Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kwanza kumshukuru kabisa kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani kubwa aliyokuwa nayo kwangu na kuniteua kushika dhamana hii. Pia nimshukuru na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile nichukue fursa hii kuishukuru familia yangu na Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo ananiongoza vizuri, nafanya nae kazi kwa karibu sana na pia kwa ushirikiano wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukurani hizo, naomba sasa nichukue fursa hii kuweza kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizokuwa zimewasilishwa leo hii na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako hili Tukufu. Naomba nianze na hii hoja ya makazi ya askari pamoja na vitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii imezungumzwa ama imechangiwa kwa maandishi na kwa kuzungumza na wachangiaji wengi, lakini nitawataja wale ambao nimebahatika kuwabaini. Mheshimiwa Hamidu Bobali, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mheshimiwa Kiula, Mheshimiwa Masare, Mheshimiwa Kigula, Mheshimiwa Kingu, Mheshimiwa Shekilindi, Mheshimiwa Komanya, Mheshimiwa Omari, Mheshimiwa Kangi Lugola na Mheshimiwa Kingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika kwamba majeshi yote takribani yana changamoto kubwa sana ya makazi ya askari pamoja na vitendea kazi na kimekuwa hiki ni kilio cha Waheshimiwa Wabunge takribani cha muda mrefu. Tunakiri juu ya changamoto hii na ndiyo maana hivi tunavyozungumza, kuna mipango kabambe ya Serikali ambayo inalenga kuhakikisha kwamba inapunguza matatizo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jeshi la Polisi, tayari kuna utaratibu wa kujenga nyumba takribani 4,136 ambapo zinatarajiwa kujengwa kupitia mkopo wa Serikali ya China kupitia EXIM BANK. Wakati huo huo kuna Ujenzi wa makazi ya nyumba za askari Mabatini-Mwanza ambao zinachukua familia 24, Buhekela - Kagera familia 12, Musoma - Mara familia 24, Ludewa - Njombe familia 12. Aidha, Serikali imejenga nyumba 22 za maafisa wa Mikocheni ambazo ziko Mikocheni na maghorofa 22 ambayo yatakuwa Kunduchi pale kwa ajili ya familia 333 za askari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa magereza, pia kuna mchakato wa kujenga nyumba takribani 9,500 lakini pia kwa upande wa vitendea kazi kwenye Jeshi la Polisi kuna mradi ambao programu ya kuleta magari 777 ya aina mbalimbali, miongoni mwao yameshaanza kufika na mengine yatakuja hatua kwa hatua, ni magari ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa upande wa Jeshi la Zimamoto katika bajeti yetu hii kwenye bajeti ya maendeleo tumetengewa takribani shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuongeza magari mawili ya kuzimia moto. Kwa hiyo, hizo ni miongoni mwa hatua ambazo tayari Serikali imeanza kuchukua kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya masuala haya ya vitendea kazi pamoja na makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna hoja ambayo imechangiwa na wajumbe wengi wakiwemo Mheshimiwa Mohamed Amour, Mheshimiwa Msigwa, Mheshimiwa Lwakatare, Mheshimiwa Kiula, Mheshimiwa Masoud, Mheshimiwa Yusuf, Mheshimiwa Mukasa, Mheshimiwa Kaiza, Mheshimiwa Anatropia na wengineo. Hoja hii zaidi ilikuwa inazungumzia kuhusiana na kubambikiwa kesi, wamelishutumu sana Jeshi la Polisi kwamba limekuwa likibambikia kesi, lakini nichukue fursa hii kuwapongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ambayo wanafanya katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya pongezi hizo ambazo nawapa Jeshi la Polisi, haiondoi ukweli kwamba kuna askari wachache sana, nasisitiza kwamba ni wachache sana ambao wamekuwa wakichafua taswira nzuri ya Jeshi la Polisi miongoni mwa wananchi na hatua nyingi zimechukuliwa katika kukabiliana na askari wa namna hii. Kuna mikakati ya kijumla na mikakati mingine ya mmoja mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati iko mingi, siwezi kuitaja yote, lakini wameweza kutoa mwongozo wa mara kwa mara kwa Wakuu wa vituo na Wakuu wa Upepelezi kuwa makini sana kwa majadiliano na mashauri yanayofunguliwa na kutoa maelekezo kwa wapelelezi wa kesi ambao watasaidia kufuatilia mwenendo wa kesi hizo. Pale ambapo askari wamegundulika kufanya matatizo kama hayo ya upendeleo, basi wamekuwa wakichukuliwa hatua za kinidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kesi moja ambayo inazungumzwa sana ambayo Mheshimiwa Kiula aliizungumza baada ya kufanya ziara ya Kamati katika gereza hapa Dodoma, lakini kesi hii hii na mimi naifahamu vizuri. Tumekuwa tuna utaratibu mzuri kupitia Mheshimiwa Waziri wangu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwakyembe kwa kufanya kazi kwa pamoja. Wakati huu niliweza kumwakilisha Mheshimiwa Waziri kufanya ziara katika lile gereza na kumshuhudia huyu msichana ambaye anazungumzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli msichana huyu alikatwa vidole viwili vya miguu na viwili vya mikono na baada ya kukatwa vidole hivi vya mikono yeye ndiyo akafungwa miaka minne. Ni jambo ambalo linasikitisha sana. Hizi ziara tumekuwa tukizifanya katika maeneo mbalimbali tunapopata fursa, tumefanya katika magereza mengi ili kuweza kubaini kama kuna wananchi ambao wamekuwa wakibambikiziwa kesi ili hatua za haraka zichukuliwe na tumechukua hatua nyingi tu.
Katika hatua specific ambayo ameizungumza Mheshimiwa Kiula kwa huyu msichana ni kwamba, mpaka sasa hivi tunavyozungumza wale watu ambao walimkata kidole wameshafungwa, wamehukumiwa kufungwa nadhani miaka mitatu kama sikosei au minne tunavyozungumza sasa hivi. Pia ile kesi yake ambayo alibambikiwa ya kuvunja nyumba nayo imefutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wale askari ambao walishiriki kwa namna moja ama nyingine kutomtendea haki huyu kijana tumeagiza wasimamishwe kazi mara moja na wachukuliwe hatua za kisheria. Kwa hiyo, kazi hii tumekuwa tukiifanya kimya kimya kuweza kutembelea kwenye magereza mbalimbali na kuweza kubaini watu ambao wanabambikiwa kesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusiana na hoja hii malalamiko yamekuja upande wa masuala ya kisiasa. Mimi niseme tu kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu. Katika kutimiza wajibu wake, wananchi tunapaswa kuwapa ushirikiano. Unapotakiwa na askari kutii lazima utii, wanaita sheria bila shuruti. Askari anapokuambia umefanya kosa fulani akakukamata basi ufuate sheria usilazimishe askari kutumia nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya masuala yamezungumzwa sana lakini niseme kwamba Jeshi la Polisi limechukua hatua mbalimbali kulingana na taarifa ambazo imezipokea. Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakilalamika hapa mara nyingi kwamba kuna jambo fulani limetokea, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa lakini ukimuuliza umepeleka taarifa hizo katika kituo gani cha polisi, hakuna. Kuna taarifa nyingi ambazo Jeshi la Polisi limezichukua na kuzifanyia kazi kwa sababu tuna lengo la kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kubakia katika amani na utulivu hasa kipindi cha uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, mnakumbuka wakati wa uchaguzi hasa Zanzibar kuna matukio mengi ya uvunjifu wa amani yalikuwa yametokea. Kuna watu waliua wanyama, walichoma mashamba, walipiga nyumba alama ya “X”, wamechoma nyumba za watu, wamechoma maofisi ya vyama na wametega mabomu. Katika hali kama hii mnatarajia kwamba Jeshi la Polisi likae kimya? Ni Serikali gani ambayo itakubali amani ya nchi inachezewa halafu ikabakia kimya? Yaliyofanyika ni kuhakikisha kwa mujibu wa taarifa zilizopo na uchunguzi uliofanyika kuwakamata watuhumiwa mbalimbali, kufanya upelelezi na kuweza kuwafikisha panapostahiki na panapostahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu ni kwa DPP ili baadaye waweze kupelekwa mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamefanyika sina haja ya kuyarudia kuyazungumza hapa. Nashukuru leo hayajazunguzwa kama kipindi kilichopita lakini nilikuwa nimejiandaa kwelikweli maana nina ripoti ambayo ni very comprehensive ina ushahidi wa kila jambo ambalo limefanyika ambapo watu wanaolalamika humu ndani leo ndiyo wafuasi wao walikuwa mstari wa mbele kufanya mambo hayo, lakini leo wamekimbilia kwenye hoja nyingine. Mimi niseme tu kwamba tusaidiane, kama kuna mambo ambayo mnaona hayajachukuliwa hatua na ni matendo ya kihalifu yote yataweza kufanyiwa kazi ili mradi muwasilishe katika sehemu stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna jambo lingine limezungumzwa hili suala la mashehe. Wanasema kuna mashehe wamekamatwa kwa nini wanashtakiwa Dar es Salaam lakini kwa nini mashehe hawa wamedhalilishwa. Kwa ufupi kabisa kwa kuwa muda haupo, niseme tu kwamba mashehe hawa wameshtakiwa kwa makosa ya kigaidi…
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Makosa haya yamefanyika Tanzania Bara. Ndiyo maana walipokwenda kuhukumiwa Zanzibar wakasema haya makosa yamefanyika Tanzania Bara kwa hiyo wakaletwa Tanzania Bara kwa sababu ndiyo walifanyia huku makosa.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Sasa wanasema wamedhalilishwa, naomba niweke mezani ripoti hii ya uchunguzi ambapo walipelekwa hospitali, wakafanya uchunguzi hakuna hata mmoja alionekana ana uthibitisho wowote wa kudhalilishwa. Ripoti hii hapa naiweka mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie sasa katika hii hoja ya wahamiaji haramu ambapo wachangiaji wengi wamechangia lakini kutokana na muda naomba nisiwataje. Ni kweli tulifanya operesheni, ilikuwa ni operesheni kabambe ambayo ilianzia tarehe 24 Disemba mpaka tarehe 31 Januari. Katika operesheni hii tulifanya mambo kadhaa ikiwemo upelelezi, doria, misako, ukaguzi na kadhalika. Mafanikio tuliyoyapata ni makubwa sana ambapo takribani wahamiaji haramu 3,339 kutoka mataifa 33 wameweza kukamatwa. Aidha, hatua mbalimbali zimechukuliwa dhidi ya wahamiaji haramu hawa, wengine wamerudishwa majumbani kwao, wengine walikuwa wakimbizi wakarudishwa makambini, wengine wamepigwa PI Notice wameondoshwa, wengine wameamriwa kuondoka na wengine wanaendelea kuchunguzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili lilikuwa na mafanikio makubwa kwani tumeweza kufanikiwa kukusanya takriban dola za Kimarekani laki moja na tisini na kitu elfu ambazo zilipatikana kupitia special visa kwa ajili ya wahamiaji haramu 317 ambao walikuwa wanaishi kinyemela. Vilevile zoezi limesaidia sana kuibua mwamko na hamasa kwa wananchi kuhusiana na madhara ya kukaa na wahamiaji haramu. Ndiyo maana tumeweza kupata karibu taarifa 750 kutoka kwa raia wema zilizoweza kusaidia kuwakamata hawa wahamiaji haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wageni walio wengi wanafuata sheria na ndiyo maana tunasema kwamba baada ya operesheni hii kabambe tumekuwa na mfumo mzuri wa kuwashughulikia. Hivi ninavyozungumza nadhani kesho watendaji wa Idara ya Kazi watafika hapa na watendaji wetu wa Idara ya Uhamiaji wako hapa tutakaa pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kazi ili tuweze sasa kuwa na mkakati wa pamoja wa kufanya zoezi letu liwe endelevu. Mkakati huu utasaidia sana kuendeleza mafanikio makubwa ambayo tumeyapata.
Mheshimiwa Mweyekiti, kulikuwa na hoja nyingine ambayo inazungumzia hili suala la zimamoto. Wachangiaji wengi wamelalamika hapa kwamba mara nyingi moto unapotokea kwenye majengo marefu kikosi chetu hakina uwezo. Mheshimiwa Lucy Owenya alisisitiza sana hoja hii katika mchango wake wa maandishi na wachangiaji wengine walisisitiza kwamba unapotokea moto katika majengo marefu kikosi chetu cha zima moto hakina uwezo wa kuzima moto, ni kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza kwa mujibu wa vitendea kazi ambavyo tunavyo, tuna gari ambayo yanaweza kufika mwisho ghorofa 18 na wakati sasa hivi tuna majengo yana mpaka ghorofa 17. Ndiyo maana tukasisitiza kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2007 na kanuni zake ni lazima majengo mapya yatakayojengwa yazingatie usalama kwa kuweka vifaa vya kisasa ikiwemo automatic fire system na automatic fire detection and suppression system. Mfumo huu utasaidia sana kuweza kupunguza madhara yatakayoweza kutokea moto utakapotokea katika majengo ambayo ni marefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo sasa hivi tunafanya jitihada za kuhakikisha kwamba tunapunguza madhara ya moto kwa kuongeza vifaa vya kuzimia moto. Juzi nilizungumza hapa kwamba miongoni mwa mambo ambayo tunajaribu kufanya ni kuhakikisha kwamba tunatumia magari yaliyokuwa ya washawasha, yale 32 ambayo yameingia pia yaweze kusaidia katika shughuli ya uzimaji moto.
Mheshimiwa Mwenyekiti naona nimetumia muda wangu vizuri, yale ambayo tumekubaliana niyazungumze nimeyazungumza. Naomba sasa nimuachie Mheshimiwa Waziri na yeye aweze kuendelea na pale ambapo mimi sikupagusa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.