Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami nichangie katika Wizara hii ya TAMISEMI. Awali ya yote, napenda kumpongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake nyingi sana na kubwa alizozifanya katika kuweka miundombinu mingi ndani ya miaka miwili katika sekta mbalimbali na hususan katika sekta ya afya na elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kuwapongeza Waziri pamoja na Manaibu Waziri wa TAMISEMI kwa kazi nzuri wanazofanya, wamekuwa wasikivu, wamekuwa wakipokea simu kwa wakati, wamekuwa wakitoa ushauri na ushirikiano uliotukuka. Nawapongeza sana. Naomba nielekeze mchango wangu katika sehemu mbili; sehemu ya kwanza ni sehemu ya afya pamoja na elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Rais wetu kwa miundombinu mizuri katika sekta ya afya hususani majengo ya zahanati, hospitali na vituo vyote vya afya katika nchi yetu. Hiyo inaonesha dhahiri kwamba nia ya Rais kuwafanya Watanzania kuwa na afya, ni kubwa sana. Ni dhahiri kabisa kwamba wananchi wanapokuwa na afya, basi wanaweza kufanya shughuli zao za kuleta maendeleo. Kwa hilo nampongeza Rais sana kwa dhati pamoja na Mawaziri wanaohusika kwa kuliangalia hilo na kwa kulishughulikia kwa uangalifu na umakini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kila mafanikio kuna changamoto ambazo ni vizuri sisi Wabunge tukatoa ushauri ili tuweze kufikia mafanikio makubwa zaidi ya hapa ambapo tumefikia. Ni imani yangu kabisa kwamba Mawaziri watayachukua na yatafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la ajira katika masuala ya afya. Ajira ni changamoto, hospitali zipo na wagonjwa wapo kila siku, lakini wafanyakazi ni wachache. Tukiangalia katika hospitali zetu nyingi kutokea zahanati mpaka hospitali kubwa, Madaktari hawatoshi, ni wachache; Manesi ni wachache; na Wataalamu wa Vifaa vinavyotumika hospitalini ni wachache au hawapo, wale ambao wanaweza kutunza vifaa na wale ambao wanaweza kufanya matengenezo pale ambapo vifaa vinaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu, nilikuwa naomba tu, katika suala hili la ajira, kwa kweli kada ya hawa watu ambao ni Madaktari, Manesi, Wataalam, Wafamasia na wengine wa Maabara kwa kweli waajiriwe kwa wingi ili wananchi wanapoenda hospitalini, hii isiwe ni changamoto kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba pia kuishauri Wizara kuangalia vifaa mbalimbali vinavyotumika katika hospitali. Kuna vifaa kwa mfano hematology machines, hizi ni chache, hebu Wizara iweze kuziangalia na kuziongeza. Kuna chemistry analyzers, kuna mashine za theater kama Anesthesia Machines, ventilators, na mashine nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi mashine wananchi wanazitumia, na wanapozikosa katika maeneo yao na wanapopewa referrals kwenda katika hospitali kubwa, inakuwa ni changamoto kwa sababu wananchi wengi hata uwezo wa kupata nauli hakuna. Kwa hiyo, naomba TAMISEMI iweze pia kuzingatia hivyo vifaa viweze kupatikana katika hizo hospitali na zahanati ambazo zimejengwa katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda pia kulishauri katika Wizara ya Afya ni eneo la mafunzo kazini. Manesi wengi wana umri mkubwa, wamesoma zamani, kwa hiyo, wakipata na nafasi ya kwenda kuhudhuria mafunzo yatawasaidia kwa sababu teknolojia inabadilika mara kwa mara, hata vitu mbalimbali vinabadilika. Kwa hiyo, naishauri Wizara iweze kutenga pesa ya watumishi kwenda kupata refresher courses ili waweze kuwa updated pamoja na mambo yanavyokwenda na magonjwa yanayoibuka mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda, naomba nigusie kwa haraka sana katika suala la elimu. Katika suala la Elimu ni dhahiri kabisa ya kwamba hata ukiwaweka wanafunzi katika hoteli ya five stars, kama wafanyakazi hawapo, kama walimu hawapo, watakaa, watakula na watapata kila kitu, lakini mwisho wa siku kama hawajafundishwa, ukiwa compare na wale ambao wamejifunza chini ya miti lakini walimu wapo, ni ukweli kabisa kwamba wale wa chini ya miti watafanya vizuri kuliko wale wanaokaa katika five stars hotel. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini? Namshukuru sana Rais kwa kujenga madarasa, kwa kujenga miundombinu, lakini waongezeke ili kuwe na balance ya wanafunzi wetu kufurahia mazingira na kufurahia walimu ili waweze kufaulu kwa kiwango kinachohitajika katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pia niweze kushauri juu ya miundombinu ya walemavu katika shule zetu. Walemavu wanapata shida hasa katika miundombinu kama vile choo. Kwa hiyo, naomba pale tunapoendelea kufanya kazi yetu vizuri, tuzingatie vyoo hasa kwa wale ambao wana ulemavu wa viungo. Vile vyoo kwa kweli usafi wake kuu- maintain ni ngumu. Kwa hiyo, at least wawe na vyoo vyao special ili nao waweze ku-enjoy fursa kama wanafunzi wengine ambao hawana ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kusema jambo moja kuhusu uzio. Naomba Serikali iweze kufikiria kujenga uzio katika shule zetu ili wanafunzi wetu waepuke vishawishi katika shule hasa wanapokuwa shuleni. Ule uzio utaweza kusaidia wasiweze kupata vishawishi nje ya maeneo ya shule. Wanapokuwa shuleni waweze kuzingatia kusoma tu na uzio japo hautamaliza, lakini utawazuia kutokutoka nje na kukutana na watu ambao nia zao siyo nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Nami naunga mkono hoja. (Makofi)