Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara muhimu kabisa ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba na mimi nirudishe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan. Hii ni kwa namna ambavyo Watanzania tumeshahudia fedha nyingi zikiletwa katika majimbo yetu katika sekta mbalimbali na wananchi wamekuwa wakishihudia na kujionea wenyewe jitihada kubwa za maendeleo katika sekta zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie pia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wake wote, Katibu Mkuu na Watendaji wengine wote katika Wizara hii ya TAMISEMI kwa namna ambavyo wamejipanga kuhakikisha wanasimamia wizara hii vizuri; na sisi wananchi wa Kishapu tunawapongeza kwa namna ambavyo wamekuwa pamoja kabisa kuhakikisha kwamba mambo ya maendeleo yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza Mkuu wangu wa Mkoa Mheshimiwa Mdeme. Mkuu wangu huyu ni Mkuu wa Mkoa wa aina ya pekee kwa sababu ana ushirikiano wa karibu na sisi Wabunge na halmashauri zetu zote katika Mkoa wa Shinyanga. Nitumie nafasi hii pia kumshukuru Mkuu wa wangu wa Wilaya Mheshimiwa Mkude, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bwana Emmanuel Johnson, pia nimshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri yangu ya Kishapu na Waheshimiwa Madiwani kwa namna ambavyo tunashirikiana kwa pamoja kupeleka mbele maendeleo katika wilaya yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nikuhakikishie kwamba nimepokea zaidi ya bilioni 11 kwa mwaka wa fedha uliopita lakini mpaka sasa nimeshapokea tena bilioni nane ambazo bilioni hizi zimekwenda kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwenye jimbo langu ikiwemo sekta ya barabara, maji, elimu, afya na maeneo mengine yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya mambo ambayo nataka niyazungumzie katika eneo la barabara, nimepokea zaidi ya bilioni 2.43. Fedha hizi mpaka sasa ninavyozungumza ipo miradi muhimu kabisa ambayo inatekelezwa. Mradi wa Mwajidalala Bulekela ambapo kuna kunyanyua daraja na kuweka makalavati, barabara ambayo inakwenda kuunganisha Wilaya ya Kishapu na Wilaya ya Igunga. Pia kuna Mangu-Somagedi kuna fedha, tayari sasa hivi fedha zipo na mradi unatekelezwa; na Ngunga pamoja na maeneo ya Munze. Kuna barabara ya Seseko, Busangwa, pia kuna Barabara ya Buganika Kabila. Barabara hizi zote mpaka sasa hivi wakandarasi wako site na shughuli zinakwenda vizuri. Kwa hiyo katika eneo hili la TARURA ninashukuru kwa sababu miradi mingi naamini kwamba itatekelezwa na maeneo haya yote yalikuwa maeneo korofi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwamba TARURA wanafanya kazi nzuri sana na ninaomba tuamine. Meneja wa TARURA wilayani kwangu Kishapu anafanya kazi nzuri na sisi Madiwani tunampa ushirikiano mzuri kazi zinakwenda vizuri. Jitihada zinazotakiwa ni kuwaongezea fedha…

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili barabara nyingi ziweze..

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Butondo.

TAARIFA

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanta sana nataka kumpa taarifa Mheshimiwa anayechangia, ukiifungua barabara inayotoka Kishapu kwenda Igunda utakuwa umeunganisha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Simiyu, kama ambavyo sera yetu inasema kila mkoa uunganishwe na barabara ya lami kwa maana ya barabara kubwa. Pia itakuwa ni shortcut nyepesi ya kutoka Simiyu Shinyanga kupita Tabora kwenda Mbeya, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Butondo unaipokea hiyo taarifa.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa ya Mheshimiwa, ni taarifa ya muhimu kabisa. Naomba niendelee upande wa sekta ya elimu. Katika sekta ya elimu tuna upungufu mkubwa wa walimu kwanza mahitaji ni 1983 waliopo ni 922 upungufu ni 1,061, ni idadi kubwa sana ya walimu. Sasa kama tunasema kipaumbele chetu katika nchi yetu ni elimu, elimu, elimu, ni lazima jitihada kubwa ifanyike kuhakikisha kwamba tunaongeza walimu ili mradi tatizo hili liweze kuondoka. Vivyo hivyo hata katika sekondari mahitaji ni 482 waliopo ni 403 pungufu ni 79, bado ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu katika ajira hizi zilizotangazwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba sana kipaumbele wapewe walimu ambao wamekuwa wakijitolea katika maeneo yetu; na hii tumejionea wenyewe. Tumekuwa tukipata ajira za watumishi kutoka maeneo mbalimbali lakini wanapofika katika maeneo hayo, baada ya muda mfupi wimbi kubwa la watumishi wanaandika barua za kuomba kuhama. Sasa kwa nini Serikali tunatumia resources nyingi kwa ajili ya kuhamisha, kuwaondoa mahali pengine na maeneo mengine yanabaki kuwa na ma-gape makubwa na hasa ambayo yako pembezoni? Naomba sana, hawa walimu wanaojitolea hata katika sekta ya afya pia tuweke kipaumbele na tuwatizame, kwa sababu tayari wakurugenzi, maaifisa elimu wamekuwa wakitoa taarifa huku wizarani, zinazoonyesha walimu wanaojitolea lakini na madaktari wanaojitolea, hawa ndio wapewe kipaumbele katika ajira hizi zitakazokuwa zinatangazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie mahitaji katika sekta ya afya. Tunahitaji watumishi 664 lakini waliopo ni 274 na upungufu ni 391; unaweza ukaona kwamba ni upungufu mkubwa sana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niishukuru sana Serikali ya Mama Samia kwa namna ambavyo mmeweza kutusaidia katika Hospitali yetu ya Wilaya, kwa mwaka uliopita tulipata bilioni 1.3 Hospitali yetu ya Wilaya, Kalitu tulipata milioni 900, milioni 500 Negezi, milioni 300 Mwangalanga na Shinongela milioni 50. Lakini kwa mwaka huu wa fedha Jakaa tulipata milioni 500, Hospitali yetu ya Wilaya tumepata milioni 50, Wella dispensary tumepata milioni 500 Mwamalasa. Hii miradi mpaka sasa ninavyozungumza inakwenda kwa kasi. Naomba niwapongeze sana Madiwani wangu kwa namna ambavyo wamejipanga kusimamia na kuhakikisha kwmaba miradi hii inakwenda vizuri, na niishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine, ninaomba sana; kuna maboma zaidi ya 32 ambayo yanahitaji kukamilishwa katika sekta ya afya. Kwa hiyo nitoe ombi kwamba katika eneo hili tuone umuhimu wa kupeleka fedha za kutosha kwa ajili ya kukamilisha maboma. Jambo lingine nilitaka nizungumzie upande wa ukaguzi. Tumeshuhudia kwamba taarifa ya CAG kwa sehemu kubwa tumeona upotevu mkubwa wa fedha. Sasa napozungumzia katika halmashauri hatuwezi tukawa na halmashauri imara na zinazosimamia vizuri taratibu, kanuni zile za kifedha na matumizi ya fedha kama hatujawa na wakaguzi wa kutosha katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ina mkaguzi mmoja tu wa ndani. Nataka niulize kata 29 halmashauri penyewe pale Makao Makuu, huyu ni mkaguzi mmoja anawezaje kusimamia shughuli hizi zote katika wilaya ya nzima? Ipo miradi inayotekelezwa katika ngazi ya kata, ipo miradi inayotekelezwa ngazi ya wilaya, majengo mbalimbali, miradi hii inayotokana na mapato ya ndani, fedha za ruzuku na wahisani wengine mbalimbali huyu anajigawa vipi, mkaguzi wa ndani mmoja peke yake? Akiugua homa mwezi mmoja halmashauri ina-paralyze. Hebu tuangalie mama yangu kama kweli una nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba hizi hati chafu, huu upotevu wa fedha hautoki ni lazima tufanye mikakati ya lazima kuhakikisha tunapeleka wakaguzi katika halmashauri zetu. Hili nilitaka niombe sana lifanyiwe kazi ili tuweze kudhibiti haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na suala la Madiwani. Tumezungumza kwa muda mrefu kwamba Waheshimiwa Madiwani walipwe kupitia Serikali, tunaishukuru Serikali kwa uamuzi wake kuamua kulipa fedha hizi moja kwa moja kupitia Serikali Kuu, lakini bado changamoto kubwa ni suala zima la fedha wanazolipwa, ni kiasi kidogo sana. Majukumu wanayoyafanya na kusimamia mabilioni haya hayastahili na kile ambacho wanalipwa kutokana na usimamizi wanaofanya. Hebu tuoneni utaratibu wa kuwasaidia hawa watu, na ni wa muhimu sana. Sisi Wabunge bila wao hatuwezi chochote kile. Ninaomba sana Serikali muwe wasikivu Serikali ya Mama ni sikivu. Ninakuomba Mheshimiwa Kairuki ufanye jitihada zote kuhakikisha kwamba ushawishi huo unatokea na Waheshimiwa Madiwani waweze kuongezewa stahili zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni waraka unaohusiana na Kamati ya Fedha kufanya ukaguzi wa miradi kila baada ya miezi minne, utaratibu huu ni wa ajabu kabisa. Kanuni zinasema kamati za kudumu zitakwenda kila baada ya miezi minne kwenda kukagua miradi iliyotelekezwa katika kipindi hicho…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Butondo.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)