Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi nichangie katika mjadala huu wa Wizara ya TAMISEMI.

Kwanza, nami nichukue fursa hii kwanza kupongeza utendaji mzuri wa Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake Naibu Mawaziri pamoja na Katibu Mkuu na Makatibu Wakuu, kwa kweli tunayo imani kubwa na tunawaomba waendelee na moyo huo wa utendaji mzuri ambao tunauona. Vilevile pia nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu ambae kwa kiwango kikubwa anatuheshimisha bajeti hizi kwa kipindi hiki akiwa madarakani miaka miwili sasa, tunaona jinsi ambavyo zinaelekea kwenye maisha halisi ya mwananchi, kwenye maeneo ambayo ndiyo tunamkuta Mtanzania, kwenye elimu, afya, kwenye barabara ndiko tunako mkuta mwananchi halisi wa Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kuwapongeza Waislam wa Mkoa wa Singida ambao jana walifanya maandamano kupinga suala la zima la mmong’onyoko wa maadili hapa nchini, ambayo hivi sasa tunaona kuna nia ovyo inayofanywa na baadhi ya watu kutaka kuteketeza kizazi, kuteketeza maisha ya mwananchi au maisha ya binadamu ambayo ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Nawapongeza sana Waislam wale wa Mkoa wa Singida pamoja na Viongozi wa Dini kwa ujumla hapa nchini hata Mkoa wa Singida Maaskofu nao wametoa matamko na wamesema kwenye maeneo yao, nawaomba waendelee na moyo huo na wasiache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Spika, ambaye pia alitoa mwongozo kuhusu suala hili hapa nchini na naomba Serikali ichukue hatua wasibaki kujitafuna na kumung’unya maneno wakati tayari wanayo mamlaka ya kushughulika na tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie upande wa eneo la afya kwenye Jimbo langu la Singida Kaskazini. Kwa nafasi ya kipekee sana nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na kumshukuru kwa fedha nyingi ambazo ametupa kwenye eneo la afya kwenye Jimbo la Singida Kaskazini. Tunayo Hospitali ya Wilaya na sasa ina vifaatiba na kazi inaendelea kufanyika, pia tunavyo Vituo vya Afya, Kituo cha Afya cha Makuro nacho kimeanza kufanya kazi Tarehe 03 Machi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa kwa kipindi hiki kifupi tumeshajenga zahanati Tisa na baadhi zinafanyakazi ikiwemo ya Mwachambia, Unyampanda pamoja na zahanati ya Mwakichenche. Ninaipongeza Serikali kwa eneo hili, ninaomba bado ninayo maeneo ya changamoto kuna Boma la Kituo cha Afya pale Ngimu, hili boma lina miaka 14 sasa, ameishafika Katibu Mkuu wa CCM ameona na amepita pia Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa ameona na alitoa machozi baada ya kuona nguvu kazi za wananchi zimepotea kwa muda mrefu lakini Serikali haijawapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Mheshimiwa Waziri, pamoja na timu yake walione hili. Eneo lile ni tense liko kwenye mazingira magumu ya Bonde la Ufa wananchi wanateseka kupanda Milima kufuata huduma za afya mbali. Naomba Serikali iwapokee wananchi hawa, iwaokoe mama zetu wanaoteseka wakati wa kujifungua. Watoto wanaohangaika na huduma za afya pamoja na Wazee wasiyoweza kutembea, niombe sana Serikali ilichukue hili na nione kwenye bajeti hii fedha zije zijenge Boma lile la Kituo cha Afya (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Kituo cha Afya Kinyagigi nalo naomba fedha pamoja na boma la zahanati pale Sagara naomba nako fedha zije pamoja na Mwakichenche pale Minyenye. Eneo hili la afya ninaiomba Serikali itupatie ambulance, kuna umuhimu mkubwa sana tupate ambulance kwa sababu maeneo haya kama nilivyosema tumepata zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali ya Wilaya hakuna ambulance. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye eneo la TARURA ninashukuru sana kwa fedha ambazo zimekuja kwenye eneo la barabara mpaka sasa tunapokea Shilingi Biloni 2.2 kwenye miundombinu ya barabara upande wa TARURA. Ninaomba fedha ziendelee kuja na TARURA iendelee kuongezewa fedha lakini na wao waendelee kuboresha madaraja, waendelee kuboresha mitaro ile ya kutiririsha maji, wafanye kazi kwa ufanisi value for money tunataka tuone fedha zinazokuja zifanyiwe kazi ipasavyo ili kuondokana na kero ambayo wananchi wamekuwa wakiipata kwenye eneo la miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili specific naomba nizungumzie ile barabara inayotoka pale njia panda Mgori kwenda Mughunga mpaka Mukulu, Nduamughanga barabara kipande cha kilomita 25 kutoka Nduamughanga kwenda Mukulu ambapo ndiyo tunakutana na Wilaya Chemba, eneo lile ni baya, lina madaraja Saba ni eneo fupi sana kilomita 25 lakini ni maporomoko, mito naomba sana barabara hii ipate fedha za ziada mwaka huu ili iweze kutengenezwa na madaraja yale yaweze kuimarishwa ili kuwaunganisha wananchi wale na wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie maeneo ya Miji yanayokua. Mji wa Ilongero ambapo ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri hakuna barabara hata kidogo, niombe sasa tupatiwe fedha kwa ajili ya kuboresha barabara za ule Mji ili uweze kuwahudumia wananchi ipasavyo wanaotoka Kanda zote za Wilaya ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe madaraja mahusisi, daraja la Mpambano nashukuru limepatiwa fedha Shilingi Milioni 650 kupitia ule mapango wa Mama wa World Bank lakini sasa niombe fedha kwenye daraja la Mgori, daraja lile limekuwa likiua watu, wananchi wamekuwa wakizama pale na limekuwa likikata mawasiliano ya wananchi hasa wakati wa mvua. Niombe sasa tupatiwe fedha na kwenyewe tukalijenge lile daraja. Kama haitoshi daraja lile la pale linalounganisha Minyaa na Mwanyonye daraja lile ni baya limekuwa likitutesa, naomba nako tupatiwe fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu ninashukuru kwa fedha za mradi wa BOOST shule mbili za msingi tumepata lakini niombe sasa ujenzi wa nyumba za Walimu pamoja na vyumba vya madarasa lakini na madawati. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abeid, muda wako umeisha ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana ninaunga mkono hoja lakini naomba next time mtupe muda wa kutosha angalau dakika kumi na kuendelea. Ahsante sana. (Makofi