Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI. Moja kwa moja niende kwanza kwa kuimpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameendelea kufanya kazi kubwa katika Taifa hili lakini kwa jinsi ambavyo ametugusa sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa kutupatia hospitali za wilaya katika kila halmashauri. Sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi tumebahatika kupata hospitali zenye level ya wilaya katika kila halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hopsitali hizo za wilaya ambazo tunazo katika halmashauri zetu hospitali nyingi zinashindwa kufanya kazi kwa masaa 24 kutokana na upungufu mkubwa sana wa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hospitali kama hospitali ya Halmashauri ya Msimbo lakini Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika lakini Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe, Hospitali ya Wilaya ya Mlele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hizi kwa kweli zina operate kwa level ya zahanati. Kama Serikali ni lazima tuhakikishe kwamba fedha hzi nyingi zilizowekezwa na Serikali katika hospitali hizi zinaenda kutumika vizuri kwa kupeleka watumishi ili wananchi waliokusudiwa waweze kupatiwa huduma iliyobora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Katavi kwa upande wa upungufu wa watumishi kwa upande wa afya pamoja na elimu. Tunaupungufu wa watumishi kwa asilimia 56.18. Kwa upande wa Wilaya ya Tanganyika tunaupungufu wa asilimia 66, katika Wilaya ya Mlele tuna upungufu wa asilimia 61 upande wa Nsimbo tuna asilimia 63.2, upande wa Mpanda Mjini tuna upungufu wa asilimia 36.1 na upande Mpimbwe tunaupungufu wa asilimia 69.1. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu huo ni mkubwa na wananchi wanakutana na adha mbalimbali kutokana na kwamba wanashindwa kupatiwa huduma Serikali iliyokusudia kwa kujenga hospitali hizo za wilaya katika Mkoa wetu wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naipongeza Serikali kwa kuleta pesa nyingi katika kuwekeza katika vituo vya afya pamoja na zahanati. Katika Mkoa wetu wa Katavi tuna zahanati nyingi ambazo Serikali imeziwekeza, hadi hivi ninavyoongea kuna zahanati zaidi ya 16 ambazo zimeshindwa kufuguliwa kutokana na upungufu mkubwa sana wa watumishi na kufikia mwezi wa Sita tutakuwa na zahanati zaidi ya 26 ambazo zinashindwa kufunguliwa kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vituo vya afya, kuna vituo vya afya ambavyo vimejengwa ikiwepo Ilunde, Majimoto, Mwamapuli, Gulamata na kwa upande wa Kibaoni. Zahanati hizi na vituo vya afya nyingi zinashindwa kufanya huduma ya upasuaji na matokeo yake wagonjwa wengi wakienda pale wanapatiwa tu paracetamol. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali kupitia Wizara hii ya TAMISEMI, kwa kuwa tumepata ajira 21,000. Tunaomba wananchi wa Mkoa wa Katavi tuweze kukumbukwa tuangalie wanaopata adha hapa sana sana ni mama zangu wa Mkoa wa Katavi. Unakuta kituo kama hiki Kituo cha Afya cha Kibaoni, cha Kasansa na Majimoto, vinashindwa kufanya huduma ya upasuaji. Sote tunaelewa wakina mama wengi wanapoenda kujifungua kuna wengine wanatakiwa wafanyiwe upasuaji lakini zahanati hizi na vituo vya afya havifanyi huduma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Waziri wa TAMISEMI aliangalie kwa jicho la pili suala hili wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kupelekewa watumishi ili waweze kuhudumiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambapo nilikuwa napenda kulichangia, katika ajira na usawa, natokea katika mikoa ambayo ipo pembezoni. Mfano Mkoa wetu wa Katavi, kuna Mkoa wa Kigoma lakini kuna Mkoa kama wa Lindi. Watumishi wengi wanapopangiwa maeneo haya wanashindwa kuja kufanya kazi kutokana pengine na miundombinu ambayo hawaijawa supported. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara iweze kuboresha mazingira ya walimu pamoja na watumishi hususan wa afya ili wanapokuja kupangiwa katika maeneo haya waweze kufanya kazi katika mazingira yaliyobora ili wasiweze kutukimbia. Kwa kweli unakuta wafanyakazi wanapopangiwa katika mikoa hii kwa mfano Mkoa wangu wa Katavi unakuta mtu amepangiwa eneo la Gulamata lipo upande ule wa Mishamo. Ni eneo ambalo ni mbali usipomuwekea miundombinu mizuri, mtumishi huyu lazima ataomba kuhama aweze kuhamia maeneo mengine. Ila tukiwawekea mazingira rafiki na mazuri lazima watumishi hawa watakaa waweze kufanya kazi na kusaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nilikuwa napenda kuchangia ni kuhusiana na kuboresha kitengo cha wakaguzi wa ndani. Katika kuboresha kitengo hiki cha wakaguzi wa ndani linaweza likamsaidia sana CAG. Kitengo hiki kimekuwa kwanza hakitengewi bajeti ya kutosha lakini pia wanakosa uhuru kutokana na kwamba wanafanya kazi kubwa ambayo wanakuwa wanamuangalia Mkurugenzi aweze kuwapatia mafuta lakini wanamuangalia Mkurugenzi ndio aweze kuwapatia magari ya kwenda kufanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Serikali waboreshe kitengo cha wakaguzi hawa wa ndani ili waweze kudadavua na kutoa madudu yote ya pesa zinazoliwa katika halmashauri zetu. Tukiwawezesha hawa wakaguzi wa ndani kwa kweli kazi kubwa itafanyika katika halmashauri zetu na fedha zote zinazopelekwa na Serikali ziitaweza kusimamiwa ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi naunga mkono hoja.(Makofi)