Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nijielekeze kwenye kuchangia bajeti ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima. Niishukuru sana Serikali kwa kutupatia fedha takribani shilingi bilioni saba hivi kwa ajili ya maendeleo na matumizi mengineyo lakini vile vile kwenye upande wa barabara lakini na pia kwenye miundombinu ya shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili la barabara tulipangiwa kupata shilingi bilioni mbili, tuna shilingi bilioni moja na milioni 300. Tunaomba zile fedha nyingine zilizobakia karibu shilingi milioni 700 zipatikane tuweze kukamilisha miradi iliyopo. Vile vile kwenye eneo la miundombinu ya shule tuna shilingi milioni 692, tunaenda kujenga shule mpya ya msingi. Tuna ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo na hizi tunazielekeza kwenye maeneo ya Maramba JKT, Mazola Kilifi, Mtimbwani, Kisiwani A na Perani. Tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la Sekta ya Afya tunaishukuru Serikali kwa kutuanzishia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na hivi ninavyozungumza tumeshaanza kutibu wagonjwa wa nje lakini bado changamoto ni kwenye matibabu ya kibingwa kwenye kuwalaza wagonjwa na kufanya upasuaji ambao bado tunatumia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga yaani Bombo. Naiomba sana Serikali itupatie fedha tukamilishe ujenzi wa wodi na vifaatiba ili hospitali hii iweze kuwa kwenye full swing.

Mheshimiwa Spika, vile vile tulileta maombi maalum tulipopewa fursa ya kuelezea maeneo ambayo tuna changamoto za sekta ya afya kwenye vituo vya afya. Tunashukuru tulipata Kituo cha Afya kimoja pale Daluni, lakini kuna eneo la kimkakati tulilolielezea ukanda ule wa Mpakani. Tulileta maombi rasmi ya Kata ya Mwakijembe ambayo wananchi wetu wanalazimika kwenda kupata huduma ya afya upande wa pili wa Nchi ya Kenya. Kwa sababu kutoka Mwakijembe mpaka Makao Makuu ya Wilaya ni kilometa 80.

Mheshimiwa Spika, tuna changamoto kubwa tuna aibu pale kwa sababu wananchi wetu hasa akinamama wanalazimika kwenda kujifungua Kenya, kwa hiyo watoto wanaozaliwa wanasajiliwa Kenya, hii siyo sawa. Tunapokuja kuwapa usajili raia wetu tunapata changamoto. Naomba kwa mara nyingine hebu tuweke mkazo kwenye eneo hili ili wananchi wetu wapate huduma stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili niliomba vile vile Zahanati ya Jasini ambayo na yenyewe inapakana na wenzetu wa ukanda wa Kenya na wananchi wetu hawa wanaenda kupata huduma kule. Wananchi wameshaanza ujenzi wa Kituo cha Afya kule Mwakijembe, wamekwishaanza ujenzi wa zahanati. Tunaomba jitihada ya Serikali tuwasaidie wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo la elimu. Tunaishukuru Serikali kwa kazi inayofanya kwenye Sekondari yetu ya kidato cha tano na sita cha Mkingaleo. Tumepata fedha pale za kukamilisha ujenzi wa mabweni. Tunaomba sasa kuna ahadi pale ya Dada yangu Ummy akiwa kwenye Wizara hiyo alituahidi kujenga uzio, Wizara itajenga uzio kwenye shule ile kwa sababu tuna watoto wa kike pale na Walimu wanaishi nje ya shule ile kwa hiyo ni hatari sana kwa malezi ya watoto wetu lakini vile vile tulikuwa tumeahidiwa ujenzi wa nyumba ya Mwalimu. Tunaomba hili na lenyewe lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali baada ya kuona jitihada zetu tulizozifanya kwenye Shule ya Sekondari ya Zingibari ya maandalizi ya kuipandisha hadhi kuwa kidato cha tano na cha sita. Tulipata fedha takribani shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ambayo yanakamilika. Tumeomba kwamba shule ile sasa mwezi wa saba iweze kupata wanafunzi iweze kuanza. Tunaomba kibali hicho kiweze kupatikana kwa sababu tayari maombi haya tumeshayapeleka, yapo Wizarani. Sambamba na hilo tunaomba tuweze kujengewa bwalo kwenye shule ile ili wanafunzi wale waende kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na Sekondari ya Zingibari tumeomba kibali maalum kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Doda. Tunaomba kibali kile kipatikane ili sekondari ile iweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, mwisho, ni eneo hili ambalo linazungumziwa, la watumishi. Wilaya ya Mkinga tuna uhaba wa watumishi takribani 87. Katika hao 87, watumishi 67 ni Walimu wa masomo ya sayansi, 20 ni Walimu wanaokuja kwa ajili ya shule hizi mbili mpya ambazo tumeziombea kibali. Tunaomba sana Serikali itupe jicho la upendeleo kwa ajili ya mahitaji hayo. Mwisho kila mmoja anayesimama hapa anazungumzia jinsi ambavyo kila Mbunge hapa ana maombi ya vijana wetu kwa ajili ya kupata ajira.

Mheshimiwa Spika, unapoona vijana hawa wanaenda kwamba tumaini lao ni Wabunge wawafanyie jitihada za kupata ajira maana yake mifumo yetu inatiliwa mashaka. Naomba tutumie maarifa ya ziada kuhakikisha kwanza tunajenga imani ya vijana wetu, wakiomba kupitia mitandao waamini kwamba watapata hizo ajira. Vile vile tuone jinsi ya ambavyo utaratibu tunaoutumia utamwingiza kila mmoja wetu isionekane kuna upendeleo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana. (Makofi)