Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii. Kabla ya yote ninakualika kwenye pambano la ngumi tarehe 23 jumapili kwa ajili ya kuchangia taulo za kike wewe pamoja na Bunge lako; lakini ninajua majukumu yako ni mengi, nilitamani sana uingie ulingoni nimekuandalia Mwasi Kamani upambane naye kama utapata nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba niendelee na kuchangia.

Mheshimiwa Spika, katika Wizara hii nitazungumzia leo walimu peke yake. Mheshimiwa Waziri katika Wizara yako kuna shida kubwa sana ya kupandisha madaraja kwa walimu. Walimu wanfundisha kwa moyo wakati mwingine ameenda kuongeza elimu kwa ajili ya kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi, lakini upandaji wa madaraja umekuwa ni shida na Serikali mliamu akila baada ya miaka mitatu angalau mwalimu akijaza zile fomu za OPRAS aweze kuongezwa daraja. Hata hivyo, na wale waliobahatika kuongezwa madaraja hawalipwi stahiki zao kwa wakati; hiyo si kabisa, tunavunja mioyo ya walimu kwasababu wanashindwa kufanya kazi na kufundisha watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana bajeti iliyopita walisema wataweka kitu kinachooitwa mserereko, kwa maana ya kupandisha daraja kwa haraka haraka kwa kuwa kwa muda mrefu hayajapandishwa. Ndugu zetu mmejisahau, ninaomba bajeti hii muwakumbuke watu wapandishwe madaraja lakini.

Mheshimiwa Spika, walimu wanaoajiriwa ajira mpya wanacheleweshewa mishahara mpaka miezi mitatu, hii pia inaongeza kuwafanya wafanye chini ya kiwango kwa sababu usipokuwa na mshahara unacheleweshwa inakuwa ngumu zaidi. Wakati mwingine hata arrears zao ambazo zinatakiwa walipwe mnaanzia pale walipoanzia. Mheshimiwa Waziri mimi nakufahamu wewe ni gender activist hakikisha unatetea watu hawa wafanye kazi sawasawa.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia capitation kwa sasa mnafanya vizuri, ninaamini, lakini kuna baadhi ya walimu wakuu hawana fedha hivyo wanaamua kuanzisha miradi midogomidogo ndani ya shule. Nikizungumzia miradi namaanisha uanzishwaji wa kambi za kujisomea wanafunzi. Mimi ninakubali, na hasa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Mtaka alipoanzisha ilikuwa na tija kidogo; lakini kuna wengine wanafanya kama biashara. Wanawaweka watoto kwenye kambi na kulazimisha wachangie fedha nyingi, ambazo sasa tunarudi kule kule kuwapa mzigo wazazi. Tunataka ubunifu wa uhakika lakini usiwe ubunifu unaombana mzazi au mtoto ashindwe kwenda kwenye hilo darasa la jioni la kujiendeleza kwa ajili ya kufaulu.

Mheshimiwa Spika, mimi ninaamini sana katika mambo ya ushindani na hasa ushindsni wa tija usio ushindani wa kuharibu. Vyama vya Walimu (CWT) na vyama vingine; kuna chama kipya kinaitwa CHAKAMWATA na vinginevyo mviache viwe huru ili walimu waweze kutoa hoja zao, waweze kulalamika kwa uhalali na hatimaye zile changamoto walizonazo katika maeneo ya kazi ziweze kujibiwa. Tunapozuia vyama vya wafanyakazi na kuwawekea viongozi na kuwalazimisha hatuwatendei haki walimu. Tunataka wao wachague wanao wataka na hatimaye waweze kujikwamua katika tija wanazotaka kufanya.

Mheshimiwa Spika, naomba sana; suala la walimu wa kike amelizungumza mbunge aliyeondoka; tusipokuwa na walimu wa kike ilhali sasa hivi tunajua dunia imeharibika; hali inakuwa mbaya katika malezi ya watoto wa kike. Tunahitaji walimu wawepo ili waweze kuwasimamia watoto hawa na hatimaye watoto waweze kufanikiwa.

MHE. JOSEH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa George Kakunda.

TAARIFA

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji. Zipo shule nyingi jimboni kwangu hazina mwalimu wa kike kwa hiyo watoto wa kike wanakosa huduma ya kuhudumiwa na mwalimu wa kike.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge niwakumbushe tu taarifa inatumia muda wa mchangiaji si muda wa kiti. Mheshimiwa Sophia Mwakagenda malizia.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante ninaipokea taarifa hiyo na ninasisitiza kwamba mtoto wa kike anapohudumiwa na mwalimu wa kiume ndipo ubakaji na mambo mabaya yanaanzia hapo. Kwa hiyo, tunaomba Wizara hii ihakikishe kuwa katika bajeti hii tunaajiri wanawake kwa wingi zaidi kwa ajili ya watoto wa kike kwenye shule zetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya ninakushukuru sana kwa kunipa muda wa kuchangia na ninaendelea kukuombea ukubali kupambana na Ng’wasi kama utakubali, ahsante sana. (Makofi)