Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kupeleka fedha nyingi sana katika majimbo yetu. Kwanza anatafuta fedha, anapeleka fedha zikafanye kazi. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amsaidie Mheshimiwa Rais kusimamia watumishi waliopo katika Serikali za Mitaa lakini pia kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ndiyo nchi, tunamtegemea sana. Ningedhani ungeshona makombati kama wale wenzake wa Kilimo ili ionekane kwamba ni mtu kazi, kwa sababu shughuli iliyopo TAMISEMI ni pevu kwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nimesoma bajeti hii sijaona mahali popote ambapo Mheshimiwa Waziri amesema kwenye bajeti hii kwamba anakwenda kukomesha shule kufungwa kwa sababu hakuna matundu ya vyoo, kwa watoto kukaa chini hakuna viti, madawati na meza, Walimu wanakaa mbali kwa sababu hakuna nyumba za kutumia watumishi wa kada za elimu na afya. Hii ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli wanavyozungumza kwamba shule fulani imefungwa haina choo, maana yake ni kuonesha kwamba hawa watu siyo wastaarabu na kwa kweli siyo jambo jema sana. Ni ama TAMISEMI wapeleke fedha au yaende maelekezo mahususi kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zetu watenge fedha na jambo hili likomeshwe mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekuwa msikivu. Kulikuwa na makisio ya fedha ya miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwenye majengo yetu kuna mabweni hayajakamilika, kuna mabwalo hajayaisha, kuna shule hazijakamilika kwa sababu wali- underestimate makadirio ya matumizi ya fedha katika halmashauri zetu, lakini naona wamegundua kwamba walifanya makosa, wameleta document hapa kuonesha kwamba angalau darasa moja ni shilingi milioni 25 na matundu ya vyoo yameongezeka. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri kilichobaki hapa ni kupeleka maelekezo mahususi kwamba vile viporo vya mabweni, mabwalo, madarasa na nyumba, fedha zitengwe ili zikamilike ili wananchi waweze kutumia katika matumizi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri afanye ukaguzi maalum wa ile asilimia 40 kwa baadhi ya halmashauri na asilimia 60 ya mapato ya ndani. Miradi mingi kwenye majimbo yetu ambayo viongozi wakienda wanaoneshwa kwenda kukagua na Waziri na Naibu Mawaziri, Waziri Mkuu na Makatibu Wakuu, wanapelekwa kwenye miradi ambayo fedha imetoka TAMISEMI kutoka Serikali Kuu. Tunaomba wakague miradi ya mapato ya ndani ya asilimia 40 na asilimia 60 ambako huo ndiyo mwanya wa upigaji mkubwa sana. Fedha nyingi zimepotea, miradi haijakamilika na watu wanagoma kulipa kodi kwa sababu hawaoni tija ya fedha ambazo wanatoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa miradi; nimeona kwenye andiko Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba zinaundwa Kamati ndogondogo za wananchi kwenye vijiji. Hapa kuna changamoto kubwa sana; zinakwenda fedha za miradi, zinaundwa Kamati za Ujenzi za Wananchi, zinaundwa Kamati z Mapokezi na Manunuzi, wanapewa vifaa kwa kuletewa, hawaendi kununua wenyewe wale wananchi. Hawana uwezo wa kuhoji, hawajui mambo ya manunuzi. Pia bahati mbaya sana katika hiyo shughuli hawana posho yoyote, kwa hiyo wanaishia kubishana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mwananchi ambaye atashinda kwenye kijiji asubuhi mpaka jioni hakuna chai wala chakula, wanagombana na Wakurugenzi, wanagombana na Walimu, wanagombana na Madaktari. Kwa hiyo miradi haikamiliki kwa sababu hakuna fedha ya usimamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hapa imeonesha namna ambavyo viongozi wa TAMISEMI watakwenda mikoani, mikoa itakwenda kwenye wilaya, wilaya waende kwenye kata na kata kwenye vijiji, wale wa chini wasimamizi wa kila siku hawapo, lakini kwenye bajeti hii hakuna mahali popote ambapo panaonyesha kwamba kuna posho hata kidogo kwa Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani mishahara au posho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zote hizi tirioni 9.1 zitasimamiwa na madiwani katika halmashauri. Wakurugenzi wamewapa mafunzo ya Kutosha, Wakuu wa Mikoa wamefundishwa, Ma DC wamekaa hapa Dodoma. Tunataka kuona semina kwa madiwani wetu wakijengewa uwezo ili waweze kusimamia fedha za halmashauri ili waweze kuhoji. Wanapewa fedha shilingi 40,000 wanapoteza mwelekeo kwa sababu ya mazingira hayo. Ni vizuri fedha itengwe wawezeshwe wawe na uwezo wa kusimamia na kuhoji ili miradi iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia usimamizi Mikoani, Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana ukamsaidia Mheshimiwa Rais, kama ambavyo umeangalia pia Baraza la Mawaziri, ni vizuri tukaanzia mikoani, hivi mkoa gani unaongozwa na nani kwa tija ipi. Kuna mwingine unamkuta ni mfanyabiashara unampeleka mkoa ambao ni wakulima au ni wachimbaji, haelewi. Lakini pia badala ya kushirikisha kumekuwa na order na amri mbalimbali. Katika maeneo yetu, amesema Mheshimiwa Jafar; kuna Migogoro pale Bunda ya ardhi haijatatatuliwa, kuna migogoro Rorya haijatatatuliwa, kuna migogoro Serengeti hakuna utatuzi, kuna Tarime hakuna utatuzi, Mkoa mzima ni vurugu match. Ukienda pale kwa Kurutambe na Magwe watu wanauana migogoro ya ardhi, viongozi hawaendi pale. Nenda Mnito Msege juzi wamechinjana, nenda Mnito Kibaso wameuana; hali ya utatuzi wa migogoro lazima…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa Mheshimiwa Waitara kwamba ni kweli kwa Mkoa wa Mara migogoro ya ardhi imekithiri na Bunda kuna mgogoro mkubwa pale Nyatwali watu wanalazimisha kuhama kwa fidia ndogo na wakidai wanatishwa, kwa hiyo hilo jambo lipo na ni very serious.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara taarifa unaipokea.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa muhimu sana kutoka kwa Ester Bulaya wa Bunda. Nilikuwa nasema kwamba hii migogoro isipo tatuliwa, Mheshimiwa Waziri anamsaidia Mheshimiwa Rais kutafuta kura za Wabunge wa CCM, Madiwani wa CCM, Wenyeviti wa CCM wa Mtaa na Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi. Ni muhimu sana jambo hili lipewe uzito kwa sababu wale wananchi wasiposikilizwa, wakaamrishwa, wakatishwa maana yake wanaleta hasira kwetu sisi. Kwa hiyo ni muhimu sana hili jambo likafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia usimamizi wa miradi; miradi mingi kwenye halmashauri, amesema Jaffar ukienda pale Bumela fedha imeenda milioni 500 imekwisha, ujenzi umesimama waliokula fedha wapo wanakula Maisha. Ukienda pale Magoma milioni 700 imekwisha kituo cha afya hakijaisha. Nenda Genkuru nenda Nyemwaga ukaguzi huu ni mwaka wa tano, timu zimeenda tisa ya ukaguzi maalumu hakuna ripoti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wabunge utaratibu wa kula fedha za umma za wananchi wakawaida hao maskini ambao tunawasemea Bungeni hapa halafu tunakaa kimya si sawasawa kwa kweli hawa watu wamejitolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa…

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ningetaka nitoe ombi kwenye Bunge hili ni muhimu sana. Baada ya bajeti hii Bunge lipate muda wa kujadili.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante sana, unga mkono hoja, muda wako umeisha.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyeki, si nitaunga baadaye?

MWENYEKITI: Mheshimiwa maliza, muda wako umeisha.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa mapendekezo ambayo nimetoa. (Makofi)