Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi, lakini na niungane kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maajabu anayotuonesha sisi Wabunge wa Majimbo katika kazi za maendeleo zinazofanyika. Baada ya kuyasema hayo niwapongeze Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,

Mheshimiwa Rais hajawahi kukosea kwenye Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Tulianza na ndugu yetu Mheshimiwa Bashungwa, tunamshukuru tulienda vizuri na sasa tupo na dada yetu tunaamini kwamba, Mwendo uleule ataondokanao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuonesha kwamba, Wizara hii inafanya vizuri wanajiamini sana, hapa nimeshika document za kuonesha ni namna gani wametupelekea fedha kwenye majimbo yetu. Ninawapongeza nasema sawasawa, mko vuzuri, kule kujiamini kwenu kunasababisha na sisi kuwaamini ipasavyo, tunawaamini sana. Pamoja na mazuri na makubwa mliyoyasema, changamoto huwa hazipungui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sasa Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alisikilize hili ninalomwambia na amwambie Katibu Mkuu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambaye naye pia tunamuanini sana, amuandikie mkurugenzi wetu wa Halmashauri ya Mji Kondoa, kufanya mabadiliko kidogo kwenye fedha hizi za boost kwa maana ya kwamba, tuna fedha ya kujenga madarasa shule ya msingi Mongoroma, shule hii ya Mongoroma imezidiwa sana, ina wanafunzi 987. Katika wanafunzi hao wanafunzi wanaotoka mtaa huo ni wanafunzi 502, wanafunzi 485 wanatoka mtaa mwingine na wanafunzi 29 kutoka kwenye mtaa huo tunaotaka tujenge hiyo shule wanatembea kilometa 6.5 na hawa wanaokwenda Mongoroma kutoka Selia wanatembea kilometa 4.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale tuliona sisi wananchi wa Selia tuanze ujenzi wa shule ya msingi, tunasema shule shikizi, na tumeanza kujenga madarasa mawili na matundu ya vyoo vinne, ili kunusuru hawa watoto wanaotembea kilometa 6 kwenda kusoma shule ya msingi mtaa mwingine. Kwa sababu, naamini ni makusudio ya Serikali kila mtaa uwe na shule ya msingi ili kupunguza umbali, basi nimuombe aruhusu haya madarasa sita ambayo yanakwenda Mongoroma yakajengwe pale Selia madarasa sita na yale ya kwetu wananchi, yatakuwa madarasa nane na vyoo vyetu vinne tukichukua na hivi vyoo tutakuwa tueweza kuwasaidia hawa watoto wetu na tutakuwa tumefanya jambo lenye tija sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mongoroma kuna madarasa kumi ya shule ya msingi ambayo yote yanatumika. Kwa hiyo, tukiwabakiza wakibaki 500 hawa 400 wengine tukawatoa, watakuwa na sehemu ya kubaki na madarsa yao yanayowatosha wao na wale wa mtaa mwingine tutakuwa tumewasaidia kupunguza umbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nimuombe Mheshimiwa Waziri. Tumekwisha kamilisha shule kama mbili shikizi, zina sifa ya kusajiliwa, lakini tumekuwa wazito sana kwenye kuzisajili hizi shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri hebu wape maelekezo tuzisajili, mbona tumejenga shule ya sekondari hii mpya, tumeisajili mapema na leo tuna kidato cha pili kwenye sekondari yenu ambayo tunawashukuru sana, mmetusaidia sana watu wa Kondoa kupunguza idadi ya wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira kwa walimu pamoja na huduma ya afya, Wizara ya Afya, wauguzi, tuna tatizo kubwa kwenye shule zetu. Ukienda shule moja ya msingi Hachwi unakuta ina mwalimu mmoja na ni shule kongwe. Tunaomba msaidie, specifically, tupeleke walimu Shule ya Msingi Hachwi. Na ikiwezekana hizi ajira mpya tuchague sisi wenyewe, yaani sisi tuwapeleke walimu moja kwa moja kwenye shule na ikiwezekana tuwaambie tunatangaza ajira Shule ya Msingi Hachwi, tunatangaza ajira Shule ya Msingi Serengeni, tunatangaza shule ya msingi hii kwa hiyo, anayeomba ajue kabisa anaomba kupelekwa shule ya msingi fulani na kama hataki akatae moja kwa moja atafutwe ambaye atakubali kwenda as long sasa hivi mmefanya kazi nzuri za miundombinu. Kondoa inafikika sehemu zote hakuna haja ya mwalimu kushindwa kwenda kufundisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine kutokana na muda, niwapongeze kwa TARURA. Kwa kweli, mnafanya kazi vizuri sana, huyu Engineer Seif huyu anapaswa apewe hiyo haki yake kwa sababu, hatumsumbui sana isipokuwa kazi zake tunaziona, anapiga kazi sana. Kwa hiyo, tumshukuru, lakinis sasa pale kwetu kuna barabara moja muhimu sana ambayo ni ya kwake, inatoka Iboni kwenda Bilisa, ni barabara changamoto sana. Wananchi sasa wanatembea kwa miguu karibu kilometa saba kuja kutafuta mahitaji mjini, hapo mwanzo kulikuwa na gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna madaraja mawili-matatu pale ya kwenda kuyajenga. Hebu tusaidieni tuyajenge madaraja yale mtakuwa mmetusaidia kwa sababu, kwanza barabara yenyewe kwa umuhimu wake ndio barabara pekee ambayo inaweza ikawa mbadala wa barabara ya kwenda mikoa yote, kuunganisha Mkoa wa Dodoma na Manyara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa harakaharaka kutokana na muda, kuna haya mapato ya halmashauri. Sisi tuko Halmashauri ya Mji, Mheshimiwa Waziri usitufundishe uwoga wa kutafuta mapato, tunaomba uruhusu ile asilimia 40 ile ya maendeleo tuendelee kupambananayo kwa sababu, inatusaidia sana na hakuna mahali tunaweza kusema tumefeli, lakini leo kutupunguzia kutupelekea asilimia 20 maana yake hata mikopo ya wale vijana wanawake pamoja na mikopo ya wenye ulemavu itapungua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaendelea kuwakopesha milioni tatu, milioni nne, sasa ukipunguza zaidi tutakuja kuwakopesha kiwango kidogo kutokana na hiyo asilimia 20. Tuna uwezo wa kuendelea kujibana tuisaidie Serikali Kuu kufanya miundombinu ambayo tuna uwezonayo, leo tumeweza kujenga angalao zahanati mbili kwa kipindi cha mwaka huu mmoja. Sasa ukipunguza hicho kiwango cha fedha tukawaachia tu watendaji wakaendelea kuzitumia hata Madiwani watakata tamaa katika kusimamia mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri turudishieni asilimia 40 ya maendeleo ili wale wananchi tunaokwenda kuchukua kodi zao kule waweze kuona matunda ya fedha wanazolipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi huu wa tactic, watu wa Kondoa tunasubiri sana barabara za lami na Taa, tunasubiri sana. Sasa tunaomba utusaidie kwa sababu ni mji, tujenge barabara zetu kwa lami kama jinsi mpango wa Serikali ulivyo kwa hiyo, tufupishie ule urefu wa mradi huu ili tuweze kuupata kwa pamoja na tukienda 2025 tuwe tayari tumekwishaweza kuweka lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia. Mheshimiwa Waziri nikuombe, kabla bajeti hii haijaisha tuwe tayari tumeanza ujenzi wa sekondari mpya ya Bolisa kwa sababu, tuliomba sekondari mbili, moja ile mmetupa tumekamilisha, lakini sasa hii ya Bolisa tunaomba na yenyewe ianze kujengwa kabla ya bajeti hii kuisha. Hilo ukilifanya utakuwa umetutendea haki sana wana-Kondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, ikumbukwe kwenye hizi sekondari mpya ambazo tumezijenga, ilikuwa ije shilingi milioni 600 mpaka leo zimekuja milioni 470. Tumekamilisha na watoto wanasoma, lakini bado katika yale ambayo tulikuabaliana kwamba, shule hizi zinatakiwa ziwe pia na nyumba za walimu. Kulikuwa na milioni 130 hatujajua zimekwamia wapi mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri, Serikali ifanye kila la kufanya shule zilizojengwa ni mnzuri sana zitakuwa na fursa zaidi endapo walimu wetu hawatatembea mbali. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri zile milioni 130 ili tumalizie miundombinu, nyumba za walimu, pamoja na mfumo wa maji ambao unasoma katika shule ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nikushukuru sana na niendelee kuipongeza Serikali. Shukrani. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ally Makoa.

MHE. ALLY JUMA MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)