Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, naomba nami nitoe pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu ambae amefanya kazi nzuri katika nchi hii, amekuwa Rais wa mfano, amekuwa suluhu ya matatizo katika nchi yetu, Watanzania kwa kweli kazi yetu ni kumuombea tu dua Mwenyezi Mungu aendelee kumuweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mkuu wangu wa Mkoa Mheshimiwa Halima Dendegu Mkuu wa Mkoa wa Iringa anafanya kazi nzuri sana katika Mkoa wetu tunampenda sana. Pia naomba nimpongeze Waziri Mwenye dhamana Angela Kairuki, Rais hakufanya kosa kumchagua nafasi aliyokupa chapa kazi nasi tuko nyuma yako Mwenyezi Mungu atakujalia, pia Naibu Mawaziri ambao yuko nao tunajua pia ni wachapakazi wazuri sana, endeleeni kuisaidia TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze TARURA kwa kazi nzuri sana, naomba kwa kweli waongezewe bajeti kwa sababu kwa kipindi kifupi tu wameonesha kazi nzuri anayoifanya. Niunge Mkono wale waliosema Seif apewe tuzo, chifu wetu apewe tuzo naunga mkono na apewe kweli kwa sababu kwa kazi nzuri ambayo barabara nyingi sana za vijijini zimefunguka na hata vifo vya akina Mama na Watoto vimepungua, Mungu ambariki sana. Pia nimpongeze TARURA Mkoa wetu wa Iringa yuko vizuri anafanya kazi vizuri, Mwenyezi Mungu ambariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kumpongeza Rais wetu kwa pesa za UVIKO na pesa za tozo ambazo alizitoa katika Mkoa wetu wa Iringa zimeongeza bajeti, karibu asilimia 200 ya bajeti kutoka Bilioni 6.3 hadi Bilioni 16.7. Ongezeko hilo limefanya barabara nyingi kuweza kujengeka za lami hata za changarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, bado zipo changamoto katika Mkoa wetu kutoka na jiografia yetu ina milima mimgi ambayo barabara zake nyingi zinahitaji madaraja mengi na wakati wa mvua huu barabara nyingi sana hazipitiki wakati wa masika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya barabara ambazo zina changamoto kubwa sana naomba tu nizitaje kwa uchache. Katika Wilaya ya Iringa kuna barabara ile ya Izazi – Mboliboli kilomita 25, kuna Mtwivira – Ikongo kilomita 1.5, Mufindi kuna barabara ile ya Tambalang’ombe – Kwa Mtenga kilomita 41, Luganga – Itimbo – Isupilo kilomita 11. Wilaya ya Kilolo kuna barabara ya Muhanga – Mugeta kilomita 18, Ilula – Uhambingeto – Ulambilelo kilomita 17, Mtandika – Nyanzo kilomita 40, Itimbo – Kitelewasi kilomita 26, Ilula – Ibumu kilomita 20. Pia kuna barabara kutoka Kitowo kwenda mpaka Masisiwe hii barabara mpaka sasa hivi nilipita juzi tu ina changamoto nyingi sana. Kwa hiyo, ninaomba TARURA iziangalie hizi barabara hizi barabara ili Mkoa wetu wa Iringa uweze kufunguka kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao upungufu mkubwa sana wa watumishi wa kada zote katika Mkoa wetu wa Iringa. Nikichukulia tu kada ya afya watumishi wanaotakiwa ni 4,647 na waliopo 2,416 upungufu kama 2,111 kama asilimia 48. Tunaomba Wizara sasa katika hizi ajira mpya iangalie kwa jicho la kipekee Mkoa wetu wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tupongeze ujenzi na ukarabati wa shule zote nchini lakini sasa waangalie pia Walimu wetu waboreshewe nyumba zao zijengwe na hasa huko Vijijini na zikarabatiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani wenzetu pia wanachangamoto nyingi sana, Mimi ni mjumbe wa ALAT. Zipo changamoto ambazo tuliainisha tulitegemea sana zingefanyiwa kazi, wanafanya kazi kubwa kwa kweli changamoto ni nyingi waangaliwe na waboreshewe maslahi yao ili waweze kufanya kazi vizuri kwa sababu miradi yote ipo chini yao. Hata Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Mitaa pia waboreshewe posho zao kwa sababu wanasimamia miradi pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitambue wadau wa maendeleo wanaochangia katika Mikoa yetu lakini wanasaidia pia katika bajeti yetu. Katika Mkoa wetu yuko mdau Mkubwa MNEC wetu mpendwa Ndugu Salim Asas, ameweza kutoa kwanza Shilngi Milioni 100 kwenye majengo ya Machinga, amechangia ujenzi wa jengo la Ustawi wa Jamii ambalo ni la mfano na Waziri Mkuu alilifungua. Pia amejenga jengo la damu salama, amejenga jengo Watoto Wachanga, ujenzi wa ICU, jengo la viungo bandia, jengo la wagonjwa maalum (VIP) lakini huwa anatoa maziwa kwenye shule zote. Mdau huyu ni wa kuigwa nchi nzima na siku nyingine aletwe hapo tumpigie makofi ili wengine waweze kumuiga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, malipo ya Wazabuni, wanapata shida sana, naomba kabisa Wazabuni hawa wamekopa benki, wanalipa riba, TRA wanatozwa zile penalty, usumbufu mkubwa sana wanakwenda huko hazina, naomba waangaliwe kwa kweli na tuambiwe kwamba wazabuni wako wangapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu asilimia 10. Kuna watu hawakopesheki, kuna wamama ambao wamezaa watoto wenye ulemavu, hawa watu hatujajua wamewekwa kwenye kundi gani? Wanabeba watoto kuanzia asubuhi mpaka jioni, wanatafuta pesa kwa ajili ya kuwasaidia hawa Watoto, bado Serikali haijajua kwamba je, hawa watu wanakopa kule kwa watu wenye ulemavu au kwa hawa wamama wa kawida? Kwa sababu, hebu tuangalie mimi nakuomba Mheshimiwa Angela Kairuki wewe ni Mama mwenzetu naomba utakapokuja utujibu hawa wamama wapi wakope? Wako kwenye kundi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hautatoa jibu nitashika shilingi nitaomba Wabunge wote watuunge mkono ili hawa wamama wajue wanakopesheka katika fungu gani, kwa sababu wote humu ndani ni walemavu watarjiwa, lakini hawa wanawake wengine wamewakimbia na waume kwa sababu wamezaa watoto wenye ulemavu. Jamani hili jambo ninalisema kwa uchungu mkubwa ninaomba Bunge hili kwa kweli hebu liangalie na tutoke na suluhu. Tumeuliza sana maswali lakini hatupatiwi majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana na Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)