Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa rehema kwa kunijali afya na kunipa kibali cha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba niunge mkono hoja. Napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri Angellah Kairuki, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa TAMISEMI kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM, nampongeza sana Rais wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kusahau ninaomba nimwombe Mheshimiwa Waziri; kwanza nimpongeze kwa kuajiri walimu na watumishi wa afya. Baada ya hapo niombe ombi maalum, naomba watumishi waalimu na wa kada ya afya waletwe Mkoa wa Kigoma, Kigoma ya sasa si ya zamani. Sasa hivi tuna barabara na zinaendelea kujengwa, lakini pia tumeshapata umeme wa grid ya Taifa; kwa hiyo Kigoma ni maeneo mazuri ya kuweza kuishi watumishi kwa sasa. kwa hiyo tunaomba mtuletee watumishi, Kigoma sasa hivi tuna barabara na tuna umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza kwa jinsi vituo vya vilivyojengwa zahanati, hospitali za wilaya, vilevile hospitali za mikoa zikakarabatiwa na nyingine zikapatiwa hadhi ya kuwa hospitali za rufaa, ikiwemo na Hospitali ya Mkoa wetu wa Kigoma. Ombi maalum; ninaomba mtuletee watumishi. Kwa mfano katika Wilaya ya Kasulu tumeweza kupatiwa fedha bilioni 3.6, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, lakini tulipata msaada kutoka kwa wadau milioni 500 kwa ujenzi wa nyumba za watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nyumba tunazo na miundombinu ni mizuri. Tumepata vifaa vya thamani ya bilioni 1.5 kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Kasulu DC ambayo ni Hospitali mpya ya Wilaya ya Halmashauri ya Kasulu DC. Hivyo basi changamoto tuliyonayo ni kwamba hatuna watumishi, hatuna wataalamu wa mionzi, maabara na huduma ya meno. Kwa hiyo tunaomba tupatiwe wataalam angalau hata watano kuja katika Halmashauri ya Kasulu DC kwa sababu hospitali hiyo ni mpya inahitaji wataalam wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ombi moja; Kata ya Kagera Nkanga ipo kilometa 80 kutoka Makao Makuu ya wilaya; ninaomba tujengewe kituo cha afya kwa sababu ni kutoka kituo hicho kuja mjini kilometa 80 tunaweza kuangalia ni kwa umbali gani. Wanawake wanapoteza maisha kwa ukosefu wa huduma ikiwemo kupoteza damu nyingi wanapokuwa wamecheleweshwa kufikishwa kwenye hospitali ya wilaya. Si hivyo tu, eneo hilo kuna majambazi wanateka sana katika aneo hilo la kutoka Kagera Nkanda kuja Kasulu au Kasulu kwenda Kagera Nkanda, kilometa 80. Angalia, kilometa zote hizo kwenda kufata huduma eneo lingine tunaomba kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Buhigwe, wilaya anayotoka Makamu wa Rais, na wakati alipokuwa akigombea, alienda katika Kata ya Mkatabnga akashuhudia wananchi wametumia nguvu wameshaanza kujenga jengo la kituo cha afya. Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Angellah Kairuki nakuomba sana, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa wananchi wameshajitolea wameshaweka msingi wana matofali ya akiba, nakuomba mama yangu utupatie kituo cha afya katika Kata ya Mkatanga Kijiji cha Kitambuka. Nakuomba sana utusaidie kwa sababu wananchi wameshaonesha njia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa Mheshimiwa Waziri ninaomba uiangalie TARURA kwa macho ya huruma kwa sababu, kwa mfano sisi Mkoa wa Kigoma hatuna mgodi wa dhahabu, wananchi wetu ni wakulima na kilimo kinafanyika shambani. Tunaomba utupatie pesa ili barabara zinazoenda mashambani barabara zinazounganisha vijiji na vijiji, barabara zinazosafirisha mbolea kupeleka mashambani ziweze kujengwa kwa mfuko wa TARURA. Kwa hiyo tunaomba TARURA waongezewe pesa barabara zinazoenda mashambani zinazounganisha vijiji vyetu ziweze kujengwa na kupitika kiurahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)