Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii. Kwa sababu ya muda naomba niende moja kwa moja kwenye mchango wangu.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoingoza kwa kazi kubwa na nzuri ambazo tunaendelea kuzishuhudia huko kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2022 katika Mkutano wa Bunge uliopita kama nakumbuka vizuri ilikuwa ni Septemba au around Desemba, nilizungumzia vigezo na mambo ambayo yanapaswa kuzingatia katika kuboresha elimu. Mchango wangu wa leo naomba niendelee pale nilipoishia mwaka jana 2022.
Mheshimiwa Spika, moja ya eneo ambalo litatusaidia kuboresha elimu Tanzania ni kuhakikisha kwamba kila mtoto anapata fursa ya kusoma au ya kujifunza katika mazingira yanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, amezungumza Mheshimiwa Regina Ndege, kuhusiana na mabweni au hosteli za watoto wa kike, lakini kwa upande wa Mkoa wa Tanga hususan Wilaya ya Lushoto, jambo hilo ni critical zaidi. Naomba nitoe mfano kwamba, sera au tamko la Serikali kwa sasa elimu inatolewa bila malipo, lakini wapo wazazi ambao wanapeleka watoto shule kwa gharama ya takribani kuanzia shilingi 600,000 mpaka Shilingi milioni moja kwa mwaka na ni shule ya Kata. Kwa namna gani?
Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari Mlola, watoto wanaotoka Makanya, hilo ni Jimbo la Lushoto, wanakwenda umbali wa zaidi ya kilomita 20 kuifuata elimu ya sekondari. Kinachotokea ni nini? Hawana uwezo wa kutembea kilomita 20, kwenda na kilometa 20 kurudi nyumbani. Wazazi wanalazimika kuwapangishia vyumba waishi karibu na shule ili waweze kupata elimu hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mzazi anakodi pango la chumba cha mtoto aweze kwenda shule, mzazi ananunua godoro, mzazi ananunua vyakula, anamwekea mtoto ili aweze kwenda shule. Huku nyumbani mzazi huyu usisahau ni yule ambaye tunampa TASAF kila mwaka kwa ajili ya kujikimu maisha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kinachotokea kwenye Wilaya ya Lushoto mahususi, wazazi wengi na nimefanya mikutano nao, wametamka wenyewe. Wamesema, wanafikia mahali hawashawishiki na kuwasaidia watoto wao kufaulu mitihani ya darasa la saba, na wengi wanazungumza na watoto wao wafeli mitihani ya darasa saba ili kumpunguzia mzazi adha ya kuongeza hii gharama ya kumpeleka mtoto shule ya sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo hili limetokea, Mheshimiwa Mkenda ana taarifa nalo. Kwenye Wilaya ya Lushoto, Tarafa ya Mlola tuna upungufu wa watoto watoto 1,600 ambao walipaswa kwenda sekondari kwa mwaka huu hawaja kwenda, kwa nini? Kwa sababu hawajafikia kiwango cha ufaulu kilichotakiwa kwa mwaka 2022. Kwa nini? Kwa sababu wazazi wamekaa na hao watoto wakakubaliana wafeli. Kwa nini? Kwa sababu gharama ya kumsomesha huyo mtoto kwenye shule ya kata ni kubwa mno. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunazungumzia elimu bila malipo, lakini wanaonufaika nayo ni wale ambao wanaishi karibu na hizo shule. Wale wanaoishi mbali na shule hizo, hawafurahii elimu inayotolewa bila malipo. Wanalipa gharama kubwa mno kwa ajili ya kusomesha watoto wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nini kifanyike? Kwanza kabla ya nini kifanyike, hoja hii tafsiri yake ni nini? Halmashauri ya Lushoto kwa mfano, makusanyo yake kwa mwaka ni around Shilingi bilioni 1.5 mpaka point 7. Watoto 1,600 ambao hawafanikiwa, maana yake kuna gap, kwa maana kila darasa lina upungufu wa watoto kuanzia 15 mpaka 20. Kwa maneno mengine, tafsiri yake ni kwamba, kuna vyumba vya madarasa ambavyo havina watoto kabisa wa kusoma.
Mheshimiwa Spika, tumepeleka fedha kila darasa lijengwe kwa Shilingi milioni 20. Ukiangalia hao watoto 1,600 vyumba vya madarasa vinavyohitajika ni takribani 40. Vyumba 40 mara 20,000 ni shilingi milioni 800. Kwa hiyo, tumepata hasara kwa kila mwaka ya shilingi milioni 800. Makusanyo yetu ni Shilingi bilioni 1.5 mpaka
7. Tunakwenda taratibu sana, hatuwezi kupiga hatua ya maendeleo kwa mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeishauri Serikali, kwanza tunapozungumzia suala la ujenzi wa mabweni, tunapozungumza sasa, Wilaya ya Lushoto, Wilaya ya Kilindi na Wilaya ya Korogwe Vijijini, ni jambo ambalo mlichukulie kama special case. Ni jambo ambalo linahitaji jicho la tatu la Serikali. Hali ni mbaya, elimu inashuka, na hatutaweza kuipandisha.
Mheshimiwa Spika, mimi ni mwalimu by professional. Hatutaweza kupandisha kiwango cha elimu kwa kupeleka key performance indicator. Huu unakuwa tayari ni mgogoro. Mheshimiwa Kairuki, nikushauri dada yangu, kama kuna sehemu unataka kutengenezea mtego, ni huu mpango au huu mkataba wa key performance indicator. Mwalimu amekuwa ameshaandaliwa chuoni, ana uwezo wa kumfundisha mtoto afaulu kwa mujibu wa taaluma yake. Ukimpelekea mpango nje ya taaluma yake, unamtoa kwenye reli aache kufundisha, aanze ku-deal na mpango ambao umepelekwa na TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, mara nyingi tunasema, TAMISEMI watusaidie jambo moja, yale masuala yanayohusu taaluma, wawaachie Wizara ya Elimu wayafanye. Wafanye yale mambo ambayo ni ya miundombinu; kujenga madarasa jengeni, kujenga barabara jengeni, lakini suala la taaluma ni sehemu nyeti ambayo inapaswa isimamiwe na wenye taaluma yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo Mheshimiwa Waziri nataka nikwambie, kuna kamgomo baridi, usipoangalia katatokea Dhahiri. Walimu hawaridhiki na namna ambavyo wanapelekewa maagizo na maelekezo mbalimbali kutoka TAMISEMI. Walimu wanaona mnaiacha professional yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niseme wazi, hiki mnachokifanya kwa walimu, hebu mjaribu kupeleka afya, mjaribu kupeleka kwenye taaluma nyingine. Kwa nini muichezee taaluma ya walimu peke yake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali, kama lengo ni kuongeza ubora, kunyanyua ubora wa elimu Tanzania, boresheni maslahi ya walimu, watajiongeza. Kama lengo ni kuongeza ubora wa elimu Tanzania, pelekeni crash programs, wafundisheni huko, waboresheni na wafundishwe na wataalamu waliowafundisha kwenye vyuo vyao. Wataboreka na elimu yetu itakuwa nzuri zaidi; lakini hili suala la kupeleka mikataba ambayo haipo kwenye taaluma, inakwamisha shughuli za walimu na mwisho wa siku haitatuweka kwenye nafasi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)