Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai na afya njema kwa siku ya leo na kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya na elimu. Sisi kama Wilaya ya Nyang’wale kwa fedha hizo ambazo mama ameweza kuzitoa kwa nchi nzima; na sisi kama Nyang’wale kwa mwaka 2022/2023 ametupatia zaidi ya shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya miradi ya maendeleo upande wa afya na elimu. Hongera sana mama, kwa kweli unafanya kazi kubwa, hongera sana, sisi tuko nyuma yako, kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya. Naipongeza Serikali kwa kuendelea kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyang’wale. Pia namwomba Mheshimiwa Waziri atenge fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo la Mkurugenzi wa Wilaya ya Nyang’wale ambaye hivi sasa anatumia jengo la Hospitali ya Wilaya na kumfanya DMO asiingie kwenye lile jengo. Kwa hiyo, tenga fedha ili ulikamilishe jengo la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’wale aweze kuhama aende kwenye jengo lake, na kumpisha DMO naye aingie kwenye jengo lake la utawala ili aweze kufanya kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo kwenye sekta ya afya hususan kwenye Hospitali ya Wilaya ya Nyang’wale, Vituo vya Afya na Zahanati, kwa kweli kuna uhaba mkubwa wa watumishi. Uhitaji wa watumishi ambao wanahitajika katika Wilaya ya Nyang’wale ni watumishi 841, lakini waliopo hivi sasa ni 193, sawasawa na asilimia 22. Kwa hiyo upungufu ukiuangalia hapo, ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwa mwaka huu wa fedha basi tupatiwe angalau hata watumishi 100 ili tuweze kupunguza gap lililopo pale. Kwa sababu ukiangalia 842 na 193 ni upungufu mkubwa sana. Waliopo kwa kweli wamechoka, lakini nawapongeza sana wanajituma na wanafanya kazi kwa moyo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zipo. Kuna wananchi walijitolea kujenga maboma ya Zahanati na maboma ya Vituo vya Afya, wametoa nguvu zao. Namwomba Mheshimiwa Waziri kupitia bajeti hii atenge fedha ili kwenda kuziunga mkono juhudi za wananchi wangu waliojitolea kwa ajili ya kujenga maboma ya zahanati pamoja na Vituo vya Afya ili kuwatia moyo, ili kwa mara nyingine hata ukiwaambia njooni tuungane pamoja watakuwa wako tayari kuliko hivi sasa wanatoa nguvu zao lakini Serikali haiwaungi mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya elimu, naipongeza sana Serikali. Kwa kweli Mama amefanya kazi kubwa kwa kipindi hiki kifupi, tumeweza kujenga madarasa mengi upande wa sekondari, madarasa mengi shule za msingi na pia kwa shule shikizi. Tumeweza kufungua sekondari tatu mwaka huu wa fedha. Kwa kweli tunampongeza Mama, anafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, palipo na mafanikio hapakosi kuwa na changamoto. Namwomba Mheshimiwa Waziri wetu aweze kutenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za Walimu kwa sababu kuna upungufu mkubwa, lakini pia atenge fedha kwa ajili ya kumalizia maboma ya vyumba vya madarasa ili kuwaunga mkono wananchi ambao walijitolea katika ujenzi huo wa maboma ya madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna upungufu mkubwa upande wa sekta ya elimu. Tuna upungufu wa walimu takribani asilimia 70 katika Wilaya ya Nyang’hwale. Ukweli Mheshimiwa Waziri jaribu kuangalia sana upungufu huo na hususan kwenye elimu ya sayansi na hisabati walimu ni wachache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa ushauri, naomba unisikilize vizuri. Ushauri huu jaribuni kuufanyia kazi. Naomba myafanyie uchunguzi magenge ya vyakula vinavyouzwa nje ya mageti ya shule zetu za sekondari na msingi. Vyakula vile na vinywaji siyo salama sana kwa watoto wetu. Pia ukiangalia maeneo haya, tayari kuna viashiria; mimi ni mmoja wa waathirika katika watoto wangu ama katika familia yangu, ameathirika na vinywaji hivi vya hapo shuleni, sasa hivi ni teja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, angalieni sana usalama wa chakula na vinywaji vya watoto kwenye magenge yaliyoko nje ya mashule. Jaribuni kufanya utafiti kwa kuwa pia ni vyanzo vya kuanza kufundisha watoto wetu mambo machafu kutokana na hizo Shilingi elfu moja moja na mia tano tano ambazo tunawa. Ukifika muda wa kwenda kula, kanunue pipi, kanunue mandazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakumbuka, Mzee Mkuchika anakumbuka, sisi tuliokuwepo zamani kidogo, tulikuwa tunafungiwa viazi, mihogo au mandazi, tunaondoka navyo nyumbani. Leo hii sisi tunaona watoto wetu ni bora umpe shilingi 1,000 aende akale chakula pale shuleni na chakula hicho kina madhara makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jaribuni kuchukua hata watoto kumi, mkawapime afya zao, utakuta watoto wanane wana matatizo kutokana na vyakula hivyo. Kama siyo Typhoid na maradhi mengine kutokana na hivyo vyakula. Hatujui vinatengenezwa kwa mfumo gani na nia zao ni zipi kutokana na hali iliyopo. Mheshimiwa Waziri chukua ushauri wangu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza TARURA, imefanya kazi vizuri sana katika Wilaya yangu ya Nyang’hwale. Mwaka huu wa fedha tunaoenda kuumalizia, 2022/2023 tumeweza kupokea zaidi ya shilingi bilioni 2.2. Pamoja na hayo, bado kuna matatizo kwenye Kata zetu. Naishauri Serikali iiongezee fedha TARURA ili aweze kufanya kazi vizuri kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna daraja ambalo linaunganisha kati ya Kata ya Kharumwa na Nyijundu, ni kilomita saba tu kati ya hizo Kata, lakini daraja hilo tumeshindwa kulijenga kwa sababu linahitaji fedha zaidi ya shilingi milioni 500. Nakuomba zitengwe Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kulijenga hilo daraja, barabara ile ifunguke. Kwa sababu barabara hiyo sasa hivi haitumiki, utakapotoka Kharumwa kwenda Nyijundu ni kilometa 30 kwa njia ya mzunguko, lakini ukitoka Kharumwa kwenda Nyijundu kwa njia ya mkato ni kilomita saba. Kwa hiyo, itasaidia sana kuinua uchumi wa wa Nyang’hwale, lakini kwa sababu tumejenga Hospitali ya Wilaya, ni karibu sana kuleta wagonjwa kwa njia ya mkato, kutoa wagonjwa wilayani na kupeleka Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili kwa ajili ya kutuongezea fedha tuweze kujenga hilo daraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)