Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami ninaomba niungane na Waheshimiwa Wabunge waliowengi kwanza kabisa kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Daktari Rais Samia Suluhu Hassan kwa uzalendo wake mkubwa kwa Watanzania katika ujumla wake lakini mahususi kwa Watanzania wananchi wa Madaba.

Mheshimiwa Spika, Madaba katika kipindi hiki kifupi cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023 ambayo iyotakamilika Juni tayari Madaba tumeshapokea zaidi ya bilioni kumi na moja na milioni mia sita kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikiwemo shilingi bilioni tatu na milioni mia tatu kwa ajili miradi ya maendeleo ya kawaida na mengineyo, TARURA zaidi ya bilioni mbili, miundombinu ya shule zaidi ya milioni mia sita na kumi na miradi mingine ya maji ambayo inafika karibu bilioni sita.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Madaba wamenituma nitoe shukrani za pekee sana kwa Mheshimiwa Rais, wanatambua sana kazi hizi zinazofanyika na Madaba inaendelea kwa kasi kubwa.

Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Angellah Kairuki Waziri wa TAMISEMI. Hapa mbele yangu nina taarifa mbalimbali zinazotoka Ofisi ya TAMISEMI kwa Mheshimiwa Waziri akitufahamisha Waheshimiwa Wabunge kuhusu miradi mbalimbali na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa maeneo yetu. Utaratibu huu ni mzuri sana unatusaidia sana kwenye ufatiliaji. Sisi ndiyo Wabunge tunaosimama hapa kuomba fedha kwa niaba ya wananchi wetu tunapopata taarifa kwa utaratibu huu mzuri ni lazima tupongeze tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Madaba tumefanikiwa mengi lakini bado tuna changamoto nyingi sana. Nitazisema mbili kwa leo lakini nafasi nyingine nitatumia kwa ajili ya maeneo mengine yatakayojitokeza. Moja katika maeneo muhimu ya Halmashauri yetu ya Madaba ni mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani. Moja katika halmashauri changa nchini ni Madaba, Madaba makusanyo yetu ya mwaka hayazidi bilioni moja na hii Waziri naomba kwa kweli anisikilize. Mapato ya ndani ya Halmashauri ya Madaba hayazidi shilingi bilioni moja kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maeneo ambayo tulitegemea tuongeze mapato walau ku-double ili tupate Bilioni Mbili walau kwa mwaka ilikuwa stendi ya mabasi ya Madaba. Mabasi yote yanayotoka Songea Mjini kuelekea Njombe, kuelea Mbeya, kuelekea Dar es Salaam yanapita Madaba na tathmini yetu mpango biashara wetu unaonyesha, kwa kujenga stendi ya Madaba tutaweza kuingiza walau bilioni moja kwa mwaka na tutaweza kuchangia shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, pale stendi wako wakina mama wenye watoto wadogo mgongoni wanafanya biashara za ujasiriamali lakini mabasi yanashindwa kusimama kwa sababu mazingira siyo rafiki ni hatarishi kwa ajili ya uhai na usalama wa abiria pamoja na wanaoishi maeneo yale. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri tumeleta andiko letu sasa ni zaidi ya mwaka, mara ya mwisho nimeulizwa nimeambiwa lipo hazina. Ninakuomba sana wewe ni mchapakazi wewe ni mzalendo tunakufahamu, naomba katusimamie kwenye eneo hili wana Madaba wanasubiri majibu ya Serikali kuhusu stendi hii ili waongeze kipato na waboreshe maisha yao.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nataka niombe Mheshimiwa Waziri Madaba tuna changamoto kubwa sana ya walimu na watumishi wa afya, hizi ajira mpya zinazotolewa naomba sana tuzitazame hizi shule za Madaba na vituo vyetu vya afya na zahanati pamoja na hospitali.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mmoja kati ya Wabunge ambao tunachangiana pamoja na wananchi kuwachangia walimu wa kujitolea kwenye shule zetu. Mimi kwa mwaka natumia zaidi ya Milioni Tano kuchangia shule mbalimbali pamoja na wazazi, tunachangia Walimu wanaojitolea ili wapate Shilingi Laki Moja Moja kila mwezi. Zipo shule nyingi ikiwemo Njegea na shule zingine nyingi za Madaba. Tunachangiana fedha kuwawezesha hao walimu waweze kusaidia watoto wetu wasome. Ninaomba hawa Walimu wanaojitolea wafikiriwe kwenye ajira, pia tuongezewe walimu na watumishi wa afya ili tupunguze mzigo kwa wananchi wa Madaba ambao wanachanga fedha kwa ajili ya kuwezesha watoto kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho sijui kama muda utaniruhusu lakini nikuombe sana na naomba hii ninukuu kwenye Taarifa ya Kamati ya iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ya Bunge la 12 Mkutano wa 10 naomba ninukuu,

ilishauri Serikali na Bunge lili-adopt walisema hivi “Serikali ibuni utaratibu madhubuti na wenye uwazi ambao utaratibu zoezi zima la ajira Serikalini kwa namna ambayo nafasi zitakazojazwa zitaakisi umoja wa Kitaifa bila kuathiri vigezo” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge wamesema sana na sipendi kurudia ila nataka niwakumbushe Serikali tunapogawa ajira tuangalie uwiano wa maeneo na Mikoa na Majimbo. Tumefanya hivyo kwenye Taasisi za Muungano zote ajira zinatolewa kwa uwiano, Zanzibar na Bara. Tumeangalia kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ajira zinatolewa kwa uwiano, tumeangalia kwenye program ya BBT hii ya juzi tu wamewa-appoint vijana kwa uwiano wa Mikoa. Leo tunashindwaje kugawa ajira hizi kwa Watanzania kwa uwiano wa maeneo wanayotoka?

Mheshimiwa Spika, ili tulijenge Taifa tunahitaji Watanzania wote wapate fursa, tusipofanya hivyo hatutaweza kujenga Taifa bora ambalo Watanzania tunalitamani.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu naomba niunge mkono hoja. Ahsante. (Makofi)