Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Anton Albert Mwantona

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni mimi nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia mpango wa bajeti katika Wizara hii ya TAMISEMI. Nishukuru na nimpongeze sana Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Waziri wake Mheshimiwa Ndejembi pamoja na Mheshimiwa Dugange, Katibu Mkuu na wote walio katika Wizara hii ya TAMISEMI wametengeneza bajeti nzuri ambayo
inaenda kutatua matatizo ya wananchi katika ngazi za chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili niseme wazi kwamba namshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Biblia inasema kila jambo lina wakati wake. Kipindi hiki ni cha Mama Samia na yuko tayari kuwasaidia Watanzania kutatua matatizo yao mbalimbali ambayo yanatukabili kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na TARURA nampongeza sana Mkurugenzi wa TARURA pamoja na Injinia ambaye amewekwa kule chini kijana wangu mmoja anaitwa Kamara anatusaidia sana kutatua matatizo ya barabara katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi kwamba kuna barabara ambazo zilikuwa hazipitiki miaka na miaka; kuna barabara ya kutoka Maskulu mpaka Kikole. Hii barabara iliwekewa jiwe la msingi na kipindi kile alikuwa anaitwa Salim Mohamed Salim, lakini kwa bahati mbaya hii barabara haikutengenezwa. Mama Samia ameingia madarakani tumeletewa milioni 473 barabara kutoka Maskulu mpaka Kikole imetengenezwa na wananchi kule wanafurahia matunda ya uhuru wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara ya kutoka Kapugi kuelekea Lienje, pia ilikuwa ni barabara ya miaka mingi haikutengenezwa; lakini Mama Samia ametuletea pesa zaidi ya milioni 270 barabara imetengenezwa na sasa iko katika hali nzuri wananchi wanafurahia matunda ya uhuru wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengi sana katika barabara. Mimi wakati naingia kama Mbunge kuna barabara zaidi ya nne zilikuwa hazipitiki kabisa lakini leo ni barabara moja tu ambayo imebaki ambayo ni kutoka namba one pale Idweri kuelekea Ngumbulu. Namwomba sana Waziri aliangalie hilo kwa sababu ni barabara pekee ambayo imebaki ambayo kwa sasa hivi upitaji wake umekuwa ni mgumu, tuwasaidie pia wananchi wa Idweri kuelekea Ngumbulu ili barabara ile pia ipitike kwa muda wote wananchi waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika TARURA ninayo changamoto kidogo, Rungwe ni wilaya ambayo ina mvua nyingi. Tuna mtandao wa barabara zaidi ya kilometa 1,300 tuna mvua za kutosha, barabara nyingi zinaharibika lakini bajeti yetu ambayo tunapata ni zaidi ya shilingi bilioni 2. 5 ambayo ni ndogo sana kwa Rungwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kama kuna uwezekano formula ya ugawaji wa fedha za barabara iweze kuangaliwa upya kwa sababu Rungwe ni kubwa lakini kipato tunachopata bado hakitoshelezi katika utendaji wetu wa kazi. Kwa hiyo, naomba hiyo tuliangalie tuone ni jinsi gani, pia hata fedha zinazopatikana za barabara kwa sababu ya hali ya hewa ya Rungwe ziweze kuletwa mapema katika maeneo yetu, zitumike mapema kwa sababu ikishaanza mvua tu utekelezaji wa barabara unakuwa tayari ni shida kubwa katika Jimbo langu la Rungwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa afya mwaka jana tulipata na ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais tumepata vituo Vitatu vya afya Bilioni 1.5. Tulipata Kituo cha Ipojora, tulipata kituo cha Ndanto, tulipata kituo pia cha Kiimo ambavyo vyote vimeishakamilika na vifaa tiba vimeishakuja. Wananchi wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwamba kazi sasa imeishaanza kufanyika na wananchi pale wanapata matibabu karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia bajeti ya mwaka huu pia tumepata vituo viwili vya afya, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwamba tumeletewa pesa Bilioni Moja ambayo itaenda kutusaidia wananchi wa Rungwe kuweza kupata huduma kwa karibu katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika hospitali yetu ya Wilaya tumepewa bilioni moja kumalizia jengo la OPD pamoja na Wodi kwa ajili ya wagonjwa zaidi ya 90, pia tunashukuru sana katika hilo kwamba Serikali imetufikilia kutusaidia katika kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa elimu...

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana kengele ya pili imelia, tunaendelea na Mheshimiwa...

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)