Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa nakupongeza wewe kwa kazi nzuri unazozifanya. Ni ukweli usiopingika wewe ni kichwa, unafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu kipenzi Dkt. Samia Suluhu kwa kazi nzuri anazozifanya. Waheshimiwa Wabunge ni ukweli usiopingika Mheshimiwa Rais anahangaika sana huku nahuku kutafuta pesa, ana uchungu na nchi yake, anataka nchi yake ipate maendeleo mapema. Mama ni mama tu, mama tuko nyuma yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Angela Kairuki, pamoja na Manaibu kwa kazi nzuri wanazozifanya, lakini pia nawapongeza Mawaziri wote wakiongozwa na jembe Mheshimiwa Jenista Mhagama na Manaibu Waziri kwa kazi nzuri wanazozifanya. Nampongeza mkuu wetu wa Mkoa, Yahya Dhewanda, anafanya kazi vizuri, anasimamia pesa za maendeleo, anazunguka huku na huku, majimbo yote anafanya ziara anasikiliza kero za wananchi na kutatua kero za wananchi. Simiyu tunapaa hatutembei, Mheshimiwa mkuu wa Mkoa unafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kutupatia pesa Wilaya ya Itilima kujenga hospitali ya Wilaya, zaidi ya bilioni nne. Haitoshi, wakatupatia milioni 800 kununua vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hospitali ya Wilaya ya Itilima hakuna uzio. Hospitali ya Wilaya ikikosa uzio ni hatari sana. Mtu anaweza akatokea popote pale kuivamia hospitali na hospitali ile ina wodi nzuri za kisasa na vifaa vyote vipo, wananchi wanalazwa pale. Ni mbaya sana, tunaiomba Serikali itupatie pesa tuweze kujenga uzio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali itujengee ma-corridor ya kupitisha wagonjwa. Hospitali ya Itilima haina corridor za kupitisha wagongwa. Vilevile hatuna generator, pindi umeme ukikatika upasuaji hauwezi ukaendelea. Tunaomba Serikali ibaini hospitali zote za Wilaya nchi nzima ambazo hazina generator iweze kununua generator. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Hospitali yetu ya Wilaya ya Itilima kuna mortuary, hatuna fridge. Tunaiomba Serikali itununulie fridge ya mortuary. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunaomba tujengewe mashine ya kufulia, hatuna jengo la mashine ya kufulia. Wilaya ya Itilima hiyohiyo ina zahanati kumi, ina vifaa vyote, lakini haina watumishi. Tunaomba Serikali ituletee watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na mama yetu kipenzi, Mama Samia Suluhu, imetupatia zaidi ya bilioni tatu kujenga hospitali ya Busega. Busega tuna vituo vya afya, Kituo cha Afya cha Mkula kina upungufu wa maabara, wodi na nyumba za watumishi. Kituo cha Afya cha Kasamo kina upungufu wa wodi na nyumba za watumishi. Kituo cha Afya cha Badugu kina upungudu wa maabara na nyumba za watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile naendele na pongezi za hospitali ya wiyala. Naendelea na pongezi za hospitali za Wilaya kwa sababu gani, hospitali za Wilaya zimesaidia watu sana. Sisi Mkoa wa Simiyu tulikuwa na hospitali moja ambayo ni Somanda tu, hizi zote ni hospitali mpya, naipongeza Serikali kwa kutoa zaidi ya bilioni tatu kujenga hospitali ya Wilaya Bariadi iDC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Bariadi tuna hospitali kongwe ambayo ni Somanda, ni ya kwanza kabisa katika Mkoa wa Simiyu, lakini haina jengo la dharura. Tunaomba Serikali itupatie pesa ili tuweze kujenga jengo la dharura na kuna vituo vya afya Ng’wang’wali na Ngulyati hawana vifaa tiba tunaomba Serikali ituletee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee na pongezi kwa Maswa. Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha hospitali ya Maswa. Hospitali ya Maswa imeboreshwa, ina wodi zote, tumejengewa theatre na tumejengewa jengo la dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi kwa Maswa kuna zahanati nne hazina watumishi, tunaomba Serikali itupatie watumishi. Kuna kituo cha afya cha Mwasai kimekamilika, lakini hakina wodi na jengo la mama na mtoto tunaomba liweze kukamilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa hospitali ya Wilaya ya Meatu imeendelea kuiboresha. Kuna ombi Wilaya ya Meatu, kuna kituo cha afya cga Mwandoya, ni kikubwa sana, ukikiona hivi unaweza ukafikiria kwamba, ni hospitali ya Wilaya, kinahudumia watu zaidi ya laki moja. Naiomba Serikali kituo hicho kiweze kupandishwa hadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, elimu, namshukuru Mheshimiwa Rais wangu kwa kutoa pesa kujenga madarasa, nchi nzima amejenga madarasa. Mheshimiwa Rais kwa kazi hii ya kujenga madarasa na kuboresha madarasa mazuri yana vigae na madawati mazuri, hao wanafunzi wanaosoma shule hiyo nakwambia wanafunzi hawa hawawezi wakamsahau Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Kengele ya pili imegonga. Sekunde 30, unaomba?

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, ombi langu naomba shule za kata za sekondari waweze kujenga mabweni…

SPIKA: Waheshimiwa mnaotembea mbele ya mchangiaji mketi. Subiri kwanza, eenhee, haya endelea. Malizia hizo sekunde 30.

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, lakini vilevile naomba tuweze kuongezewa watumishi, tuna upungufu mkubwa wa watumishi Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)