Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa nafasi. Naomba niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri inayofanyika katika majimbo yetu lakini na Taifa letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, wana-Misenyi wamehemewa kwa mambo mazuri ambayo yamefanyika ndani ya miaka miwili ambayo nitayataja kama sehemu ya pongezi kwa wana-Misenyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hatuwezi kumpongeza Mheshimiwa Rais bila kuwapongeza pia wasaidizi wake; na nikianza na Waziri wetu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Naibu Waziri ndugu yetu Ndejembi na Daktari kwa kumsaidia Waziri kufanya kazi nzuri. Niseme dada yetu Mheshimiwa Waziri umeanza vizuri; na kwa mikutano ambayo unatuunganisha katika mikoa kabla ya kuja kwenye bajeti ukaona mapungufu yanayohitajika ni sehemu ambayo umeupiga mwingi na Mwenyezi Mungu aendelee kukuongoza katika hilo.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na Wizara kufanya vizuri lakini katika ngazi za Mikoa tumeona viongozi wetu ndani ya mikoa wanafanya kazi nzuri ya usimamizi; na hivyo nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila na RAS wake Pamoja na viongozi wote. Niseme ndugu yangu Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunakuelewa wana Kagera piga kazi na endelea kutusimamia katika Mkoa wetu. Lakini pia na uongozi wa Wilaya ya Misenyi, nikitambua Mkuu wangu wa Wilaya, Madiwani wote, Mkurugenzi pamoja na watumishi, wote tunafanya kazi kwa umoja na ushikamano ndio maana mambo yanaonekana ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa tunaongea lugha nyingine ndani ya Wilaya ya Missenyi. Tunayo Hospitali mpya ndani ya miaka miwili, tuna vituo vya afya vipya viwili na pia zipo zahanati za kutosha na Serikali bado mnaendelea kutuletea fedha ambazo tunaendelea kujenga majengo mengine. Lakini leo tunasimama ndani ya miaka miwili tuna shule ya sekondari mpya, madarasa 53 mmetuletea na leo Mheshimiwa Waziri tumepokea barua kupitia Mradi wa BOOST tunaenda kujenga shule ya Msingi mpya na madarasa mengine 20; ni pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo sasa wana- Misenyi bado wanayo mahitaji mengi kwa nia njema kwa sababu wameshaonjeshwa maendeleo mazuri wanapenda maendeleo sasa yaendelee kufika mpaka ngazi za vitongoji.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Misenyi, kama ambavyo alitangulia kusema kaka yangu Mheshimiwa Jasson Rweikiza Mkoa wa Kagera kwa ujumla tuna mvua takribani asilimia 80 ya muda wote wa mwaka. Nimeona Mheshimiwa Waziri umekuja na utaratibu mpya, bei elekezi hizi za ujenzi wa madarasa mabweni na vyoo; hii model uliokuja nayo tuombe uipeleke pia na kwenye upande wa ujenzi wa barabara. Ukitoa bajeti linganifu katika mikoa yote na majimbo yote kwa sehemu ambazo tunapata mvua kubwa hiyo bajeti inakuwa haitoshi. Wana-Missenyi wanatambua kuwa miaka miwili nyuma tulikuwa tunapata milioni 700 lakini leo tunapata bilioni 2.4, ni ongezeko kubwa sana, lakini bado uhitaji ni mkubwa.

Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa miundombinu imeendelea kujengwa mpaka katika maeneo ya vitongoji mahitaji ya barabara yameongezeka; na sisi Wilaya ya Misenyi tumeleta maombi ya kuongeza mtandao wa barabara kilomita 131.7. ninachoomba naomba Mheshimiwa Waziri aipokee na reflection ya bajeti ya Wilaya ya Misenyi kwa mwaka huu katika kilomita zetu tulizokuwa nazo 921.7 basi mwaka huu 131.7 iongezeke tuwe na mtandao wa kilometa 1,053 ili tuweze kufika kule amabako Mhehsimiwa Rais amepeleka shule, amepeleka zahanati na amepeleka vituo vya afya. Niombe sana katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine, mwaka juzi tulijengewa barabara ya lami ambayo ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyeko madarakani. Kutoka Hospitali Teule ya Mgana tukajenga kilometa 1.2, kipande kilichobaki ni kilometa 4.6. Hatupendi kulalamika Mheshimiwa Rais akija kwetu najua ipo ndani ya uwezo wa Mheshimiwa Waziri. Mwaka huu tuongezewe bajeti tuendeleee na kilomita angalau mbili ili angalau mwaka unaokuja angalau tuweze kumaliza barabara hiyo na wananchi waweze kuona ahadi njema Mheshimiwa Rais inaweza kutekelezwa kwa wakati. Najua hilo Mheshimiwa Waziri analiweza.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kwenye upande wa afya ambapo wana-Misenyi wanamshukuru Mheshimiwa Rais, tunavyo vituo vya afya vipya viwili; lakini issue ni vifaa tiba. Wilaya ya Misenyi hatujapata vifaa tiba kabisa; lakini pia suala la watumishi, kama wenzangu walivyoongea, tuombe sasa tuweze kuongezewa watumishi ili wananchi waweze kupata huduma inayotakiwa. Pia kwenye mpango unaokuja, zipo kata za kimkakati ambapo tukipata vituo vya afya katika Kata za Buzinga, Buyango, Kitoga, Bugandika, Kilemile, Mabale, Mtukura na Minzilo angalau kwa Wilaya ya Misenyi kwa coverage iliyopo ya huduma za afya utakuwa ume cover vizuri na wananchi wataendelea kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni ombi la wana-Misenyi. Pamoja na kushukuru kwa shule mpya ambayo tumeletewa, na madarasa ya msingi manne nimeshapeleka ombi kwa Mheshimiwa kwako ka kushirikiana na uongozi wa Wizara yangu kupitia Katibu Tawala wa Mkoa. Kuna mabadiliko kidogo naomba ayabariki, yatakuwa yana-reflect hali halisi na uhalisia kwenye ground kule. Kwa hiyo hili nitakuwasilishia nitaomba ulibariki ili tuweze kwenda vizuri na wananchi waendelee kushukuru kwa kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, lingine niende kuomba kwa upande wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FLORENT L. KYOMBO: …naona umewasha king’amuzi; basi nikushukuru, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.