisha nani? Kama sisi tumefanya tathmini ya Baraza la Madiwani ambalo liko kikanuni na kisheria, limepitisha shilingi bilioni 1.7 ambayo tutakusanya kwa mwaka, na ninyi ndio mnawaambia Baraza la Madiwani wasimamie mapato na matumizi na mianya inayopoteza mapato; wameazimia kwamba sisi tunataka tu tukusanye shilingi bilioni 1.7, inakuja huku mnasema, hapana, tunawawekea shilingi bilioni 1.5. Nimeona hapa mnatuwekea shiligi bilioni 1.5 ya mapato ya ndani. Najiuliza, hii mmeitoa wapi? Inatoka wapi kama Baraza la Madiwani lenyewe limekaa na wataalamu, wamedhamiria kukusanya shilingi bilioni 1.7? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa madhara yake ni nini? Mwishoni ndiyo mnakuja kutuweka kwenye asilimia 20 ambayo alikuwa anaizungumza Mbunge mmoja hapa, kwamba fedha ya maendeleo itaenda asilimia 10, fedha ya mikopo ya vijana itaenda asilimia 10. Mmetutoa kwenye asilimia 40, mmetupunguzia fedha ya mapato yetu na kuwa madogo na wakati sisi mapato yetu tumeweka shilingi bilioni 1.7, ninyi mmeshusha, mmeweka shilingi bilioni 1.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwaomba Mheshimiwa Waziri, kwanza, irudi shilingi bilioni 1.7 kama ilivyopitishwa na kikao halali cha Baraza la Madiwani, na pili asilimia 40 ambayo ilikuwa inaenda katika miradi ya maendeleo, iende kama ilivyopangwa ili kuimarisha na kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo ya wananchi wetu inazinduliwa na fedha ya Serikali inatumika vizuri.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chege kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa nataka nimpe taarifa tu Mheshimiwa Jafari kwa anachokisema cha kuweka shilingi bilioni 1.7 then ikashuka kuja shilingi bilioni 1.5. Huo umekuwa ni ugonjwa ambapo wanajiwekea malengo madogo hafu baadaye wanakuja wanasema tumekusanya zaidi ya asilimia mia moja na kitu, kwamba tumefikia malengo zaidi ya asilimia na kitu. Kwa hiyo, ni ugonjwa ambao uko nchi nzima. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Chege, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo. Hili ndiyo kusudio; na ukisoma taarifa ya CAG ameizungumza hii hadharani kwamba Halmashauri nyingi zinajiwekea mapato madogo ili mwishoni wakikusanya asilimia 50 wafurahi na kujipongeza. Tunajiuliza, tunamfurahisha nani? Kwa sababu kwa kufanya yale, siyo tu kwamba tunataka kumfurahisha mtu, tunapunguza fedha ambazo zingekwenda kwenye miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi. Sasa angalia mnatuambia asilimia 10 ndiyo iende shughuli za maendeleo, haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwanza irudishe, lakini pili, kama siyo Wizara yako imefanya hili, kuna mtu ambaye ali-temper na maelekezo na maazimio ya Baraza la Madiwani, mchukulie hatua. Mheshimiwa Waziri kwenye hili nakuomba sana uwe mkali ili kuweza kurudisha haya tuliyokuwa tunayazungumza.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Chege.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)