Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia kwenye bajeti ya Wizara yetu ya TAMISEMI. Niungane na wazungumzaji waliopita kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri pamoja na Watendaji wote wa TAMISEMI kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya. Kubwa kuliko yote nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya, Watanzania wanajua, Afrika inafahamu na dunia vilevile inajua kazi anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nimpongeze Mkuu wangu wa Mkoa Alhaji Abubakar Kunenge, baba huyu ni mchapa kazi, anasimamia vizuri shughuli za kimaendeleo katika Mkoa wetu nasi tunafarijika sana na uwepo wake katika Mkoa wetu wa Pwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijachangia bajeti hii naomba nikumbushe mambo mawili, matatu ambayo yapo katika Jimbo letu la Kibiti. Jambo la kwanza naomba nikumbushe ahadi ambazo zimetolewa na Wizara hii katika miaka miwili iliyopita. Kuna ahadi ya ujenzi wa barabara katika kiwango cha lami kutoka pale Kibiti Mjini kwenda katika jengo letu la Halmashauri. Wizara hii ilitoa ahadi mpaka sasa hivi bado haijatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii katika suala zima la ujenzi wa kituo cha afya. Tuna fedha ambazo tulikuwa tumeziomba na zilizokuwa zimeahidiwa shilingi milioni 200 katika kituo chetu cha afya cha pale Bungu ili tuweze kukamilisha baadhi ya majengo. Fedha hizo hazijatoka nasi tunazihitaji, Mheshimiwa Waziri nakujua upendo ulionao, najua tu kwamba hizi fedha unaenda kuzitoa ili sasa tuweze kuona jinsi gani wananchi wa Bungu katika Jimbo la Kibiti wanaenda kunufaika na uwepo wako katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Salale katika eneo la Nyamisati. Mheshimiwa Waziri eneo lile lina watu wengi sana, tunahudumia vilevile Wilaya ya Mafia, kuna zahanati iliyopo pale lakini zahanati ile imehewa. Tuna shule iko pale ya Sekondari ya WAMA wananchi wako wengi, ndugu zetu kutoka Mafia wanategemea pale, chondechonde tunaomba sana tuweze kukamilishiwa ili tuweze kujenga katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, wiki mbili zilizopita tulikuwa na Azimio hapa la kuweza kumpongeza Mheshimiwa Rais, moja katika nukta ambayo tulikuwa tumezungumza ni suala zima la kudumisha demokrasia. Mimi niseme tu tuende mbali zaidi, pamoja na pongezi hizo Mheshimiwa Rais vilevile tunapaswa tumpongeze jinsi alivyoweza kudumisha suala zima la uzalendo katika nafsi za Watanzania.

Mheshimiwa Spika, ninayasema haya kwa sababu ninapenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mwenyekiti wangu wa Kamati ya LAAC Mheshimiwa Halima James Mdee, kwa uzalendo wake mkubwa anaouonesha, tumeweza kufanya nae kazi katika kipindi kifupi lakini huko tulikokuwa tunapita katika ziara zetu unaona jinsi gani alivyokuwa anaweza kuwatetea Watanzania. Fedha za Serikali zinavyokuwa zinapotea na yeye jinsi alivyokuwa anatoa mapovu katika kuweza kuzisemea. Katika hili sina shaka, Mheshimiwa Halima James Mdee uzalendo wake hauna kiwango ni lazima uweze kuigwa na Wabunge wengine wote waliopo humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie bajeti hii katika nukta zifuatazo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichangie katika suala zima la asilimia 10. Serikali mmekuja na maelezo mazuri sana na kuweza kusisitiza suala zima la asilimia kwamba sasa hivi limesitishwa kwa muda, lakini hivyo haitoshi! Ningependa sana Mheshimiwa Waziri wakati unakuja kuhitimisha hapa utueleze zile fedha zilizopotea kule chini kwenye Halmashauri Serikali mna mpango gani wa kuweza kuzirudisha fedha hizo. Hili ni jambo la msingi sana kwa sababu fedha nyingi zimepotea na wale wanaoitwa Maafisa Masuuli they are not accountable katika suala hili.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la msingi ambalo vilevile Mheshimiwa Waziri naomba nilisisitize ni kuhusiana na suala zima la uhamisho wa watumishi. Pamekuwa na destruri mbaya sana katika Wizara ya TAMISEMI. Mtumishi anafanya maovu katika taasisi moja au katika Halmashauri moja lakini kinachotokea anakwenda kuhamishwa kwenda katika Halmashauri nyingine, hiki kitu hakikubaliki. Mamlaka ya nidhamu lazima ichukue nafasi yake hivi sasa kuweza kuhakikisha watumishi wote ambao wanakuwa wanafanya madhambi katika Halmashauri sio tu kwamba wanahamishwa kwenda katika eneo lingine, vilevile wanakwenda kuchukuliwa hatua za kinidhamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la mwisho na la msingi sana ambalo nataka nilisisitize ni kuhusiana na suala zima la mambo ya ajira. Zimetangazwa ajira na mimi niseme tu katika Jimbo langu la Kibiti tuna shida kubwa sana katika suala zima la Walimu. Mimi nina Walimu wanaojitolea hivi sasa takribani zaidi ya 100, katika eneo la sekondari nina Walimu wasiopungua 60, katika eneo la msingi nina Walimu wanaojitolea wasiopungua 81 na katika sekta ya afya kuna watumishi wasiopungua 45. Mimi niseme kupanga ni kuchagua.

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya watumishi ambao wamekuwa wakiomba ajira hizi, kinachokuwa kinafanyika wanatumia Wilaya hizi ambazo ziko pembezoni kama madaraja, wakishafika kule kinachofuata wanasema kwamba mazingira siyo rafiki, mwingine anasema hali ya hewa siyo nzuri, mwingine anaongopa sijui leo nimelala, kesho nimeamka niko nje, mwengine anaongopa fedha zangu zimeibiwa katika mazingira ya kutatanisha, hii kitu haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni lazima sasa kama Serikali mje na mkakati halisia Walimu hawa wanaojitolea waweze kupewa kipaumbele ili sasa tuweza kuona ni jinsi gani kwa namna moja ama nyingine wanakwenda kutusaidia katika maeneo yetu. Kuna
vijana wengi sana ambao wanayajua mazingira haya lakini vijana hawa kimbilio lao kubwa sana ni kwa Wabunge na Wabunge wengi wamesimama humu ndani wanalisisitiza jambo hili, ni lazima sasa ifike wakati Serikali mje kuwa na maamuzi halisia.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani watu wanajitolea lakini Serikali inakwenda kutoa ajira kwa watu wengine, sawa wote ni Watanzania lakini hawa wanaojitolea nao wanazo sifa, ndiyo maana wanafunzi wanafaulu. Sasa kama hivyo ndivyo lazima sasa muweze kuhakikisha mnakuja na jambo halisia la kuweza kuajiri vijana hawa ili waweze kupata ajira.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)