Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nichangie hoja iliyoko mezani. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana anayofanya ya kutuletea fedha nyingi kwa ajili ya elimu, afya, barabara na mambo mengi sana ambayo tumeyaona tangu ameingia madarakani, tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri Kairuki, Manaibu wake Mheshimiwa Dugange na Ndejembi na wakuu wa taasisi wote zilizoko chini ya TAMISEMI kwa kazi kubwa wanayoifanya, tunawapongeza sana. Nichukue nafasi hii kumpongeza pia Mkuu wetu wa Mkoa Balozi Batilda Buriani kwa kweli ameishi vizuri na Wabunge namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi tena kumpongeza Mheshimiwa Waziri Kairuki kwa jinsi ambavyo anatupa taarifa sasa za fedha zote zinazokwenda kwenye majimbo yetu. Hongera sana kwa hiyo tunajua kazi nzuri ya Serikali inayofanya kutokana na taarifa unayotupa, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais, ziko changamoto kidogo ambazo ningependa kuzitaja na hasa zinazohusiana na jimbo langu. Kwa mfano, ametusaidia sana kupata madarasa mengi, tunaomba sana sasa atusaidie tuna uhaba wa walimu wa shule za msingi 639, wa sekondari 118 na wafanyakazi wa afya 758. Tutashukuru sana wakitusaidia lakini pia watusaidie kumalizia maboma ya madarasa na zahanati ambazo bado hazikakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono wenzangu waliosema Engineer Seif anayeongoza TARURA apongezwe pamoja na walio chini yake wote wanafanya kazi nzuri ya TARURA lakini kutokana na mahitaji mengi na ukiangalia kipindi cha TBC asubuhi Mwandishi wa Jambo kila siku anaonyesha mahali ambako wanahitaji barabara vijijini na kadhalika. Kwa kweli tunaomba TARURA waongezewe fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ziko changamoto zingine zinazohusu kazi ya ualimu,kazi ya ualimu ni kubwa na idadi yao ni wengi sana. Tunaomba sana TAC irekebishwe. Kulikuwa na utaratibu wa kiufanyiwa muundo mpya wa TAC lakini mpaka sasa ile kazi haijakamilika tunaomba muundo ambao ulikuwa umeshaanza kufanyiwa kazi ukamilike ili waajiriwe. Wale makatibu wasaidizi walioko wilayani mpaka sasa hivi hawajapata uthibitisho kazini na hata mpango wao wa mishahara haujafanyika. Tunaomba TAC iimarishwe ili kutoa huduma kwa waalimu wengi sana na sasa hivi wanazidi kuongezeka ili waweze kufanya kazi ya muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wakati huo huo tulikua tunaomba Teachers’ professional Board irudishwe ndani ya TAC ama la si hivyo tunapoteza hela bure kuanzisha taasisi mpya ambako ingeweza kufanya kazi ikiwa ndani ya TAC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na wengine wote walioko ngazi ya chini ambao wanafanya kazi kubwa sana. Tutashukuru kama Serikali itawaangalia kwa upande wa mafunzo lakini pia na kuwaongezea posho kidogo waweze kufanya kazi yao vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la wadau wanaofanya kazi sambamba na Serikali. Kwa mfano, hawa wanunuzi wa tumbaku, wapo wanaotusaidia sana katika mahitaji mbalimbali. Kwa mfano ukichukua JTI ambao wananunua tumbaku kwetu wametusaidia kujenga shule ya watoto wa kike. Tunawashukuru sana na tunaomba na wengine waendelee kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la upungufu wa madawati, nilikua naomba kama Serikali inaweza kukaa chini na kuangalia hizi mbao zinazokamatwa zinakaa kwenye vituo mpaka zinaharibika. Kwa nini Serikali isikae na Wizara mbalimbali zikakubaliana kwamba mbao zinazokamatwa badala ya kupelekwa minadani, zipelekwe moja kwa moja kwenye shule ziende zikatengeneze madawati kutokana na uhaba uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nilikuwa nimefikiria pia kwamba ni muhimu sana kuangalia jinsi gani ambavyo wafanyakazi wengine pamoja walimu wanaweza kurekebishiwa posho zao, madai yao ili waweze kusaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tulikuwa na mengi lakini kwa sababu ya muda, naipongeza sana Wizara hii ya TAMISEMI na kwa kweli wanafanya kazi, wote wote katika ngazi za mikoa ngazi za wilaya wote wanafanya kazi, tunaomba kabisa tuwatie moyo wakiongozwa na Mheshimiwa Kairuki ambaye yeye kazi anaiweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nimpongeza tena Mheshimiwa Rais kwa kurudisha wasichana waliopata mimba kurudi shuleni. Hongera sana, jumla ya wanafunzi 1,907 wamerudi shule wakiwemo pia wanaume waliokuwa wametoroka 861 na watoto wa kike pia ambao wamerudi shuleni ni 999, wakiwemo 377 ambao walikuwa wamepata mimba. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo naipongeza tena Serikali yetu kwa ujumla kwa maendeleo na Wizara inayohusika, wote katika ngazi zote. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)