Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, na mimi nitachangia kwa uchache. Mosi nikitambua maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri Mkuu katika mahitimisho yake Tarehe 13, Mwezi wanne mwaka 2023, kuhusiana na asilimia kumi ya mikopo ya Vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika utambuzi huo nilidhani Waziri wakati anajibu atusaidie mambo kadhaa. Kwa sababu siku zote huwa nasema hii ni Wizara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ninyi hapo mmepewa dhamana ya kumsaidia. Katika mazingira ya kawaida, Wizara ambayo ni ya Rais inategemewa iwe ni mfano kwa Wizara nyingine kuiga. Sasa, tumeambiwa kwenye taarifa mbalimbali za Mkaguzi Mkuu; ya mwaka jana, ambapo mwaka jana pamoja na mambo mengine ilifanya majumuisho ya fedha ambazo hazijarejeshwa katika kipindi cha miaka mitano ya mfuko wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Kwa hiyo ukijumlisha za mwaka jana ambayo ilikuwa ni bilioni 47.1 na za miaka ya nyuma yake minne inaenda kama bilioni 100 plus, ukijumlisha na za mwaka huu ambazo ni bilioni 88 maana yake unaenda 188 billion plus.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida yangu ni moja, nimesoma maelekezo yako mahsusi ambayo umepeleka kwenye mamlaka za Mikoa na Halmashauri, maelekezo 14, hatuoni popote ulipotoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa, kwa Wakurugenzi kuhakikisha kwamba hizi fedha ambazo zimepotea huko chini inasemekana zimepotea huko chini, ziweze kupatikana zote. Sasa unapotoa maelekezo 14 lakini elekezo la upotevu wa billions of money hamtoi maelekezo mahsusi, unatupa jibu gani? Kwamba inawezekana kabisa hili jambo hamlichukulii serious, inawezakana kabisa hiyo miezi mitatu ikiisha ukaja mfumo mwingine mambo yatakuwa yale yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaitaka Serikali kabisa na nikutake Waziri, ukiwa unajibu hapa utoe maelekezo ya fedha hizi zilizopotea huko chini kwa wajanja, zikusanywe. Ulizungumza hapa Bungeni ukiwa unajibu swali lakini kujibu swali hapa Bungeni ni jambo lingine, kutoa maelekezo mahsusi kuhusu suala la kibajeti ni jambo lingine, hamjaliona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapopitia Kanuni za utoaji wa asilimia 10, unagundua kwamba hizi fedha hazijapotea, hizi fedha zimepotezwa. Sasa kama fedha zimepotezwa kuna element ya jinai hapa, lazima watu wawajibike kama wamehujumu uchumi, haiwezekani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu mnasimama hapa mnasema Rais wetu anazunguka mataifa kwenda kuomba fedha, hivi hamuoni aibu Rais anahangaika, fedha zinakuja halafu wajanja huko chini wanapiga? Kwa sababu ni kweli hizi ni mapato ya ndani ya Halmashauri yes, lakini ni sehemu ya mapato ya ndani ya Halmashauri ambayo kutokana na Halmashauri zetu kutokuwa na uwezo wa kimapato tunategemea mikopo ya nje kuendesha mambo mengine ya kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kanuni hii nitarejea tu kwa mfano, Kanuni ya Saba inawataja Watendaji wa Kijiji, Watendaji wa Mitaa na Watendaji wa Kata kama watu wa kutawakilisha vikundi, kuanzia Kijiji. Kanuni ya 13 Afisa Maendeleo ya Jamii anatajwa yeye ni usajili na uratibu, Kanuni ya 14 kuna Kamati ya Huduma ya Mikopo kuna Mkurugenzi wa Halmashauri na timu yake yeye anachambua na anajadili na kufuatilia vikundi. Kanuni ya 17 inataja Kamati ya Kudumu ya Fedha na Mipango ya Halmashauri zetu, wao wanaidhinisha mikopo, wako Madiwani, tuko Wabunge huku ndani, Kanuni ya 18 ni Mkutano wa Halmashauri kupitisha kile ambacho Kamati imepitisha. Kanuni ya 20 Sekretatarieti ya Mkoa wana jukumu la ufuatiliaji, Kanuni ya 21 Ofisi ya Rais - TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Bunge lituambie hapa eti kuna vikundi hewa huko chini? Nchi hii ilivyokuwa na cheo mpaka huko chini? Nchi hii mtu ukifanya hata uhalifu wa kawaida unavyoweza kutafutwa, kwa nini hapa kuna kitendawili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninapendekeza, CAG afanye kitu kinachoitwa Forensic Auditing yaani ukaguzi wa kiuchunguzi ili tuangalie kama kuna udanganyifu, kuna wizi ama kuna rushwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vitu hatuwezi kuviacha viende hivi. Mimi niseme wazi kabisa ili mradi Kiongozi wetu wa Muhimili Mheshimiwa Spika ametuamini kwenye Kamati ya LAAC tutafanya kazi yetu kwa uaminifu na kwa uadilifu mkubwa kulisaidia Taifa hili. Haiwezekani unaenda kuomba omba huko halafu unakuja Bilioni zaidi ya 100 zinadondoka chini halafu na wewe unacheka cheka tu! No, no, no! Mambo hayaendi hivyo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Halima muda wako umeisha.