Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hii ya Wizara ya TAMISEMI. Kiukweli niseme tu kwamba nilikuwa najaribu kupitia pitia taarifa ya Mheshimiwa Waziri, lakini mengi niliyokuwa nikiyapitia sioni yale ambayo nilitamani kuyasema. Mimi nitasema ya kwangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie nilipoishia kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu kuhusiana na suala zima la hizi shule kongwe. Nadhani hapa sasa leo ndiyo hasa sehemu yenyewe. Niiombe sana Wizara ya TAMISEMI na kwa bahati nzuri wakati tunatembelea miradi tulikuwa na Mheshimiwa Dugange, anajua nilichoomba na naendelea kusisitiza kwenye taarifa hii hapa sasa hivi. Hebu tujitahidi, ni aibu kubwa shule kongwe ambayo hata Baba wa Taifa amesoma, inatia aibu. Naomba sana wasitegemee sisi Tabora eti mapato ya ndani yaweze kufanya karabati za shule zetu kongwe, haiwezekani kwa sababu hatuna fedha hiyo, kutokana na mapato yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shule hizo niongelee hata shule nyingine za msingi. Tuna Shule moja inaitwa Town School. Hii shule imeanzishwa mwaka 1940, ujenzi wa shule hii umetumia mawe. Hapa ninavyozungumza shule imechoka kweli kweli. Sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mambo ya kuja Tabora waje watupe pole watoto wetu kule wameangukiwa na madarasa, jamani hatutaki. Kinga ni bora kuliko tiba. Nawaomba sana pamoja na shule nyingi kuwa kongwe na zina changamoto, lakini naomba hii Shule ya Town School waiangalie kwa jicho la peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombeni sana na niombe mbele ya Bunge hili tukufu mambo ya kuja kupeana pole, hapana. Tunaomba watusaidie hii shule ni ya toka mwaka 1940, ina changamoto, imechakaa sana na iko kati kati ya Kata yetu ya Gongoni. Kwa hiyo niombe sana Wizara iangalie hizi shule kongwe na hizi za msingi maana walikuwa wanahangaika na shule za sekondari na hizi za msingi nyingi zimechoka sana. Kwa hiyo tunaomba sana waweze kuzifanyia ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombee TARURA fedha. TARURA inahitaji kuongezewa bajeti. Mimi natoka Mkoa wa Tabora na hapa naomba nizungumzie hususan kwenye Jimbo ambalo natokea mimi la Tabora Mjini. Kwenye kata zetu kuna mitaa mbalimbali, kuna vijiji na kuna vitongoji. Barabara hazipitiki, leo nikikwambia hizo kata zetu za mjini barabara nyingi za ndani kwenye mitaa yetu ni barabara za vumbi. Hazina mitaro, mvua ni nyingi zikinyesha maji yanaingia kwenye nyumba za watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana wakati wanafikiria kununua magari ya ma-DC na ma-RC na watu wengine, tunaomba sana bajeti iongezwe kwenye TARURA. Wananchi wetu wanateseka, wanapata shida. Mvua zikinyesha maji yanaingia ndani. Sisi hatukatai ununuzi wa magari, wanunuliwe kwa sababu ni watendaji, lakini watapita wapi huko hawa ma-DC kama barabara ni mbovu. Lazima wawatengenezee na barabara kwanza ili yale magari watakapowanunulia waweze kupita kwenye sehemu salama. Wapunguze bajeti kidogo wazipeleke kwenye TARURA ili hawa watu waweze kufanya kazi vizuri jamani, wananchi wetu wanalalamika. Barabara za mitaani nyingi ni mbovu na especially sasa hivi mvua ndiyo zimekatika, wawape hizo fedha watu wa TARURA ili waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie juu ya hii miradi ya afya ambayo haikamiliki, ni aibu kubwa. Amezungumza Mheshimiwa Mbunge wa Itilima, Mheshimiwa Njalu. Amesema, hizi fedha wanazopeleka kwa maelekezo wanakosea. Maeneo mengine wananchi wameshatumia nguvu kubwa ya kujenga zahanati, vituo vya afya, wakiwapelekea fedha shilingi milioni 500 hii eti nendeni mkajenge kituo cha afya wanacha yale majengo waliyokuwa wameshayajenga, wanaenda kujenga majengo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepita huko Naibu Waziri wa TAMISEMI anajua, kuna majengo mengine ya afya yamekaa mpaka yameshachakaa hayajatumika kwa sababu ukiwauliza wameanza kujenga miradi mipya kwenye maeneo hayo badala ya kuwa wamepewa fedha ama TAMISEMI waulize kwenye maeneo wanayopeleka fedha, je, mnahitaji kujenga vituo vya afya maeneo gani na maeneo gani? Mnahitaji kujenga hospitali za wilaya zipi na zipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta hospitali ya wilaya tayari ilishajenga majengo saba, Serikali imepeleka fedha ya kujenga majengo mengine matatu. Yale saba yanaachwa, yanajengwa yale matatu ambayo zile fedha wamepeleka. Kwa nini zile fedha wasiwaambie kwamba wamalizie yale majengo ili watu waweze kupata kutumia hayo majengo. Fedha nyingi za Serikali zinazopelekwa, Mheshimiwa Rais anapeleka fedha nyingi lakini hazina thamani kwa wananchi kwa sababu hawatumii miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kidogo kwenye elimu wanajitahidi kwa sababu tunaona watoto wetu wanasoma madarasani lakini hawana madawati. Kuna mikoa ambayo unapita kuna baridi ya hatari. Sisi tumeenda Sumbawanga huko Rukwa, tumeenda Katavi kuna baridi kweli kweli. Wanajenga madarasa mawili mnatoa madawati 30, kila darasa madawati 15, 15. Darasa gani la Tanzania ambalo watoto wanakaa 45? Darasa moja watoto 100, watoto 70 watoto wote 40 unakuta wamekaa chini na baridi iliyoko katika mikoa hiyo mpaka unasikia huruma wewe mzazi tumbo linakucheza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe wakati huu ambapo wako kwenye bajeti waweke bajeti wasaidie halmashauri zetu waweze kupata madawati. Pamoja na halmashauri zetu kujikongoja, lakini bado Serikali inatakiwa isaidie wananchi wetu, kule watoto wetu wa Kitanzania waweze kusoma wakiwa wamekaa kwenye madawati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala la hii 10%. Ni aibu kubwa, amezungumza Mheshimiwa Halima hapa na ndiyo ukweli ulioko huko chini. Hizi fedha hazijapotea hizi zipo. Kuna maeneo tumekwenda kuna kikundi cha familia; baba, kaka, mtoto wa baba mkubwa, mtoto wa mjomba, mtoto wa nani. Wamekaa sasa pale ehee, biashara gani ambayo mnafanya tunawauliza, wanaanza ooh, vikaenda vikarudi, vikafanyaje. Wamepewa zaidi ya shilingi milioni 30. Hiyo fedha inarudi na nini? Unawauliza wamebaki hawa, wawili. Sasa hawa wengine wako wapi? Wameingia mitini. Unamuuliza Afisa Maendeleo ya Jamii wakati unakuja kukikagua hiki kikundi ulijua kwamba hawa watu wakoje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha kupitia Bunge lako Tukufu tunataka pamoja na kusimamisha mikopo ya 10%, hizi fedha kwanza zirudi. Zirudi fedha hizi za Watanzania walipakodi, wavuja jasho, halafu ndiyo tuanze mpango mzima wa kuhakikisha tunaanza kugawa tena hizi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla hatujaanza kugawa fedha hizi huko kwenye halmashauri wapelekwe wataalamu wa fedha kwenye vikundi hivi ili waweze kusaidia wananchi wetu kujua miradi. Hawa maafisa maendeleo wa jamii mnaowapelekea hizi kazi si za kwao; na ndiyo maana maeneo mengi wamefeli kwa sababu hawana ushauri mzuri kwa vikundi wafanye biashara gani ili waweze kutoa marejesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ajirini maafisa maendeleo ya jamii kwenye maeneo husika, na mnapoajiri msiajiri kwa upendeleo. Tumekwenda eneo moja jimbo lina kata 19, maafisa maendeleo wa jamii wako 43 wako kwenye jimbo moja. Katika mkoa huo kuna jimbo lina kata 27 lina maafisa maendeleo ya jamii wawili, kuna jimbo lingine kina kata 27 maafisa maendeleo wa jamii watatu. Sasa kata 27 zinafanywaje kazi maafisa maendeleo ya jamii 23? Hapo ndipo utakapoona huu ubabaifu wa hizi fedha unapoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha nyingine, watendaji wetu wasiokuwa waaminifu wa TAMISEMI, wanachukua fedha hizi kwa visingizio vya vikundi halafu wanazichukua wao wenyewe. Ndiyo maana tunasema hili Bunge tusikubali fedha hizi zipotee, hizi fedha lazima zirudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme, namshukuru Mheshimiwa Spika kwa kunipangia kwenye kamati ya LAAC, nitakuwa nasema kila siku hizi fedha mpaka zirudi ndipo zitoke fedha zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.