Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Minza Simon Mjika

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mambo makuu ambayo ameendelea kutupatia. Tuna afya njema na ndiyo maana tuko hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika nchi yetu ya Tanzania. Wala haina sababu ya kueleza, wote tuanaona mambo makuu ambayo anaendelea kuyafanya. Vilevile namshukuru dada yangu, Waziri wa TAMISEMI kwa ajili ya kazi nzuri ambazo anaendelea kufanya pamoja na Naibu Mawaziri. Endeleeni kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwa upande wa TARURA; TARURA ni watu ambao wanafanya kazi vizuri sana. Barabara zetu zimefunguka, ziko vizuri, japokuwa ni za changarawe, lakini tunaenda vizuri utadhani ni barabara ya lami, tunashukuru kwa hilo. Tunapenda kumshukuru sana kiongozi wetu wa mkoa, Meneja wa TANROADS Gaston Gasana anafanya kazi nzuri sana, ikiwa ni pamoja na Mkuu wetu wa Mkoa anafanya kazi nzuri sana, anasimamia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya, namshukuru Rais wetu ametupatia hospitali kubwa mbili tena za wilaya; Wilaya ya Itilima na Wilaya ya Busega. Meatu, Maswa pamoja na Bariadi tuna hospitali hizo za muda mrefu na zina vifaa, tunashukuru sana kwa kazi nzuri ya Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hizi mbili ambazo zimejengwa bado ni mpya na bado ni changa zinahitaji wafanyakazi wa kutosha, tunaomba tupate wafanyakazi katika hospitali hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vifaa vya kufanyia kazi katika hizo hospitali, tunaomba vifaa vipatikane kwa ajili ya kazi hiyo. Vinginevyo ninapenda tu nimshukuru sana Mama kwa kazi nzuri ambazo anaendelea kufanya. Wafanyakazi ni wachache sana katika hospitali, kwa mfano Mkoa wa Simiyu una asilimia 33 ya wafanyakazi mkoa mzima una wafanyakazi 1,500 tu. Kwa hiyo, tuna upungufu wa asilimia 65, ni upungufu ambao ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Waziri wa TAMISEMI, Dada yangu Angellah jitahidi sana kutupatia wauguzi katika Mkoa wa Simiyu. Tunawapenda sana kazi mnazozifanya lakini tunaomba tuongezewe wafanyakazi. Nadhani ajira zimetangazwa nyingi tunaomba basi na sisi katika mkoa wetu tuweze kupatiwa wafanyakazi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ninahama hapo naenda upande wa barabara, kuna barabara ambayo imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana, Kolandoto – Lalago inapita mpaka Kishapu – Lalago mpaka Meatu. Barabara ile iko katika Ilani na ni ya muda mrefu, miaka mingi. Tunaomba mtupatie lami na sisi ili nasi tujisikie kwamba ni miongoni mwa Watanzania, kutoka Meatu mpaka Kolandoto tunaomba tupate barabara ya lami lakini pia kuna barabara inayotoka Bariadi inapita Itilima – Meatu mpaka Singida. Tunaomba barabara ile pia tuwekewe lami. Tunahangaika sana barabara ile ni nzuri sana na ni shortcut nzuri haina sababu ya kuzunguka Mwanza au Shinyanga tukishatengenezewa ile barabara magari mengi yatapita pale na uchumi wa nchi yetu utaendelea kuwa juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naingia upande wa elimu, ninashukuru Rais wetu ametupatia madarasa mengi ya kutosha. Sekondari na primary madarasa ni mengi tu yanatosha vizuri lakini tatizo ni moja, changamoto hatuna walimu wa kutosha. Walimu ni wachache sana, wanafunzi ni wengi ndio wanakaa kwenye madarasa lakini hata yale madarasa yana upungufu tena wa madawati. Tunaomba wanafunzi wakae katika sehemu ambazo ni nzuri ili anapojifunza basi ajisikie vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia tunaomba walimu muwasaidie waweze kupata na wawe na ofisi za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho napenda niseme ni kwa upande wa maji. Katika Mkoa wa Simiyu tunachangamoto kubwa sana ya maji. Maji ni tatizo sana yaani wakinamama wa Mkoa wa Simuyu, kina baba tunahangaika sana juu ya maji. Tunaomba msaada mkubwa ambao ni mwarobaini utakaotibu hili tatizo ni kupata maji ya kutoka Ziwa Victoria.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hili mlifanyie kazi, TAMISEMI tusaidieni sana Mkoa wa Simiyu tunahangaika sana hasa Wilaya ya Meatu. Wilaya ya Meatu haina vyanzo vya maji muda mrefu tumekuwa tukihangaika tukilia. Nadhani Mheshimiwa Angellah ulifika katika Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Meatu uliona changamoto iliyoko kule ni shida huwezi hata ukapanda miti ukamwagilia. Tuna ukame wa hali ya juu sana lakini hata vile visima tulivyonavyo tena tembo wanashambulia yale maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba mtusaidie tunapoongea namna hii kweli masikitiko ukifika katika Mkoa wa Simiyu hizo wilaya zina changamoto kubwa sana, tunaomba Serikali iweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho napenda nikiiongee hapa ni kwa upande wa walimu, nirudi samahani kule, walimu wengi wanadai malipo ya muda mrefu, wameenda likizo hawajapewa pesa zao na wengine wanachangamoto nyingi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwa upande wa elimu muweze kuwasaidia. Mwalimu anafanya kazi kubwa sana unajikuta mwalimu mmoja anaweza akafundisha watoto 140 darasa moja mwalimu pekee yake lakini bado hata yale malipo yake ni shida anapoeenda likizo hapati chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna upungufu wa nyumba za walimu, walimu wengi wanaishi mijini shule zao zipo vijijini unajikuta kutoka mjini mpaka kijijini kule ni kilometa saba. Mwalimu aende na kurudi kilometa 14, tunaomba walimu wa kutoka kule kwetu Mkoani Simiyu tupate walau hata kila shule hata nyumba kumi kumi za walimu waweze kukaa karibu na mazingira ya shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda niseme kuhusu upungufu sasa wa hivo vifaa katika hizo hospitali nilizozisema nadhani hilo nimeliongea na ninaamini kwamba nimeelewaka. Napenda kushukuru, naishia hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)