Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Jonas Van Zeeland

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya, lakini la pili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri ambazo anazifanya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda mbele sana kwenye mchango wangu, naomba nitoe ushauri kwa dada yangu, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Tunapokaa hapa ndani Bungeni tunapokea hizi taarifa za utekelezaji wa bajeti kwenye maeneo yetu na taarifa za mgawo wa fedha. Naomba nishauri kwanza kabla sijaenda mbele kwenye mchango wangu; taarifa hizi ni nzuri tukizipata kabla ya fedha hizi hazijaenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nimepokea taarifa miradi kule yote imeshatekelezeka na imeshaisha, leo napokea taarifa, lakini ni vizuri tukiipata mapema inatusaidia na sisi kwenda kusimamia kwenye utekelezaji. Ni ushauri tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Mheshimiwa Waziri pamoja na Manaibu Waziri kwa kazi nzuri na namna ambavyo wanamsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza ilani yetu ya uchaguzi 2025, lakini pia sisi mpaka sasa Mvomero tumeshapokea bilioni 3 na milioni 700 ya kujenga vyumba vya sekondari 187. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake. Lakini nina ombi hapa, haya madarasa tuliyoyajenga shule nyingi hasa za pembezoni hazina walimu. Tumejenga madarasa mazuri, lakini walimu ni wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, tuna uhaba mkubwa wa madarasa kwenye shule zetu za msingi. Pamoja na fedha tulizozipokea, lakini tuna uhaba mkubwa wa madarasa, lakini pia tuna uhaba mkubwa wa madawati, tuna uhaba mkubwa wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe sana, tunayo maboma ambayo tuliyajenga kwa nguvu zetu na ni maboma mengi sana. Tunaomba maboma haya Mheshimiwa Waziri utuangalie kwa macho mawili utuwekee kwenye bajeti yako mwaka huu kwa sababu, haya maboma mengine yameanza kuanguka. Yako maboma ambayo yamejengwa toka 2017 mpaka leo maboma yale yapo hayajamaliziwa, lakini tunawakatisha tamaa wananchi. Wananchi wanajitolea kwa kujenga wenyewe maboma, lakini Serikali inachukua muda mrefu kuyamalizia haya maboma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niishukuru Serikali, Mheshimiwa Waziri. Mmetupa fedha za kumalizia maboma ya zahanati pale Dihinda, mmetupa milioni 50 na boma lile tumemaliza na zahanati inafanya kazi, pale Ndole mmetupa milioni 50 tumemaliza boma na zahanati inafanya kazi. Chenzema mmetupa milioni 50, lakini mmetupa juzijuzi hapa shilingi milioni 50 pale Kidudwe na zahanati inaendelea na ujenzi. Mmetupa milioni 50 pale Manyinga ujenzi unaendelea. Lakini mmetupa milioni 500 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya pale Mziha na tumepokea milioni 600 kwa ajili ya kujenga pia, kituo cha afya pale Mlali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, bado tuna maboma mengi ya zahanati. Fedha tulizozipokea tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini tunaomba mwaka huu muendelee kututengea fedha kwa ajili ya kumalizia maboma ambayo tunayo katika Wilaya yetu. Pia tunazo nyumba za watumishi nyingi ambazo zimeanzishwa na wananchi, tunaomba pia mtusaidie ili tuweze kuyamaliza haya maboma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye TARURA, wenzangu wamezungumza hapa na wamempongeza Engineer wa TARURA na mimi nimpongeze. Tumepokea bilioni mbili na milioni 600 tumetengeneza barabara zetu, hasa zile za pembezoni, kule ambako ndiko wanatoka wakulima wetu, ndiko ambako tuna mazao ya kimkakati. Hizi barabara tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tumezitengeneza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu na ombi langu kwenu, hizi barabara nyingine tumeshindwa kwa sababu ya bajeti kufika mwisho. Mfano, barabara ya kutoka pale Magunga kwenda Maskat, ile barabara ina urefu wa kilometa 15, lakini kwa awamu hii tumetengeneza kilometa nane. Bado tuna upungufu pale wa fedha ya kumalizia ile barabara kilometa saba. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yako safari hii usituache, endelea kutupa fedha tumalizie hii barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, tuna barabara ya kutoka Muhonda kwenda Kweuma. Hii barabara na yenyewe haijafika mwisho kuna kipande kama cha kilometa tatu-nne, tunaomba Mheshimiwa Waziri na hii barabara utuangalie, utupe fedha tuweze kuimalizia hii barabara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali, mmetupa fedha tumeweza kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami pale Dakawa. Tumetengeneza barabara kutoka Manyinga kwenda Madizini kwa awamu ya kwanza yumeishia pale stendi kwa kiwango cha lami. Tunategemea tutaendelea kupata fedha kwa ajili ya kumalizia hizi barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna barabara ambayo tumeitengeneza ya kutoka Sangasanga kwenda Lubungo, tunataka barabara hii iende ikatokee Kilosa. Hii ni barabara ambayo ikiisha itakuwa ni barabara kubwa ya short cut kwa wakulima wetu ambao wanazunguka umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, kwa sababu ya muda, Dakawa ni eneo kubwa sana la biashara, nilikuwa ninaomba Mheshimiwa Waziri safari hii mtupe fedha tuanze ujenzi wa soko la kimkakati, Dakawa. Na pale kuna wakulima wengi, kuna wafanyabiashara wengi, tukipata fedha tukajenga soko pale la kimkakati tutawasaidia sana wananchi wetu wa Mvomero, hasa wananchi wa Dakawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jingine nimalizie, fedha zote ambazo tunazipokea sisi Mvomero, hizi za miradi, hasa hii miradi ya sekondari, vyumba vya madarasa na hii miradi ya zahanati, hawa watumishi wetu kwa maana ya watendaji, fedha nyingi zinazokuja, hasa kwenye vituo hivi vya afya mfano pale Mziha tulipopokea milioni 500 fedha ile haijatosha. Sasa hivi wanasema tuwaongezee bajeti kwa ajili ya kumalizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hizi zahanati zetu ambazo tumepokea milioni Hamsini-hamsini wanasema tuwaongezee fedha za kumalizia baadhi ya maeneo, fedha hazijatosha. Mheshimiwa Waziri nikuombe, kama unataka kweli kumsaidia Mheshimiwa Rais, Imarisha kitengo cha ukaguzi wa ndani. Kama kuna eneo ambalo tunapigwa na kama kuna mchwa ambao wapo kwenye halmashauri zetu, basi ni hawa wataalam wa haya majengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila jengo ambalo limejengwa kwenye Halmashauri lazima utaambiwa fedha ziliongezwa. Mwanzo wanafanya tathmini jengo litaisha kwa milioni 50….

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JONAS V. ZEELAND: zikija milioni 50 wanasema tupe 30 tumalizie.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa maliza.

MHE. JONAS V. ZEELAND Naomba Mheshimiwa Waziri imarisheni kitengo cha ukaguzi wa ndani, mtamsaidia sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)