Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii ya TAMISEMI. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya katika nchi yetu, amejipambanua kwa jinsi ambavyo analeta pesa nyingi katika Majimbo yetu. Ninaapongeze wasaidizi wake Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo wanamsaidia na jinsi ambavyo wanakimbia kimbia huko kwenye Majimbo yetu kuhakikisha kwamba utekelezaji wa Ilani unakwenda kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Watendaji wa Wizara ya TAMISEMI nikianza na Mheshimiwa Waziri Angela Kairuki na Wasaidizi wake wote na timu yake nzima wanafanya kazi nzuri kuhakikisha kwamba kule Majimbani tunaweza kusimama kwa kujiamini kwa sababu miradi mingi inatekelezeka katika Majimbo yetu. Niwapongeze watumishi wetu wa Mkoa wa Kigoma wakiongoza na CP. Thobias Andengenye, hususani wale wa Halmashauri ya Kibondo kwa jinsi ambavyo wanapambana kutekeleza hii miradi inayokuja na kipekee kwa jinsi ambavyo wamekamilisha kwa wakati miradi iliyokuja ya madarasa na vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Muhambwe naomba nifikishe pongezi na shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa pesa nyingi alizoleta. Jimbo letu limepokea Bilioni 18 zikiwa ni pesa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hizi zimewezesha kutekeleza miradi mbalimbali katika Jimbo letu la Muhambwe. Tumetekeleza miradi mingi kwenye elimu afya na barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pesa hizi bado Jimbo la Muhambwe lina changamoto. Nitaanza na changamoto kubwa ya ajira hasa ajira ya Walimu na Watumishi wa Afya. Mkoa wetu wa Kigoma una watumishi 1,955 wa afya ikiwa mahitaji yetu Mkoa wa Kigoma wote tunahitaji watumishi 7,699 kwa hiyo tuna uhaba wa asilimia 74 kwa kiwango cha juu cha uhitaji, lakini kwa kiwango cha chini cha uhitaji tuna uhaba wa asilimia 64.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Muhambwe lina mahitaji ya juu ya watumishi 977 lakini tuna watumishi 311 tu ikiwa ni upungufu kwa asilimia 76, Jimbo hili la Muhambwe tunazalisha wakinamama 50 mpaka 55 kwa siku. Kwa hiyo, kwa mwaka mzima tuna vizazi hai 17,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba huu mzigo tuliokuwa nao jimbo la Muhambwe basi na Mkoa mzima wa Kigoma katika ajira hizi tunazotegemea kupata naomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma tukiwa ni Mkoa wa pembezoni, watumishi wengi wanakimbia, tupewe watumishi wa kutosha wakati huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhaba wa walimu. Katika Jimbo la Muhambwe tuna shule ambazo zina walimu wanne kama ile ya Nyaruhaza na Ntoyoyo tuna walimu wanne tu shule ya msingi. Vilevile nimepata taarifa kwamba kwenye mgao huu wa walimu tumepata mgao wa Walimu 15 hawatoshi kabisa. Nimuombe Waziri, Jimbo la Muhambwe mtusaidie tupate walimu 60 ili angalau hizi shule ambazo zina digit moja moja basi angalau kutoka wanne wawe nane. Tuna shule zina walimu sita nyingi, naomba mtusaidie Jimbo la Muhambwe tupate walimu 60 wa msingi ili tuweze kupambana na uhaba wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile shule za sekondari tuna uhaba mkubwa sana, kipekee nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu kwa mgao wa madarasa tuliyopata Jimbo la Muhambwe tumefanikiwa kusajili shule tatu za sekondari mwaka 2022 na mwaka 2023 tumesajili shule nne, hivyo tuna uhaba mkubwa wa walimu. Niiombe Serikali tupate mgao mkubwa kwa ajili ya walimu wa sekondari angalau walimu 70 ili tuweze kukabiliana na uhaba huu wa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya Shule 24 tulizonazo za sekondari tuna sekondari Tatu tu za Kidato cha Tano na cha Sita. Kati ya hizo, shule za sekondari moja ilikuwa ni Kambi ya Wakimbizi ya Mkugwa, ninamuomba Mheshimiwa Waziri siku moja aje tukaitembelee hii shule inatia aibu haina madarasa. Ninakuomba shule hii ipatiwe madarasa pia ninaomba tupatiwe na mabweni mawili ili tuongeze shule mbili za Kidato cha Tano ikiwa ni ile shule ya Busagara na Kumgogo ili angalau tuwe na Shule za Kidato chaTano Tano katika Jimbo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa TARURA nami niwapongeze TARURA wanafanya kazi nzuri na Engineer Victor kwa kweli anastahili sifa zote tulizompa. Sisi tumepata utekelezaji wa madaraja ya mawe, tumepata madaraja ya mawe 19 katika Jimbo la Muhambwe. Kwa hiyo, baada ya kupata haya madaraja tunazo barabara ambazo zinahitajika kuunganishwa, hizi barabara zikiunganishwa basi wananchi wetu wataweza kupita. Tunahitaji kuunganisha Kitahara na Bunyambo, tunahitaji kuunganisha Luhunga na Bunyambo, tunahitaji kuunganisha Nengo na Mbizi, tunahitaji kuunganisha Nyakasanda na Mukarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji Milioni 591 tumeomba, ninawaomba TARURA, nimuomba Mheshimiwa Waziri anisaidie kupata hizo pesa ili hizi Kata na hizi barabara ziweze kuunganishwa kwa sababu tunayo tayari madaraja ya mawe ambayo yamejengwa na Shirika la Enabel, kwa hiyo, tunaomba tuunganishiwe hizi barabara ili wananchi waweze kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo bado pia tunauhitaji wa madaraja ya mawe ambayo pia tumeleta, tunahitaji madaraja ya mawe 20 ambayo tunategemea kujenga kule Kagoti na Nyaruranga ili kuwasaidia wananchi wanokwenda mashambani lakini na watoto wa shule wanaokwenda mashuleni wasipite kwenye maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali tuchukue teknolojia hii ya bei nafuu ya kutengeneza madaraja ya mawe ili tuweze kuwasaidia wananchi wa Muhambwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Muhambwe nalo lina maboma ambayo yanahitaji kumaliziwa ikiwemo lile boma la kituo cha afya cha Kizazi lakini madarasa ya karukambati, madarasa ya Kigina, niombe TAMISEMI waje na mpango mahsusi wa kumalizia haya maboma kwa sababu hizi ni nguvu za wananchi na wananchi wanapenda kuona utekelezaji ukifanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuomba utekelezaji wa ahadi za viongozi. Niombe ahadi ya kituo cha Afya cha Mulungo na ahadi ya Milioni 200 kituo cha afya cha Nyaruyoba iweze kutekelezeka. Wananchi wanasubiri kuona utekeleaji wa ahadi hizi kwa sababu ni ahadi za viongozi wakubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)