Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri na leo hii nikaweza kusimama katika Bunge hili lakini pia nikupongeze kwa namna unavyoliongoza vizuri Bunge letu, Mwenyezi Mungu akujalie Spika wetu ili uweze kutuendelea kutoongoza vizuri katika Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza kuzungumzia kwa upande wa wakulima wa korosho. Upande wa wakulima wa korosho, dawa, viwatilifu vipelekwe kwa wakati. Kumekuwa na mabadiliko kila mwaka aina nyingine ya dawa kila mwaka aina nyingine ya dawa hali hii inapelekea wakulima wetu kutofanya vizuri katika uzalishaji wa korosho.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie kama kutakuwa na mwaka mwingine kunakuwa na mabadiliko ya dawa basi naomba watu wetu wa kilimo wawe wanatoa elimu kwa wakulima wetu juu ya matumzi ya dawa hiyo. Maana mara nyingi wakulima wamekuwa wakitumia dawa bila kuwa na uhakika. Hali hii inapunguza tija kwa uzalishaji wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kuzungumzia kwenye suala la afya. Mara nyingi nimekuwa nikisema hapa ndani ya Bunge kuhusu juu ya matibabu kwa wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Vijijini. Wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Vijijini wanapata tabu sana wanapokwenda kwenye matibabu hasa wale wenye magonjwa ya moyo, figo na magonjwa mengine. Wanapokwenda katika hospitali zetu kupata matibabu kwa kweli wamekuwa wanakosa madaktari Bingwa. Tumekuwa na uhaba mkubwa sana wa madaktari bingwa katika Mkoa wetu wa Mtwara. Hivyo niiombe sana Serikali itupatie madaktari bingwa wa magonjwa haya ya moyo, figo na magonjwa mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaomba Serikali iweke utaratibu hata kwa mwezi mara moja wawe wanatuletea madaktari bingwa katika mkoa wetu wa magonjwa haya; kwa sababu watu wetu wanapata shida sana wanapokwenda kwenye hospitali tumekuwa na changamoto kubwa ya madaktari bingwa. Wanaambiwa waende Muhimbili wanapewa rufaa ya kwenda Muhimbili sasa kutokana na kipato cha watu wetu wanashindwa kwenye Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu.

Mheshimiwa Spika, tuna hospitali yetu ya kanda ya kusini; Kwanza ninaishauri Serikali kwa kutujengea hospitali ya kanda ya kusini. Tunaishukuru sana Serikali kwa kuliona hili katika mkoa wetu lakini pia kumekuwa na changamoto kubwa katika hospitali hii ya kanda ya kusuini. Tumekuwa na changamoto ya nyumba za kulala watumishi, watumishi wanaishi mbali na hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niiombe sana Serikali itujengee nyumba kwa ajili ya watumishi wetu katika hospitali yetu ya kanda ya kusini lakini pia ituletee madaktari bingwa pamoja na vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi kwenye zahanati na vituo vya afya kwenye Jimbo langu la Mtwara Vijijini. Tumekuwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi katika sekta hii ya afya kwenye zahanati zetu watumishi hawapo wa kutosha kwenye vituo vya afya watumishi hawapo wa kutosha. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali ituletee watumishi wa kutosha katika vituo vyetu vya afya pamoja na zahanati zetu.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Vijijini kwa kweli wamekuwa wakijitolea sana kujenga maboma kwa ajili ya zahanati. Wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana wananchi wangu ya kuhakikisha wanapata zahanati katika ngazi zetu za vijiji lakini sasa wanashindwa wanakwama na wakikwama maboma yanakaa muda mrefu bila muendelezo. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali iwaangalie wananchi hawa wa Jimbo la Mtwara Vijijini ambao wanajitoa kuhakikisha wanajenga wenyewe na maboma ya zahanati. Kwa hiyo, Serikali lazima itie mkono na lazima iwape nguvu.

Mheshimiwa Spika, sasa nije nizungumzie suala la maji. Kila nikisimama kwenye Bunge hili siachi kuzungumzia suala la maji. Katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini bado tumekuwa na changamoto kubwa ya maji katika Jimbo la Mtwara Vijijini bado hatujafikiwa kwenye huduma hii muhimu ya maji safi na salama. Sielewi tatizo liko wapi, tuna vyanzo vya maji, tuna Chanzo cha Maji cha Mto Ruvuma, tuna Chanzo cha Maji cha Bwala la Kitere tuna Chanzo cha Maji cha Makonde.

Mheshimiwa Spika, vyanzo vya maji tunavyo, tatizo liko wapi, kwa nini Serikali haitumii vyanzo vya maji hivi ili kumaliza tatizo la maji katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini ili kumaliza tatizo la maji katika Mkoa wetu wa Mtwara. Vyanzo vya maji vipo lakini tatizo ni nini msitumie vyanzo hivi vya maji ili kuwatua ndoo kichwani wamama wa Mtwara Vijijini. Wamama wa Mtwara Vijijini wanapata tabu sana, ndoa zinakufa, wamama wanaliwa na wanyama wakali kwa sababu ya kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika jimbo ambalo limekuwa na changamoto ya maji ni Jimbo langu la Mtwara Vijijini. Niiombe sana Serikali iliangalie hili vyanzo vya maji tunavyo. Naomba mtumie vyanzo vya maji hivi ili kumaliza tatizo la maji katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye suala la elimu; tuna upungufu mkubwa sana wa walimu kwenye shule za msingi na sekondari katika jimbo langu. Kuna mapungufu makubwa ya walimu, kwa hiyo, niiombe sana Serikali iangalie katika jimbo langu mtuletee walimu wa kutosha wanafunzi ni wengi, walimu ni wachache. Kwa hiyo niiombe sana Serikali iangalie katika upande huu ya kutuletea watumishi katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini.

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)