Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi, lakini kutokana na changamoto ya muda naomba kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa ajira kila mwaka. Nasema hivi kwa sababu katika kipindi kama hiki ambacho wote tunafahamu kwamba uchumi wa dunia umeyumba lakini uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika. Vile vile tumeshuhudia kwamba baadhi ya nchi hata suala la kulipa mishahara kwa watumishi wake imekuwa ni changamoto, lakini kwetu sisi kama Watanzania siyo tu kwamba Mheshimiwa Rais ana uwezo wa kulipa mishahara kwa wakati, lakini vile vile ana nguvu ya kuweza kutoa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili siyo jambo dogo, ni jambo ambalo tunapaswa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu. Sote tunafahamu, Mheshimiwa Rais ametoa hizi ajira 21,200. Ni vyema tukafahamu kwamba mahitaji kati ya mkoa mmoja na mkoa mwingine yanatofautiana. Kwa hiyo tukipeleka kwenye mlengo wa kuzigawa hizi ajira kwa kuangalia tu kwamba kuzigawa hizi ajira kimikoa bila kuangalia kwamba mahitaji yanatofautiana, ni wazi kwamba kuna baadhi ya mikoa tutakuwa hatujaitendea haki hususan mikoa mipya kama ilivyo Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kwamba Mkoa wa Songwe ni mkoa mpya. Tangu kuanzishwa kwake sasa hivi una takribani miaka saba, lakini katika hiyo miaka saba, ni miaka mitano sote tunafahamu kwamba Serikali haikutangaza ajira. Ajira zimetangazwa ndani ya hii miaka miwili ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan. Katika Mkoa wetu wa Songwe, ndani ya muda mfupi hii miaka miwili sasa hivi tumeshuhudia kwamba Hospitali yetu ya Mkoa imekamilika japo haihusiani na TAMISEMI na iko tayari kuanza kazi.

Mheshimiwa Spika, tunayo Hospitali yetu ya Wilaya ya Songwe. Wilaya ya Songwe kwa muda mrefu ilikuwa haina Hospitali ya Wilaya. Hivi ninavyoongea hospitali hiyo imekamilika na ipo tayari kuanza kazi. Tunayo Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma ambayo ina hadhi sawa na Hospitali ya Wilaya. Hivi ninavyoongea Hospitali ile imekamilika na ipo tayari kuanza kazi.

Mheshimiwa Spika, hii inaonyesha kwamba namna gani ambavyo Mkoa wangu wa Songwe una uhitaji mkubwa sana wa watumishi wa afya ukilinganisha na mikoa mingine. Hili siyo jambo la upendeleo ni suala la uhitaji. Ukiangalia hata kwenye takwimu. Hivi tunaposema Mkoa wangu wa Songwe mahitaji rasmi ya watumishi wa afya ni 3,481 lakini waliopo mpaka sasa hivi ni watumishi 1,191. Gap iliyopo ni watumishi 2,385. Hata nusu hatujafikia. Hili ni janga na ninavyomfahamu Mheshimiwa Waziri ni mtu ambaye ni rahimu sana. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kwenye hizi ajira atakavyokuwa akizigawa autupie jicho Mkoa wangu wa Songwe, uhitaji ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado kwenye vituo vyetu vya afya, bado kwenye zahanati zetu tumepata zahanati nyingi, vituo vya afya vingi lakini uhitaji ni mkubwa sana na zipo kada ambazo zina uhitaji mkubwa. Nikianza na kada ya Wauguzi, ambayo ni kada ya muhimu sana. Kwenye Mkoa mzima wa Songwe takwimu zinaonyesha kwamba mahitaji ni Wauguzi 1,284, lakini waliopo ni wauguzi 434 tu. Gap iliyopo ni wauguzi 890, bado hatujafika hata nusu. Sasa ndiyo maana hata ukienda kule kwenye vituo vyetu vya afya, changamoto ni kubwa sana. Kwenye zahanati changamoto ni kubwa sana. Unafika kwenye kituo cha afya au kwenye zahanati unakuta hakuna Muuguzi wala Daktari.

Mheshimiwa Spika, hili ni janga na sisi kama Wabunge wa Mkoa wa Songwe tuna kila sababu ya kuomba kwamba Serikali iangalie kwa kina Mkoa wetu wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, tuna suala la Madaktari; mahitaji maalum ni madaktari 67, lakini hivi ninavyoongea tuna Madaktari 29 tu. Tuna gap na uhitaji wa Madaktari 38. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri kwenye mgawanyo wa hizi ajira aweze kuutupia jicho Mkoa wa Songwe kwa sababu mahitaji ni makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, vile vile tuna mahitaji makubwa sana ya watumishi katika sekta ya Wakunga na hawa ni watu ambao ni wa muhimu sana. Serikali ya Awamu ya Sita imejikita kuhakikisha kwamba la kwanza tunapunguza vifo vya mama na mtoto. Ni wazi kwamba hatuwezi kupunguza vifo vya mama na mtoto kama hatujahakikisha kwamba kule kwenye zahanati zetu kwenye vituo vya afya, kwenye hospitali za wilaya, kuna kuwa na Wakunga wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge tunapokuwa tunahamasisha akinamama kwamba wanapojihisi kwamba ni wajawazito waende kwenda kuripoti clinic. Wakifika kule basi wawakute Wakunga au wawakute hawa wahudumu. Nilikuwa naomba sana Serikali iweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, pia nikija kwenye upande wa elimu. Mkoa wetu wa Songwe ni mpya na tunaishukuru sana Serikali ya Mama Samia kwa sababu ametupatia Shule ya Mkoa ya Sekondari kwa ajili ya wanawake, mabinti wasichana. Tunamshukuru sana lakini sisi Mkoa wetu wa Songwe tuna upungufu mkubwa sana wa Walimu wa masomo ya Sayansi. Tunatamani kwamba tuzalishe Madaktari wengi, tunatamani kwamba miongoni mwa Madaktari bingwa nchini Tanzania watoke ndani ya Mkoa wa Songwe, lakini kwa sababu tuna upungufu mkubwa sana ya hawa Walimu wa masomo ya sayansi, haitawezekana!

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kwamba 440 hatuna Walimu wa masomo ya sayansi ndani ya Mkoa wa Songwe. Tunaomba sana kwenye huu mgao, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa akifanya basi ni vyema akautupia jicho Mkoa wetu wa Songwe. Wabunge wengi wamezungumza sana kuhusiana na zile ajira za Walimu na kutoa ushauri kwamba ni wakati muafaka sasa Serikali ikawaangalia wale Walimu ambao wamejitolea kwenye halmashauri zetu na napenda kusisitiza hilo na kuungana na maoni ya Wabunge wengine ambao wameongea kwamba ikiwezekana hizi ajira zikatolewe kule kwenye halmashauri.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu kule kwenye Halmashauri ndiko ambako hawa Walimu wapo kule wanajitolea maana yake Halmashauri ndio zinawajua kwamba fulani anafaa, fulani hafai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika vile vigezo ambavyo Mheshimiwa Waziri juzi nilikuwa namsikiliza wakati akivitaja, kigezo cha kujitolea pale hakikuwepo. Ukienda Wizara ya Kazi na Ajira wamekuwa wakitoa program za Walimu kuweza kujitolea ili waweze kupata uzoefu waweze ku- compete kwenye soko la ajira. Sasa kama kwenye vile vigezo vya kutoa hizi ajira kwa nafasi ya ualimu tusipoweka kile kigezo cha watu wanaojitolea tukawapa vipaumbele itakuwa ni disaster kubwa sana. Kwanza tutakuwa tunawavunja moyo nasi tunafahamu kwamba katika shule zetu Mikoa yote Tanzania upungufu wa Walimu ni mkubwa. Kwa hiyo, hawa walimu ambao wanaenda kule kwenye shule zetu wanajitolea wanasaidia sana kuweza ku-cover lile gap la upungufu wa walimu. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri muweze kuangalia na kuwatupia jicho wale Walimu ambao wapo kwenye Halmashauri zetu wanajitolea bure ili pia kuweza kuwahamasisha na wengine katika miaka mingine waone umuhimu wa kusema ukijitolea unakuwa kwenye possibility kubwa ya kuweza kupata ajira.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)