Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hii Wizara yetu ya TAMISEMI. Sina shaka kabisa na utendaji wa Waziri pamoja na wasaidizi wake. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna alivyoweza kutupa fedha za kutosha katika Manispaa yangu au Jimbo langu la Musoma Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa leo ninayo maombi matatu machache. Ombi la kwanza, kama nilivyosema namshukuru Mheshimiwa Rais ameweza kutupatia fedha Shlingi milioni 500 kwa ajili ya Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Sambamba na hilo, ameweza kutupatia Hospitali iliyokuwa ya Mkoa baada ya kuwa tumejenga Hospitali ya Rufaa. Sasa tumekabidhiwa rasmi kuwa Hospitali ya Manispaa ya Musoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu sasa, kwa sababu tayari tunazo Shilingi milioni 500 kwenye akaunti; na wakati huo huo tayari tunayo hospitali ambayo sasa tumekabidhiwa, lakini hospitali ile ina upungufu mwingi, haina fensi, mawodi yamechoka pamoja na miundombinu mbalimbali; ombi langu dogo kwa Mheshiiwa Waziri, hapa nilipo ninayo barua ya kuomba kubadili matumizi ya zile fedha zikatusaidie kuboresha ile hospitali iweze kuwa hospitali ya kisasa kwa ajili ya Manispaa ya Musoma. Naomba watumishi wetu waje wachukue wakupatie ili hilo tuwe tumelimaliza kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi la pili, pamoja na hiyo hospitali yetu ambayo sasa ni Hospitali ya Manispaa, kulingana na ikama yake, inahitaji iwe na watumishi 200, lakini mpaka hivi tunavyoongea ina watumishi 45 peke yake. Kwa hiyo, ninayo barua ya pili hapa ya kukuomba tuweze kupata watumishi, kwa sababu mpaka hivi sasa tuna zahanati nzuri, na tumepata fedha za kutosha. Tuna vituo vya afya vizuri, tumepata fedha za kutosha, hebu sasa tuboreshe hiyo hospitali yetu ya Manispaa ili watu wetu wa Musoma waweze kupata huduma nzuri ili waweze kuendelea na maisha yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi la tatu, mwaka jana 2022 nilisema hapa Bungeni kwamba pale kwetu Musoma kwenye ile Shule ya Mtakuja, ni shule ya siku nyingi, shule kongwe. Sasa shule ile imechoka na kusema kweli kwa mwaka huu bahati nzuri tumepata fedha Shilingi milioni 90 kwenye shule ile, lakini hizi fedha ambazo tumepata ni kwa ajili ya ukarabati. Ombi lingine ninaloomba Mheshimiwa Waziri ukipata nafasi njoo ujionee mwenyewe ile shule. Kama ingekuwa ni shule ya private tungekuwa tumei-condemn haina sifa za kuwa shule, kwa sababu mabati yametoboka, makenchi yamechoka, yameliwa na mchwa, lakini baadhi ya vyumba vya madarasa havina hata lenta kwa sababu ni madarasa ya zamani. Kwa hiyo, ombi langu la kwanza ni kwamba zile fedha badala ya kukarabati, kitu ambacho hakikarabatiki tunaomba zile fedha zitumike kujenga vyumba vipya vya madarasa, lakini tuongeze fedha nyingine ili ile shule yote iweze kujengwa vizuri na watoto wetu waweze kusoma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni madawati. Leo kama kuna tatizo tunalo katika nchi hii hasa kwa shule za msingi, ni madawati. Watoto wetu kama pale kwangu, nusu ya watoto wa shule za msingi wanakaa chini. Sasa Serikali imesema hivi, wazazi wasichangishwe, lakini wakati huo huo Serikali haitoi madawati. Hata ukiangalia katika hii bajeti tuliyonayo mpaka leo haioneshi kama kuna madawati tutayapata.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wakati anasimama, azungumze kinagaubaga ni namna gani tunamaliza tatizo la madawati? Tofauti na hapo, Mheshimiwa Waziri, wewe jua Shilingi yako lazima niing’ang’anie. Haiwezekani tumepata fedha za kutosha, madarasa mapya yamejengwa, lakini ukiona mle watoto wanakaa chini. Hii ni aibu na ni jambo ambalo halikubaliki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najaribu kuzungumza kwa haraka haraka ili niweze kumaliza ya kwangu. Lingine ni suala la hizi ajira kwa walimu. Tunaipongeza sana hii Serikali ya Mama Samia kwa ajira nyingi ilizozitoa. Sasa leo ukiangalia wakati mwingine ni vitu vya ajabu sana. Tunao walimu wengi ambao Serikali imewasomesha, halafu wamekaa tu pale, hakuna ajira. Upande huu wa pili wanafunzi wetu wako madarasani lakini hakuna walimu. Upande huu walimu wapo, Serikali imewasomesha, hakuna ajira. Upande huu wanafunzi wapo, na miaka inaenda lakini hakuna walimu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ombi la kwanza, ajira kama hizi zinazopatikana, wewe angalia tu; gawa ratio, angalia Musoma ni ajira ngapi? Tuambiwe Musoma tunawapa ajira 500. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni kwamba wale walimu wanaojitolea, tuwe tunawapa kipaumbele. Advantage yake ni moja. Leo inatokea kwamba yuko mwalimu ambaye alipomaliza miaka minne iliyopita, alienda kulima au alienda kufanya shughuli nyingine, lakini yuko mwalimu ambaye amejitolea toka alivyomaliza shule. Leo nafasi inapatikana unakwenda kumchukua yule ambaye alikaa miaka minne bila kutusaidia, wakati yuko mwalimu aliyejitolea.

Mheshimiwa Spika, kwanza hata huyu aliyejitolea tu yeye mwenyewe kwanza imemfanya aendelee kuwa current, kwa sababu ameendelea ku- practice. Kwa hiyo, tunadhani hilo bahati nzuri kwa sababu liko kwenye uwezo wako, hebu tusaidie kuhakikisha kwamba linakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)