Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Santiel Eric Kirumba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naanza kwa kuunga mkono hoja. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya, hasa kwa Mkoa wetu wa Shinyanga. Mama huyu ameonesha kwa vitendo wanawake tunaweza. Mama huyu ameonesha kwamba kipaumbele chake cha kwanza ni elimu, ameweza kutoa elimu bila malipo. Pia tumeweza kupokea bilioni sita za madarasa 336 kwa Mkoa wetu wa Shinyanga. Napenda kumwongelea Mama Samia kama ni mwanamke wa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Kairuki, kwa kazi kubwa anayoifanya, pamoja na Mkuu wetu wa Mkoa kwa kazi kubwa anazofanya kwa kushirikiana kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni moja, ya elimu. Napenda kujikita katika hoja ya elimu kuhusu chakula shuleni. Mwaka 2021 tulipitisha Mpango hapa wa Kitaifa chini ya TAMISEMI kuhusu kutoa chakula shuleni na mpango huu TAMISEMI walisema watausimamia kwa namna moja kwa kishindo. Hata hivyo, mpango huu nikianza kuuongelea kwa Mkoa wetu wa Shinyanga, umeweza kutekelezeka kwa shule 295. Kati ya shule tulizonazo katika Mkoa wa Shinyanga ambazo ni 609 ni shule 295 zinazotoa chakula cha mchana.

Mheshimiwa Spika, tumejenga madarasa mazuri lakini kwa Mkoa wa Shinyanga tunapata changamoto ya utoro kwa watoto wa shule kutokana na kwamba watoto wanaamka mapema, saa 12.00 kwenda shule, mpaka afike shule ni saa 2.00. Watoto hawa wanaondoka nyumbani hawajapata kifungua kinywa. Ukiangalia geographical area ya Shinyanga na Dar es Salaam ni tofauti. Shinyanga tunapoongelea saa 12.00 asubuhi bado ni giza. Mzazi anahamasika kumsindikiza mtoto wake ambaye ni darasa la kwanza mpaka la tano kuelekea shule. Mzazi huyu unakuta asubuhi hiyo hawezi kuamka na kumuandalia mtoto kifungua kinywa na hii huwasababisha Mkoa wetu wa Shinyanga kukabiliwa na udumavu wa afya, watoto kuwa watoro shuleni na kurudi nyuma kielimu. Shule nyingi hazifanyi vizuri kutokana na kwamba hawapati chakula shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watoto wadogo wa miaka saba mpaka 14 wanakwenda shule wanakaa kuanzia saa 1.00 mpaka saa 9.00 hawapati chakula. Kwa namna yoyote huyu mtoto hawezi kufanya vizuri shuleni. Naomba Mheshimiwa Waziri aridhie wale wadau ambao walijitokeza siku ile ambapo mdau wa kwanza ni PSI, alisema kwamba atatoa vyakula kwa halmashauri 295 za kanda ya ziwa. Naomba mpango huu waupitie tena ihamasishwe.

Mheshimiwa Spika, hapa ninapoongelea hawa watoto wanaokwenda shule, siyo hawa watoto wa international, hawa daddy I’m going, hapana, nawaongelea watoto ambao wanatoka familia duni ambao wazazi wao, mtoto huyu akienda asubuhi akirudi saa 9.00 anakula mlo mmoja kwa siku. Kwa hiyo Waziri aridhie, kama Rwanda, nchi jirani hapo walivyofanya, wamepunguza saa za kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuangalie, kama huu mpango hauwezekani, basi shule zianze masomo kuanzia saa 3.00 kuliko mtoto anavyoamka asubuhi hapati chakula anafika shule hapati chakula na kumfanya arudi nyuma kimasomo. Namna nyingine ni bora masomo yakaanza saa tatu asubuhi na pia tuangalie mitaala yetu. Mtoto mdogo wa darasa la kwanza anasoma saa tisa na masomo matano. Tuangalie namna ya kuboresha elimu yetu.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wetu wa Shinyanga tuna changamoto kubwa ya Walimu. Mpaka sasa Mwalimu mmoja anafundisha watoto 100 mpaka 105 ambapo TAMISEMI mwongozo wao unaelezea kwamba Mwalimu mmoja afundishe watoto 45, lakini pia tuna upungufu wa takribani walimu 5,000. Pia ukiangalia Wilaya ya Kishapu, Msalala, maeneo yale yana upungufu wa samani za Walimu katika nyumba. Mwalimu anakaa katika darasa siku nzima na ana-share vitendeakazi na wanafunzi, meza hakuna. Kwa hiyo napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aangalie namna ya kusaidia Walimu, kuwaboreshea mazingira yao ili waweze kufanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)