Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya TAMISEMI. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu mpendwa Daktari Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyofanya kazi, kiukweli Watanzania tunafarijika sana na namna ambavyo Mama ameendelea kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Waziri wetu wa TAMISEMI pamoja na Naibu Mawaziri wote wawili kwa namna wanavyoendelea kumsaidia Mama kufanyakazi na kutatua kero za wananchi hapo kwa hapo.
Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizi na pongezi hizi naomba nijikite katika vipengele vichache ambavyo ningependa kuchangia kwa siku ya leo.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ya kujenga shule nyingi za sekondari na kwa kujenga shule nyingi za msingi. Madarasa aliyojenga Mheshimiwa Rais ni madarasa yanayovutia na kupendeza sana. Tunapotaka kupandisha hadhi ya elimu yetu ya Tanzania ni pamoja na kuangalia mazingira ambayo watoto wetu wanayasomea. Nasema haya kwa sababu shule zetu nyingi za Kata zimejengwa katika Makao Makuu ya Kata jambo ambalo linawapelekea watoto katika mazingira haya kutembea umbali mrefu kufika katika Makao Makuu ya Kata ili kwenda kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yapo maeneo ambayo watoto wanatembea kilometa 20, 30 hadi 50 kutoka kwenye vijiji kuja kwenye Makao Makuu ya Kata ambayo ndiyo shule zetu za sekondari zilipo. Watoto hawa wameendelea kukumbana na changamoto nyingi mno ni kitu ambacho kimewapelekea watoto wameamua kupangisha wanaita gheto. Yale maisha ya geto watoto wanajipikia, watoto wanajitafutia mahitaji yao lakini usalama ni mdogo sana.
Mheshimiwa Spika, usalama huu tulikuwa tunawalilia watoto wa kike lakini sasa hivi mpaka watoto wa kiume wamekuwa wakijiingiza katika matendo ambayo hayapendezi. Watoto wetu wa kike waliopangisha katika maisha haya ya geto wanaendelea kuvamiwa kule wanabakwa, wanapata mimba na wengine kuambukizwa magonjwa. Jambo hili linawafanya watoto wengi wasitimize malengo yao na wasifikie ndoto zao. Wapo watoto ambao wamefikia kuacha shule kwa sababu pia kutembea kwa umbali mrefu kwenda kufata elimu. Ninaombe sasa Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga madarasa mazuri. Sasa niombe nguvu hiyo hiyo iliyotumika kujenga madarasa yapelekwe sasa kujenga bweni ili watoto wapate mazingira ya kusomea na waweze kutimiza ndoto zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Wabunge wenzangu wameongelea mengi watumishi. Mimi katika Mkoa wangu wa Manyara hali ni mbaya zaidi. Ninasema haya kwa sababu kuna wilaya zetu hasa Wilaya zile za kifugaji, ukienda shule moja unakuta ina walimu watano, shule ina darasa la kwanza mpaka la saba. Mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi wa darasa la kwanza wanafunzi wako 100 darasani halafu unataka mwanafunzi yule ajue kusoma na kuandika, jambo ambalo haliwezekani.
Mheshimiwa Spika, mimi niombe kulingana na upungufu mkubwa wa watumishi tulionao sasa Serikali iwekeze katika kuona namna ya kurekebisha Ikama katika idara ya elimu. Tusipofanya hivi tutaendelea kuboresha mitaala lakini hatutafanikiwa na hatutafikia malengo kwa sababu mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 100 kwa darasa moja ni jambo ambalo haliwezekani.
Mheshimiwa Spika, wapo vijana wetu wanaojitolea katika maeneo yale mimi niombe katika ajira hii waangalie hasa waliotoka maeneo yale wanayojitolea. Nasema hivyo kwa sababu wapo vijana ambao wanaomba ajira hizi wakishafanikiwa wakipangwa katika mazingira yale ambayo sio wenyeji wenyewe wanaanza kuomba kuhama kwa sababu mbalimbali. Sasa wakianza kuhama kumbuka umewanyima vijana ambao tayari walikuwa wamekwishajitolea mwaka wa kwanza wa pili na wa tatu.
Mheshimiwa Spika, katika ubora kijana aliyejitolea kwa miaka miwili mfululizo ukienda kwenye ujuzi na maarifa yule ameboresha zaidi kwa vitendo, kwa hiyo anakuwa na uwezo mkubwa wa kufundisha kuliko yule ambaye amekaa mtaani na kuja kuanza kazi. Yule ambaye amejitolea atakuwa na uwezo mkubwa wa kufundisha na atatoa elimu bora kwa watoto wetu. Kwa hiyo, niombe sana Wizara iliangalie hili ili kuona namna gani vijana wetu wazalendo waliojitolea, tusiwakatishe tamaa ili waweze kujitolea na wengine waone mfano kwamba mtu akijitolea mwisho wa siku atafanikiwa, atapata ajira, badala ya kuwaacha tena katika nafasi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ya kutujengea vituo vingi vya afya. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ndoto yake kubwa na malengo yake makubwa ni kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya mama na mtoto, lakini vituo hivi haviwezi kwenda kufanya na kutoa huduma bora kama hatuna watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vipo vituo vyetu vya afya, unakuta ina daktari mmoja au nurse mmoja, jambo ambalo linakuwa ni gumu sana katika utoaji huduma. Kwa hiyo, wagonjwa wanafika kwenye kituo lakini hakuna madaktari. Wagonjwa wanapewa rufaa kwenda maeneo mengine kwa sababu tu kituo chao cha afya hakina wataalam. Kwa hiyo, naomba, ili kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma za afya katika vituo vyetu vizuri vilivyojengwa, ni lazima pia kurekebisha ikama katika Idara hii ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais na ninamshukuru sana kwa sababu aliamua na kukubali kwamba vijana wetu amboa walikatizwa masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba, warudi shuleni. Vituo hivi ambavyo sasa wale vijana wetu wamerudi kwenda kusoma, bado vimekuwa na changamoto. Kuna mafanikio, lakini kuna changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, changamoto wanazokutana nazo, wale vijana wanaenda kujifunza kwenye Vituo vya TRC. Sasa katika vile vituo, unakuta wamepewa chumba kimoja cha kujifunzia na kufundishia. Wale wanafunzi wanasoma kwa miaka miwili tu ili aweze kufanya mtihani wake wa Kidato cha Nne. Sasa kwa miaka miwili tu, mwanafunzi anatakiwa awe amemaliza vitu vyote ili aweze kufanya mtihani wake na aweze kufaulu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, changamoto wanazokutanazo wale wanafunzi kwanza hawana walimu wa kufundisha, na pia hawana vitabu vya kujifunzia. Naiomba Serikali sasa iwapelekee vitabu kama ambavyo wanapelekewa katika shule hizi ambazo ziko kwenye mfumo rasmi. Tunasema haya kwa sababu kama lengo kweli ni kuwaokoa hawa vijana wetu ambao wamekatizwa masomo waweze kufikia malengo yao, Serikali ni lazima iweke jitihada zake ili kuhakikisha wale vijana wanafaulu na kutimiza ndoto zao. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)