Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Taifa letu. Vilevile naipongeza Wizara ya TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri, Manaibu na timu nzima na vipaumbele vyao 19 walivyoviainisha kwenye bajeti hii ya 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye mikopo ya asilimia 10. Ni kweli fedha nyingi zimepotea kwenye mikopo hii na sababu kubwa za msingi zinasababisha kwanza ni wahusika na wasimamizi wa mikopo hii kutokuwa waaminifu, hali iliyopelekea kuwa na utitiri mkubwa sana wa vikundi hewa. Vile vile wanufaika wa mikopo hii, wengi wao hawana elimu ya fedha, hawana elimu ya ujasiliamali, yaani ni watu tu kujikusanya; watu watano kutengeneza kikundi, wanapata fedha. Pia maandiko mengi; wanahamasishwa kuandika maandiko ya viwanda vya ufyatuaji matofali, ununuzi wa magari, kilimo cha mjini (green house), na ufugaji wa ngombe wa kisasa. Sasa hivi vitu vyote siyo kweli kwamba mtu anapewa mikopo wiki hii, wiki ijayo anaweza kufanya haya. Hivi vyote vinahitaji elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuona mikopo hii sasa itoke Halmashauri ipitie kwenye taasisi za Kifedha. Naomba, tumeshaona udhaifu mkubwa kwa vikundi hivi vya watu watano watano, kwa nini mikopo hii sasa wasishirikishwe na vikundi vya huduma ndogo za kifedha, hawa ambao ni VICOBA? Kwa sabbau ni vikundi ambavyo vinazungusha hela zao benki. Wananunua hisa zao, wanakopeshana wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona vikundi vidogo hivi vya watu watano watano wakipata zile fedha, walikuwa wanagawana mtu mmoja mmoja, matokeo yake wanashindwa kurudisha, lakini vikundi vya huduma ndogo za kifedha, wale tayari wana fungu lao ambalo wanakopeshana ndani ya kikundi. Ni vikundi ambavyo vina miaka mitano, miaka kumi na wana uwezo wa kukopeshana Shilingi milioni tano, milioni 10 mpaka milioni 20 kwa mtu mmoja. Kiu yao na malengo makubwa ni kufanya mambo makubwa sasa; kufungua viwanda, kufungua makampuni na biashara kubwa kwa ajili ya vikundi. Sasa kwa nini fedha hizi zinazopotea wasiingize na hawa wakawa wanufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawa wanapeleka fedha zao benki, marejesho yao yanapitia benki na benki wanaona kabisa cashflow yao inavyokwenda, ni rahisi zaidi hata marejesho kukatwa kule. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, vikundi vya huduma ndogo za kifedha wanatamani nao wakawa wanufaika wa mikopo hii ili wafungue viwanda, akina mama wapeane ajira. Watoe ajira kwa vijana, hata kwa watu wenye ulemevu, wote wapo kwenye vikundi vya VICOBA wanahitaji mikopo hiyo wafanye vitu vikubwa. Lengo lao siyo kukopeshana, wana malengo ya kufanya vitu vikubwa, lakini mikopo hii haiko wazi kuonesha kwamba wao ni wanufaika. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho, tunaomba aliweke hili wazi: Je, vikundi vya huduma ndogo za kifedha ni wanufaika wa hii mikopo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa tunaiomba Wizara itakapokaa na mabenki kuweka utaratibu, wekeni utaratibu mzuri. Mikopo hii wapate watu sahihi kabla ya kupata mikopo watu waandaliwe kwanza at least hata miezi miwili, mitatu. Siyo kweli, elimu ya wiki moja tu, mtu anapewa fedha, anaweza. Kuna wanufaika ambao ukiwafuata huko mtaani, ukiwauliza kwa nini hamrejeshi? Anashangaa, lini amepata mkopo? Tunaamini kwa kupitia benki haya yote yatakwisha. Kwa hiyo, tukuombe Mheshimiwa Waziri, mikopo hii hata kama itapitia kwenye mabenki, lakini bado Halmashauri ina kazi kubwa ya kufanya. Kuwe na utaratibu wa Halmashauri husika kukaa na vikundi; waliopata mikopo, wasiopata na wanaotarajia kupata. Kuwe na elimu endelevu za hii mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kabisa VICOBA wanafanya vizuri kuliko hawa; lakini ndio hawa hawa akina mama, ndiyo hao hao vijana na ndio hao hao watu wenye ulemavu. Shida kubwa ni kwamba hawa wanaohamasishwa hivi vikundi vya watu watano kuna kitu hakiko sawa. Unakuta kikundi kimeandikiwa andiko. Ukikaa nao ukiwauliza hili andiko lenu mlikuwa mnataka nini? Hawajui hata wameandikiwa andiko gani? Wanaandikiwa maandiko hawayajui. Wanapewa hela, Halmashauri inajua kabisa tunawapa hii hela hawa, andiko lao linasema hivi, hii hela wana uhakika itakwenda kurudi, lakini hairudi, kwa sababu hata walichoandikiwa hawakijui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe suala la elimu na kuandaa watu lizingatiwe sana. Kinyume na hapo, kama mikopo hii itaenda benki, utaratibu usipowekwa vizuri, wanufaika wakawa ndio hawa hawa, na taratibu za benki zikatumika kama zile za kuwakopesha watu wengine, tunaenda kutengeneza janga kubwa kuliko lile la PRIDE. Kwa Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nasisitiza utaratibu, Halmashauri itenge fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa hivi vikundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba Wizara, tuangalie kada ya akina mama wanaofanya biashara ya Mama Lishe. Tunaona majengo ya biashara makubwa yanajengwa, lakini akina mama hawa hawapewi kipaumbele, hawapewi eneo. Akina mama hawa, wateja wao ndio hao wafanyabiashara. Majengo yanajengwa, wanapewa wafanyabiashara tu, wao wanakosa maeneo; na wengi wana mikopo, wanatakiwa warudishe marejesho. Biashara zao wanunuzi ndio hao walioko hapo. Kwa hiyo, tunaomba masoko yaliyojengwa maeneo ya biashara yaliyojengwa litengwe eneo kwa ajili ya akina Mama Lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, nami niungane na wenzangu waliozungumzia na suala la ajira. Mtaani tuna vijana wengi hasa kada ya walimu ambao wanafanya kazi kwa kujitolea. Tunaomba ajira za safari hii zije kitofauti. Hawa wanaojitolea wakapewe kipaumbele; wapate kwanza wao kabla ya wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)