Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala huu wa bajeti ya TAMISEMI. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nikushukuru wewe kwa jinsi unavyoongoza Bunge letu, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anapambana katika kuhakikisha kwamba, Taifa letu linasonga mbele.

Mheshimiwa Spika, nisiache kumshukuru Mkuu wangu wa Mkoa, Ndugu yetu Mongela, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kwa uaminifu na uadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe niseme mambo yafuatayo ambayo kwa kweli, bajeti hii ni bajeti nzuri ambayo tumewasilishiwa na Waziri wetu Mheshimiwa Kairuki. Lakini nisiache kusema kwamba, miundombinu ya Jimbo la Arumeru Magharibi hali sio nzuri kwa sababu mafuriko yamelikumba jimbo hilo na wananchi wanateseka sana sasa kwa kukosa barabara ya kupitia.

Mheshimiwa Spika, TARURA inafanya kazi nzuri ambayo hakuna mtu anayepinga na Bunge hili linaendelea kuipongeza TARURA, lakini barabara yangu katika Jimbo la Arumeru Magharibi kuna barabara ya Hospitali ya Oturmeti na yenyewe haipitiki. Barabara ya Loning’o kwenda Mringa imekatika daraja. Barabara kutoka Mnadani kwenda Hospitali ya Oturmeti imekatika, hivyo naiomba sana Wizara kupitia Waziri wetu aone namna gani tunapata fedha za dharura kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, maeneo haya yaliyokatika yanaweza kutengenezwa mara moja kwa sababu, wananchi wanateseka.

Mheshimiwa Spika, lakini ningeomba TARURA iongezewe fedha kwa sababu, katika Jimbo la Arumeru Magharibi tuna barabara nyingi ambazo sasa hazipitiki kutokana na mvua hizi. Barabara ya Sanawari – Oldonyosambu hali ni mbaya, Barabara ya Malalua – Nduruma – Bwawani hali sio nzuri, Silent Inn – Freedom sio nzuri, Barabara ya Kisongo – Musa sio nzuri, madaraja yanakatika. Barabara ya Kigarai – Likamba hali sio nzuri, Barabara ya Lemanyata – Orkokola Kituo cha Afya sio nzuri, Barabara ya Kilima Moto – Mwande – Kingalaoni sio nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri, ujue Jimbo la Arumeru Magharibi lina kata 27, vijiji 86, vitongoji 268. Tuangalie kwa jicho la huruma Jimbo la Arumeru Magharibi kwa sababu wananchi wanateseka kutokana na maeneo ya maporomoko ya maji na barabara ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mgawo wa fedha tuione Arumeru kama ni sehemu na yenyewe ya kupata fedha za kutosha. Na niombe TARURA iongezewe pesa kwa sababu, pamoja na kufanya kazi nzuri TARURA isipoongezewa fedha haya yote tunayoyasema hayawezi kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la ajira, sisi Wabunge hapa tulipo na hapa nilipo nina message zaidi ya mia mbili, mia tatu, vijana wanasema tutafutieni ajira kwa sababu, bila connection, kama hakuna connection ina maana hatupati ajira. Jambo ambalo sio sawa kwa sababu, Serikali haitoi ajira kwa connection, Serikali inatoa ajira kwa usawa kwa wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe kusema basi, ajira hizi zigawanywe kwa mikoa na badae hata kwenye mikoa zigawanywe kwenye Wilaya, ili tuweze kupata usawa katika kugawa ajira hizi, ili kuondoa hii sintofahamu ya vijana wetu ambao kwa kweli, wanaendelea kuzungumzia kuhusu suala la connection, jambo ambalo halipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la posho ya Madiwani na Wenyeviti wa vijiji na vitongoji. Kama Serikali imeweza kuchukua suala la Madiwani ikalipa hiyo posho ya mwezi, zile fedha ambazo zilikuwa zinalipwa na halmashauri kwa nini isiunganishwe hapo ikawasaidia Madiwani, ikajumlishwa ikawasaidia hawa Madiwani? Ikawa ni sehemu kabisa ya kuhakikisha kwamba, wanapata mshahara? Kwa sababu, kama tunavyopeleka billions of money kwenye Halmashauri kwenda kumsimamia mkurugenzi anayelipwa labda milioni nne au milioni kadhaa, yeye analipwa posho, hatuoni kwamba, tunapoteza fedha nyingi kwa sababu ya usimamizi mbovu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana hili suala la sehemu ya Madiwani iangaliwe, lakini pia Wenyeviti angalau na wao waangaliwe. Wenyeviti wa vitongoji na vijiji waangaliwe kwa sababu, wanafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la umaliziaji wa maboma. Wananchi wamejenga maboma mengi ya zahanati na vituo vya afya na hata madarasa. Ningeomba sana hili eneo liangaliwe kwa sababu, ni eneo muhimu kwamba, tukiwavunja wananchi nguvu kwa sababu, wanachangia na hatimaye wasione nguvu ya Serikali ikimalizia hizo zahanati za kutoa huduma kwa kweli, itakuwa ni kuwavunja moyo na kazi hiyo haitakuwa imekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na umaliziaji wa maboma kumekuwepo na shida kubwa sana katika suala la vifaa tiba katika zahanati na vituo vya afya n ahata hospitali ya Wilaya. Hospitali ya Wilaya ya Oturmet tangu Serikali imeanza kugawa migao ya fedha kwa ajili ya Hospitali za Wilaya hospitali hiyo haijawahi kupata hata shilingi kumi ya mgawo wa Serikali kwa ajili ya kupanua hospitali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hospitali hiyo imepandishwa hadhi na Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Kikwete mwaka 2012, lakini haijawahi kupata hata senti. Nimekuwa nikiimba kwenye Bunge hili, labda sasa nifike mahali na mimi niimbe kimasai, labda nikiimba kimasai “laleiyo” ndio mtajua kwamba, hospitali hiyo inahitaji msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali hii sio nzuri kwa sababu, tunapoona maeneo mengine yanapata fedha zaidi ya bilioni tatu, bilioni nne, lakini hata shilingi milioni 500 hospitali ya Wilaya haijapata, si sawa. Naweza kufika mahali nikasema siwezi kusema ni ubaguzi, lakini naweza kusema Serikali imesahau hospitali hiyo, ni kwa nini? Mheshimiwa Waziri naomba sana hospitali hiyo, ukifika pale huwezi kusema ni hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nimeona umewasha kipaza sauti. Nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)