Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu inayogusa maisha ya Watanzania, Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye hoja kwa sababu muda wangu ni mfupi, na ninataka nijikite sana kwenye suala la ugawaji wa maeneo ya kiutawala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imesimamisha muda mrefu sana suala la ugawaji wa maeneo ya kiutawala. Zipo Kata zetu ni kubwa mno kiasi kwamba wananchi wanapata taabu sana kufuata huduma. Nikitoa mfano, Kata yangu ya Mwangeza, kutoka mwanzo wa Kata mpaka mwisho wa Kata ni takribani kilomita 70. Kata kama hii yenye wananchi takribani 30,000 ina vijiji sita tu. Kutoka Kijiji mpaka Kijiji hakuna barabara. Mtu akitaka kwenda Kijiji kingine aje Makao Makuu ya Wilaya ndiyo aende Kijiji kingine. Kwa hiyo, wananchi wanapata taabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sensa za mfano, kwenye Kitongoji kimoja tu, kwa mfano cha Gajaroda katika Kata hii kulikuwa kuna kaya 280. Kitongoji kama cha Msanga kaya 265, na Kitongoji cha Midibwi kaya 315. Unaweza ukaona kwamba hivi ni Vitongoji, maeneo mengine kaya 300, unaongelea Kata. Sasa tunapokuwa hatugawanyi maeneo, tunawatesa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia maeneo ya utawala ndipo wananchi wanakopata huduma. Sasa wapo wananchi kuna maeneo yao ni madogo tu, wana vijiji vya kutosha, wana mitaa ya kutosha, wana-enjoy hii nchi nzuri inayoongozwa na Mama Samia anayemwaga mambo huku. Sasa inapokuja kwenye Kata hizi kubwa ambazo hazigawanywi, wananchi wanapata taabu, hawafurahii maisha mazuri ya Watanzania. Kwa sababu mtu anasafiri umbali mrefu kufuata shule, kufuata hospitali na Mahakama; na hivi vitu viko kwenye maeneo ya kiutawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara sasa ifuatilie maombi ambayo tumeshayatuma mengi, ambayo tumeyaleta mara nyingi, yanawekwa kapuni. Mfano, tumesema kata kama hii, tunataka tupate Kata ya Dominiki, tupate kata ya Endasiku na tupate Kata yenyewe ya Mwangeza kutoka kwenye Kata moja. Kata kubwa kama ya Ibaga, tunataka tupate Kata ya Ibaga na Kata ya Mkalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya tunayoongea kama ni Matawi ya Chama, tunaongelea matawi mpaka 15, au 20, tunapata shida. Kwa hiyo, namwomba Waziri suala hili alichukulie umuhimu mkubwa. Nimeamua nibaki kwenye eneo hili kwa muda mrefu kwa sababu tumekuwa tunalisema tu na kulipapasa, hebu tugawe maeneo ili wananchi wapate huduma nzuri ambayo Rais wetu anaitoa, kwa sababu bila kugawa maeneo, huduma hizi haziwafikii, wananchi wengine anateseka maporini kwa sababu Serikali iko mbali na maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa nataka niseme kuhusu uhaba wa watumishi. Naomba wakati Waziri ana-wind up atueleze, hivi ni kwa nini tunashindwa kujaza ma-gap ya wafanyakazi ambao tayari walikuwa kwenye bajeti? Wafanyakazi waliostaafu na waliotangulia mbele ya haki. Kwa sababu mtu anapostaafu, anastaafu katikati ya mwaka; au mtu anapofariki, kifo ni ghafla, tunaweza tukapitisha bajeti leo, mtumishi akafariki kesho; tayari yuko ndani ya bajeti. Kwa nini, tusitumie kanzidata kujaza yale ma- gap kwa sababu tayari wako kwenye bajeti, ili Rais anapotangaza ajira mpya ziwe ajira mpya kweli? Kwa sababu hizi ajira mpya zinaishia kujaza ma-gap tu ya wastaafu na watu waliofariki, matokeo yake hatuoni ajira mpya zinafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waziri atueleze, tatizo ni nini? Kama tumeshapitisha bajeti ya watumishi kwa mfano 1,000, wakafariki 50, si wajazwe wale 50 kwa sababu wako kwenye bajeti? Hii ikiendelea tutapunguza hili gap la watumishi, kwa sababu wastaafu wanastaafu kila siku. Watu wanatangulia mbele ya haki kila wakati, lakini nafasi zao wako kwenye bajeti hazijazwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuelezwe tatizo liko wapi? Kama tumeshapitisha bajeti, tutumie kanzidata, mtu aandikiwe tu barua, nenda karipoti mahali fulani. Interview zinafanyika kila wakati, kwa hiyo, tunayo list ya watu wamesoma hawa, kuna walimu hawa, kuna manesi kuna madaktari, mtu anaandikiwa tu karipoti ujaze gap, ili hizi mpya zinapotoka ziwe mpya kweli. Hizi ajira tunasema mpya, siyo mpya hizi, kwa sababu ma-gap yamejaa kote huko. Kwa hiyo, hakuna cha ajira mpya, ndio maana tatizo hili halipungui kwa sababu hiyo. Kwa hiyo, naomba kabisa Waziri akija, aliambie Bunge hili, kwa nini hatujazi ma-gap wakati watumishi tunao na bajeti tunakuwa tumeipitisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la watoto wetu kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu. Tatizo hili ni kubwa. Leo ukienda kwenye shule za msingi unaweza ukakuta zaidi ya watoto hata nusu, hata robo tatu au robo darasa, hawajui kusoma na kuandika. Hili tatizo halisababishwi na watoto. Watanzania hatuna watoto wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika. Haya yanasababishwa na matatizo mengine ambayo pengine sisi hatujayapa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo mojawapo kubwa kabisa ni la utoro; watoto kukosa chakula cha mchana shuleni. Watoto kama hivi hatugawanyi maeneo, wanakaa mbali. Mtoto anasafiri kilometa sita mpaka saba au 10, anaenda shuleni hajala; anafika anakaa shuleni muda wote hajala. Kwa hiyo, naomba hili tatizo la kutokuwapa watoto chakula kutoka shuleni, Wizara iliangalie upya.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mtoa taarifa, yuko wapi? Mheshimiwa Amar.

TAARIFA

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, KKK inasababishwa na upungufu wa waalimu na pia tatizo hilo la chakula. Nilikuwa nataka nimpe tu taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Isack unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine walishachangia, naomba unilinde muda wangu hata dakika moja nimalizie.

MWENYEKITI: Malizia dakika moja basi.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, tungeweza kupata chakula shuleni pia kupitia kuwafundisha watoto wetu somo la EK ambalo limefutwa. Shule zetu zina maeneo makubwa ya kulima, lakini watoto wetu tumeacha kuwafundisha EK, kwa hiyo, tukirudisha lile somo tukawafundisha watoto wetu jinsi ya kulima vizuri kisasa ili wakitoka wakasaidie jamii, watapata chakula na wazazi tukichangia kiasi kidogo kilichobaki watoto wetu wapate chakula shuleni, tuondoe hili suala la kutokujua kusoma, kuandika na kuhesabu. Linatutia aibu nchi yetu na Mama yetu anamwaga fedha huko kwa ili ya watoto wasome lakini watoto wetu wanakuwa hawajui kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.