Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambako ameniwezesha kuwa mzima na kunipa afya njema, ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu tunavuta na kupumua hewa yake bure. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya. Kazi hizo zinaonekana kiuhalisia, nimshukuru sana kwa sababu Mkoani kwetu Mbeya amekuwa akitutumia fedha za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wetu Juma Zuberi Homera pamoja na timu yake namna ambavyo wanasimamia vizuri sana shughuli za maendeleo kule Mkoani kwetu Mbeya. Na kupitia Mheshimiwa Mkuu wetu wa Mkoa Zuberi Homera, Mkoa wetu sasa hivi unakwenda kwa kasi na umetulia kweli kweli kama jinsi ambavyo Mbunge wa Mbeya Jiji anaitwa Mheshimiwa Dkt. Tulia na Jiji letu la Mbeya limetulia kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niipongeza sana TAMISEMI, TAMISEMI ambapo wanafanya vizuri wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri Kairuki pamoja na Manaibu Waziri wake. Nawapongeza hawa vijana wetu wa TARURA wanafanya kazi nzuri, TARURA Mkoa wa Mbeya ni wachapakazi na wanajituma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bajeti inakuja hapa Bungeni tunaipitisha na tunaamini kwamba fedha zile tunapitisha, zinakwenda kufanya kazi zilizolengwa. Mwaka 2022/2023 tulipitisha hapa kazi za maendeleo matengenezo bilioni 8.4 zimepokelewa bilioni 4.2 sawa na asilimia 51. Fedha za jimbo bilioni 3.5 zimepokelewa bilioni 2.1 sawa na asilimia 60, fedha za tozo bilioni 7.5 zimepokelewa bilioni 4.3 sawa na asilimia 60. Maendeleo bilioni 1.7 zimepokelewa milioni 968 sawa na asilimia 56. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi mwaka unakwendakwisha imebaka kama miezi wiwili tu, fedha zile hazijafikishwa kule TARURA, ambapo wazabuni nikimaanisha makandarasi
wanafanyakazi kwa kujituma kuhakikisha wasikwamishe maendeleo ambayo ni ya mkoa, hasa kwa barabara na wakandarasi hawa fedha wakati fulani wanakua wanakopa na zingine wanachukua fedha za moto. Wanaishia kuuziwa nyumba zao ama mashamba yao waliowekewa rehani. Sasa tunatakakujua Wananchi wa Mkoa wa Mbeya, fedha zinakuwa zinakwenda wapi? Na kwa nini zisifike kwa wakati kule? Zile ambazo tumeshazipitisha hapa. Nini kinasumbua? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, sasa hivi mwaka kesho tunakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mkoa wetu wa Mbeya unatatizo kubwa sana la Maafisa Watendaji, wamekuwa ni shida hawapo. Ukienda Wilaya ya Rungwe hatuna Maafisa Watendaji 48, Mbeya Jiji Maafisa Watendaji 60 hawapo, Chunya 10 hawapo, Mbeya DC 16 hawapo, Busokelo 12 hawapo. Jumla Mbeya tuna upungufu wa Maafisa Watendaji 146 na sasa mwaka kesho tu tunakwenda kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa, tunaomba sana mliangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo nimeongea kuhusu TARURA. Sasa hivi vyakula vipo bei juu, wazabuni ambao wanapeleka vyakula kwenye shule za kwetu kwa maana shule za Serikali. Fedha zilizokuwa zikipelekwa zimepunguzwa sana. Chakula kipo bei juu, chakula kipo baharini kabisa kule bei zake lakini fedha zinapelekwa kidogo. Sasa hivi Serikali inatengeneza madeni kwa mazabuni. Mazabuni wanapata shida sana namna ya kuendesha biashara zao namna ya kuendesha kazi zao.
Mheshimiwa Spika, tulikuwa tukiongelea sana kuhusu mabweni ya watoto wa kike. Kwa namna ambavyo walikuwa wakipata changamoto huko mitaani lakini sasa hivi ninaomba sana Serikali iwekee mkazo hili, ione jicho la huruma. Sasa hivi changamoto iko kwa watoto wa kike, ipo kwa watoto wa kiume. Naomba sana tunapoelekeza kuendelea kujenga mabweni tuelekeze kujenga mabweni kwa ajili ya watoto wa kike na watoto wa kiume. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaipongeza sana Serikali ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, amesema kazi iendelee na nimefanya msisitizo hata kuvaa nguo hii ambayo niivaa mitaani kote kuonyesha kazi iendelee na kweli kazi itaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunafanya kazi nzuri naipongeza Serikali kwamba wamejenga zahanati, vituo vya afya lakini watumishi wamekuwa ni changamoto nikimaanisha kwamba vile vituo vya afya vimejengwa lakini madakatari ni tatizo. Tunaomba sana mpeleke madaktari, mmpeleke manesi lakini pia hata vitendea kazi vimekuwa ni duni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iweke jicho la huruma juu ya haya ninayoyaongea hapa. Naomba sana jambo lingine kwa upande wa ndugu zetu hawa wa TAMISEMI. Nimeongelea suala la barabara, naomba nijaribu kuongelea kwa upana wake. Safari hii tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa fedha ambazo amezipelekea TARURA, lakini hazijafika zote ila barabara zile ambazo zilifikiwa kiukweli zimekuwa nzuri na mafuriko kidogo yamepungua hata usumbufu umepungua.
Mheshimiwa Spika, kipekeeā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa kengele imegonga ya pili.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii lakini ningependa sana kujua anavyokuja kuhitimisha hapa Mheshimiwa Waziri atuambie fedha zile ambazo zinacheleweshwa nini kinasababisha zicheleweshwe hizi fedha
badala ya kwenda kwa muda muafaka ili makandarasi waache kusumbuliwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)