Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu katika Wizara hii ya TAMISEMI, lakini pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake, Naibu Mawaziri Waziri wawili pamoja na wetendaji katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi alizozileta katika jimbo la Mbagala. Elimu msingi tuna bilioni nne, tumejenga madarasa 142 na shule mpya za msingi nne. Elimu Sekondari tumejenga Shule mpya tatu, tumejenga madarasa 165 na jumla ya fedha zilizo letwa katika elimu sekondari ni bilioni 5.6. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya tumeletewa bilioni mbili kwa ajili ya kujenga hospitali ya Wilaya pale ya Zakem ambayo nimeipigia kelele muda mrefu sana. Tumepewa vituo vitatu vya afya na zahanati mbalimbali zimejengwa katika Jimbo langu la Mbagala. Kwa dhati yangu ya moyo nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na fedha alizozileta katika jimbo la Mbagala. Niwashukuru pia Mawaziri ambao wamesimamia na kutekeleza pamoja na viongozi wangu wa ngazi ya Wilaya, Mkurugenzi pamoja na Mkuu Wa Wilaya na Madiwani kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Sekta ya barabara tumeletewa bilioni 24, imetekeleza barabara mbalimbali katika jimbo langu la Mbagala. Ni jimbo ambalo lilikuwa halina miundombinu kabisa ya barabara; tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo mchango wangu nataka nijikite katika suala zima la barabara. Serikali inatuletea mradi wa uboreshaji wa barabara katika jiji la Dar es Salaam, awamu ile ya pili na ya tatu. Mheshimiwa Waziri ametuahidi mpaka mwezi wa nane mradi huo utaanza, lakini sisi watu wa pwani tunasema dalili ya mvua ni mawingu. Tunatarajia mvua itanyesha kwa maana ya ujenzi uanze mwezi wa nane lakini mawingu hatuyaoni. Barabara hizi sehemu zote zinapokwenda kupita zinahitaji zilipiwe fidia. Hatujaona mpango wowote kwenye bajate iliyotengwa wala kutoka Serikali Kuu, kwa maana ya Wizara ya Fedha, kwa ajili ya kulipia fidia katika maeneo yatakayo pisha ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti,tumuombe Mheshimiwa Waziri akija hapa atupe ufafanuzi, kama fidia hizi zitalipwa na halmashauri basi ni vyema halmashauri zikaambiwa mapema ili na tuweze kujipanga ni namna gani ambavyo tutalipa fidia; kuliko fedha zimekuja mradi unatakiwa uanze lakini fedha za kulipa fidia zinakuwa vikwazo vya utekelezaji wa miradi ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, miundombinu ya barabara katika Mkoa mzima wa Dar es Salaam ni tatizo; na hasa katika jimbo langu la Mbagala. Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Rais ya kutuletea fedha za kujenga barabara lakini ni lazima sasa tuone Wizara kupitia TARURA wanatutengea fedha za kutosha kujengea barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza msongamano katika Jimbo la Mbagala ni lazima barabara za kuunganisha kati ya Wilaya na Wilaya zijengwe; ni lazima barabara za kuunganisha kati ya jimbo na jimbo zijengwe; ni lazima barabara za kuunganisha kati ya kata na kata zijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanaotokea kusini wanajua pale kuanzia Kokoto mpaka Kongowe kunakua na foleni, ni kilometa mbili, lakini kama Madaraja yanayounganisha Mkuranga na Mbagala yakijengwa msongamano ule unaenda kuwa historia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kuna lile Daraja la Kidete ambalo liko katika Mtaa wa Bamia litaunganisha eneo la Kidete-Mkuranga pamoja na eneo la Mbagala. Kuna lile Daraja la Mbanga Kwalu ambalo liko katika mtaa wa Bamia, likijengwa linaenda kuunganisha Mbanga Kwalu, Mkuranga pamoja na Jimbo la Mbagala. Pia tunalo lile daraja la Churwi ambalo liko Kata ya Mianzini na Kata ya Chamanzi likijengwa linaenda kuunganisha jimbo la Mbagala pamoja na Mkuranga. Kwa kufanya hivi tunaenda kuondoa msongamano wa barabara ile ya Kilwa road.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunataka tujenge barababara ni lazima tuzingatie barabara zipi zinaenda kuondoa msongamano wa foleni katika barabara zetu. Tunazo barabara ambazo zinaunganisha kata kwa kata. Kwa mfano barabara ya Habari Zako hii inaunganisha kata ya Chamazi pamoja na kata ya Mianzini. Tunazo Barabara za Mabwawa ya Samaki, Kona Tope, Maandazi Road, Stanley, kwa Ndunguru na Kwamakuka. Majina haya yanatokana na asili ya Kizaramo ambao ndio wanaishi sana maeneo yale; na ndiyo maana wananchi wa Mbagala miaka hii mitano wamenikabidhi mimi mtoto wao kwa kuwa wanajua nazifahamu kwa majina barabara hiziā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti,nakushukuru sana naunga mkono hoja.