Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya katika Taifa letu. Pia nampongeza sana Waziri wa TAMISEMI, wifi yangu Kairuki na Manaibu wake pamoja na watendaji wote wakiongozwa na Katibu Mkuu. Nawapongeza sana. Pia nampongeza Mkuu wangu wa Mkoa, Albert Chalamila, anatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Mkoa wetu wa Kagera, anafanya kazi asubuhi, mchana na jioni. Nampongeza sana Mkuu wangu wa Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye mchango wangu. Ujenzi wa madarasa ya msingi na sekondari, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ujenzi huo. Hata hivyo, kuna changamoto ambayo ipo kwenye shule hizo ambayo ni matundu ya vyoo. Kwa kweli shule nyingi zimejengwa lakini matundu ya vyoo ni machache sana, nilikuwa naomba sana Serikali iweze…
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Oliver, kuna taarifa.
TAARIFA
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji anayechangia kuwa, kazi kubwa sana imefanywa kujenga madarasa na miradi mingi, na Mkoa wetu wa Arusha ni mfano wa Mkoa mmoja, na yote hayo yamefanywa chini ya Mkuu wa Mkoa John Mongella. Tunampongeza sana na tunakushukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuletea John Mongella. (Makofi)
MWNEYEKITI: Mheshimiwa Oliver, unaipokea hiyo taarifa?
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili na John Mongella alikuwa ni Mkuu wetu wa Mkoa wa Kagera kabla hajaenda huko. Namjua ni jembe sana, kwa hiyo, naipokea sana taarifa yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka kwenye matundu ya vyoo, naomba nijielekeze kwenye nyumba za watumishi. Kwa kweli waalimu wanapata shida sana. Tumejenga madarasa ya kutosha katika shule za sekondari na shule za msingi, lakini waalimu hawana nyumba za kuishi. Unakuta mwalimu anatoka kilomita kama 10 au 20 kutoka sehemu A Kwenda B, anafika shuleni ameshachoka, atafundishaje wadogo zetu na watoto wetu kwa weledi sana? Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali ijielekeze kwa nguvu zote kwenye ujenzi wa nyumba za watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile walimu wanatakiwa wawe na mazingira mazuri, wakitoka shuleni kuna jinsi ya kuandaa andalio la kesho yake, na kuandaa notes. Anatoka shuleni ametembea kilomita saba au kilomita 10, anakuwa ameshachoka chakari. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu sikivu iweze kujenga hata nyumba za watumishi hasa za walimu wa shule za msingi, kwa kweli wanapata shida sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa watumishi. Mheshimiwa Waziri naomba kipaumbele kwenye ajira hizi wanazoajiri wapewe wale ambao wanajitolea. Unakuta mtu amejitolea zaidi ya miaka mitatu, lakini ajira zikitokea hayupo.
MBUNGE FULANI: Kweli!
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mmoja, kuna shule moja ya Ngara; Shule ya Msingi Nyamiaga, kuna mwalimu ameshajitolea zaidi ya miaka mitatu, lakini huyo mwalimu kila akiomba nafasi zikija jina lake halipo. Kwa bahati nzuri, hakati tamaa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Serikali yetu sikivu iwaone kwa jicho la pekee, hawa walimu wanaojitolea, kwa upande wa afya pia, waweze kuwapa kipaumbele kwa ajira hizi ambazo zimetokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu pia nilikuwa naomba katika hizi ajira, nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa Kairuki wakati anasoma hotuba, kwamba wakishaajiri hawawezi kukuhamisha kabla ya miaka mitano. Nilikuwa naomba iwe hivi, kwa mfano kama Kagera waajiri kikanda. Wakiajiri kama ni mwalimu, wameshaona kwenye database ni wa Kagera, basi wamwajiri Mwanza au Geita au Kahama ili iwe rahisi hata kwenda kuona familia yake, wasianze kusumbua kwamba naomba uhamisho. Kwa mfano, umemtoa Kagera, umemepeleka Mtwara. Umemtoa Kagera, umempeleka Songwe, kwa kweli inakuwa ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, naomba katika hizo ajira wazingatie sana Kanda ili kupunguza kusumbuliwa katika mambo ya uhamisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri waangalie katika ajira hizi, pembezoni huku, kwenye Halmashauri za vijijini unakuta hakuna waalimu, hakuna watu wanaoenda huko; kila mmoja anakataa. Kwa mfano, ukimwajiri mtu ambaye yuko Kagera ukampeleka Wilayani kule pembezoni, ataenda tu, lakini umtoe Kagera, umpeleke Songwe huko karibu na Zambia, kwa kweli inakuwa ni changamoto. Ndiyo hii inaanza kuleta usumbufu kwa ajili ya kuomba uhamisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najielekeza TARURA. Kwa kweli TARURA wanafanya kazi nzuri sana. Wana muda mfupi lakini kazi zinaonekana. Changamoto kwa TARURA ni bajeti. Mfano kwa Mkoa wangu wa Kagera, nilikuwa naomba, kuna Kivuko cha Nyabasa kiko Wilaya ya Bukoba Vijijini. Hicho ni kivuko ambacho tunategemea tujenge daraja. Nilikuwa naiomba Serikali yangu Sikivu, na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, huko ndio nyumbani kwenu pia. Naomba sana kuharakisha usanifu na ujenzi wa Daraja la Chanyabisa la Halmashauri ya Bukoba. Mwaka jana 2022 kuna gari ilitumbukia kwenye hicho kivuko, likakaa almost one-week mle, bila kutolewa.
MBUNGE FULANI: Uuh!
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Kwa kweli ni shida. Ukitupatia bajeti ya kutosha, daraja likajengwa, italeta tija pia kwa wananchi na maendeleo kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza bajeti kwa ajili ya ujenzi pia wa barabara za ulinzi na usalama katika Wilaya za mipakani hasa kule kwetu Ngara, Kyerwa na Missenyi, tujenge barabara ambazo zitakuwa ni za usalama zaidi. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iweze kutupatia bajeti ya kutosha katika hii TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Missenyi na Bukoba vijijini naomba zipatiwe fedha maalum (special fund) kwa sababu kule barabara zake hutengenezwa kwa bajeti ambayo ndiyo hiyo ya special fund. Barabara ni tambarare, mvua zikinyesha maji yanajaa, wananchi hawawezi kwenda upande A na upande B, yaani inakuwa ni changamoto kubwa sana. Tukipata bajeti ya kutosha, watatengeneza barabara ziinuke ili mvua zikinyesha sana maji yasituame na kusababisha wananchi kushindwa kwenda kwenye shughuli zao katika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umeisha! Eh, mh!
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili hiyo.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani! Naunga mkono hoja. Mengine nitaandika kwa maandishi. Ahsante sana. (Makofi)