Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru nami niweze kuchangia, kwa mara nyingine tena nimshukuru Mwenyezi Mungu. Kwanza naunga mkono hoja iliyoko katika meza yako. Naomba nitoe ufafanuzi wa mambo mawili matatu ambayo yamezungumzwa hapa. Hoja ya kwanza ni iliyoletwa na Mheshimiwa Esther Matiko kuhusu uhifadhi na utunzaji wa watoto walioko magerezani.
Sheria ya Mtoto, The law of the Child ya Mwaka 2009, katika kifungu cha 144 inaeleza namna gani mtoto aliyeko gerezani kwa sababu amekwenda kule na mama yake au na mzazi, anavyopaswa kutunzwa. Naomba niisome sheria yenyewe na ambacho tumefanya katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa sababu ya umuhimu wa sheria hii, tuliamua kuitafsiri, kwa hiyo, iko kwa Kiswahili. Ni sheria muhimu sana na naomba Waheshimiwa Wabunge mtafute hii sheria muisome, itatusaidia sana kwenye maeneo yetu kule tunapokuwa tunaongelea haki za watoto, haki za Watoto wanaoshtakiwa Mahakamani, walioko mbele za Polisi na hawa ambao sasa wanakwenda magerezani wakiwa na mama zao au wamezaliwa kule magerezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 144 cha sheria hii kinasema hivi:-
(i) Pale ambapo mama atakuwa gerezani na mtoto wake katika mazingira yoyote yale, hatua zote zitachukuliwa na uongozi wa magereza kuhakikisha kuwa mtoto anapata matunzo yanayohitajika kutoka kwa mama inavyostahili, mlo kamili, virutubisho na huduma ya afya pamoja na chanjo.
(ii) Uongozi wa Magereza utamfahamisha Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya kuhusu mtoto aliye gerezani na mama yake na ambaye ameacha kunyonya.
(iii) Endapo Afisa Ustawi wa Jamii amepokea taarifa kutoka katika uongozi wa gerezani, ataamua sehemu stahili ya kumweka mtoto huyo ambayo inaweza kuwa;
(a) Mzazi ambaye hayuko gerezani;
(b) Ndugu;
(c) Mlezi; na
(d) Mtu anayefaa kumlea huyo Mtoto.
(iv) Iwapo watu waliotajwa chini ya Kifungu kidogo cha (3) wanakosekana, Afisa ustawi wa Jamii ataagiza mtoto huyo apelekwe katika makao yaliyothibitishwa hadi hapo mama yake atakapoachiliwa kutoka gerezani
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utakuta sheria imeweka utaratibu na mwongozo mzuri. Inawezekana kukawa na changamoto Waheshimiwa Wabunge mnapokwenda kule mnazipata, haya basi mzijulishe mamlaka zinazohusika ili hatua zile zirekebishwe. Magereza wenyewe wana utaratibu mzuri sana wa kuwaangalia hawa watoto wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ambalo ningeomba kushauri, hili ni wajibu wa kikatiba wa kila mwananchi. Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naomba kuisoma tu hii inasema hivi: “Kila mtu ana wajibu wa kuifuata na kuitii katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano.” Sasa Bunge hili na lenyewe linaongozwa na katiba, sheria na kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika chombo kama hiki ambacho kinafikia maamuzi yake kwa majadiliano, maana maamuzi hapa yanafikiwa baada ya kujadiliana, inafaa sana zile sheria ambazo tumejiwekea za kuongoza majadiliano humu ndani ili tufikie Maamuzi ziheshimiwe sana na sheria zenyewe kwanza ni Katiba yenyewe; pili, sheria ya haki na kinga za Bunge, tatu na kanuni hizi ambazo zinatungwa kwa mujibu wa ibara ya 89, tukifanya hivi, Waheshimiwa Wabunge shughuli zetu hapa zitafanyika kwa amani, kwa hekima kubwa, kwa ufanisi mkubwa, kila tunachotaka kuishauri Serikali kitafika kwa wakati maana hakutakuwa na kuingiliana na Serikali itachukua hatua kukifanyia kazi. Huo ndiyo ushauri wangu, vinginevyo hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili naona niliomba nilifafanue kusudi turudi katika utamaduni wa Bunge hili wa kufanya shughuli zetu kwa amani, kwa ufanisi, kwa kuzingatia katiba na sheria na kanuni ambazo tumejiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu na la mwisho ambalo ningeomba kushauri hapa, Jeshi la Polisi mimi nafanya nalo kazi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inafanya kazi kwa karibu sana na Jeshi la Polisi. Ni jeshi ambalo linafanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana kuhakikisha kwamba amani na usalama katika nchi hii vinaendelea kuwepo. Unaweza ukawepo upungufu kwa baadhi ya askari, lakini haiwezi ikachukuliwa kwamba ni jeshi lote na haiwezi kuwa kwamba, kama wote hawa wangekuwa ni wala rushwa, kama wote hawa wangekuwa wameshiriki ku-league uchaguzi, basi baadhi ya Wabunge leo wasingekuwa humu ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilifahamishe Bunge lako Tukufu, baada ya Uchaguzi Mkuu kulikuwa na mashauri 52 ya uchaguzi ambayo yamefunguliwa lakini katika mashauri yote hayo wako wa Chama cha Mapinduzi, wako wa Vyama vya Upinzani CHADEMA, CUF na NCCR, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewatetea na sasa mashauri 39 yameshamalizika Mahakamani. Kwa hiyo, kama kuna kasoro zimetokea hoja siyo kuleta humu Bungeni, kwa mfano, aliyosema Mheshimiwa Lwakatare kama kungekuwa na shida pale hoja ingekwenda mahakamani pale, lakini hakuna hata election petition kutoka kwenye lile Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kushauri kwamba, Waheshimiwa Wabunge tujizuie sana kutoa majumuisho ya jumla jumla ya kulaumu jeshi kwamba linafanya hivi, linafanya hivi, lazima tuishi tu kwa kuzingatia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono. Ahsante sana.