Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DUA W. NKURUA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Nanyumbu kwa kunifanya kuwa kiongozi wao kama Mbunge na kuwa msemaji wao katika eneo hili, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa anazofanya ambazo kila mtu mwenye dhamira ya kweli katika nchi yetu ni lazima amuunge mkono, kwa sababu analengo la kuwafanya Watanzania waishi maisha mazuri na Tanzania iwe sehemu salama ya kuishi watu. Nampongeza sana Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nianze kuchangia katika suala la elimu.
MHE. DUA W. NKURUA:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Katika suala la elimu ni dhahiri kwamba, mkakati ambao umekuja na TAMISEMI unaonesha una dhamira ya kweli ya kupambana na hali halisi tuliyonayo sasa hasa ya mfumuko kwa watoto ambao wamezalishwa utokana na tamko na Sera ya CCM inayotamkwa kwamba, sasa elimu itakuwa bure.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali kama hii ni lazima Serikali ijipange vizuri kuhakikisha kwamba yale mambo ya ziada ambayo lazima yaongezeke Serikali ianze kuweka mkakati. Kwa sababu tuna ongezeko kubwa la watoto tutahitaji Walimu wengi, tutahitaji nyumba nyingi za Walimu, tutahitaji madarasa ya kutosha kwa ajili ya kuweza kukabiliana na hawa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hii tusiziachie Halmashauri peke yake kujenga nyumba za Walimu na kuongeza madarasa, kwa sababu mapato ya Halmashauri nyingi nchini ni madogo sana. Kwa hiyo lazima Serikali ije na mpango utakaozisaidia Halmashauri kujenga nyumba za Walimu, madarasa na vifaa vingine. Waziri atakapokuja aje na mkakati akaotuonyesha kwamba tumejiandaa kukabiliana na ongezeko kubwa la watoto katika mashule yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili, ni kuhusu suala la maji, maji ni tatizo katika nchi yetu hasa katika Jimbo langu la Nanyumbu. Kutokana na hali halisi ya mazingira na uoto
tuliokuwa nao maji ni tatizo kubwa sana. Nashukuru bajeti hii imejitahidi kuonesha mikakati mbalimbali katika nchi nzima ya kupambana na shida ya maji, lakini naiomba Serikali iweke mkakati maalum na wa kipekee, kuliondoa tatizo la maji katika Mji wa Mangaka ambapo ndiyo Makao Makuu ya Wilaya na Nanyumbu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mtwara kwa ujumla una shida kubwa sana ya maji, naomba Serikali ijipange kama ambavyo imeshatoa maelezo na nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba, wananchi wa Tanzania wanapata maji ya kutosha ili waweze kufanya shughuli zingine za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maslahi ya Madiwani na Wenyeviti wa Halmashauri za Vijiji. Waheshimiwa Madiwani wanafanya kazi kubwa sana katika maeneo yao ya kazi, kila tatizo linalotokea katika maeneo yetu, watu ambao wananchi wanakwenda kuwafuata moja kwa moja ni Madiwani. Kwa hiyo, Madiwani ni lazima tuwatengenezee mkakati utakaowapa maslahi yatakayoweza kusaidia kukabiliana na kazi ambazo zinawakabili kwa sasa.
Naomba maslahi ya Madiwani yaangaliwe na Wenyeviti wa Vijiji walipwe mshahara. Mkakati huu lazima uanzie huku Serikali Kuu, Halmashauri hazina uwezo huu ambao tunauzungumza leo.
Naomba Serikali iwalipe Wenyeviti wa Vijiji nao ni watu wanaofanya kazi kubwa sana k
atika nchi yetu, tusipowaangalia hawa tutakuwa hatutendi haki.
Naomba suala hili tulipe kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichangie asilimia 10 ambayo inapaswa iende kwa Vijana na akinamama, ni kweli Halmashauri nyingi nchini hazitengi pesa hii, hata kama zinapata mapato haya lakini hazipeleki asilimia 10 ya mapato yao. Naomba tutengeneze mpango ambao utakuwa endelevu na mpango ambao utazifanya Halmashauri ziweze kutimiza hiki kigezo, kwa sasa kuna mambo yanawashinda kufanya hii kazi ambayo tumewapa waifanye.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba, asilimia 60 ya mapato ya ndani ya Halmashauri yanatakiwa yaende kwenye miradi ya maendeleo, asilimia 20 ya mapato ya Halmashauri ya ndani yanatakiwa yaende kwenye vijiji, asilimia 10 iende kwa wanawake na vijana. Asilimia 10 peke yake maana 90 tayari tumeshazigawa, kumi peke yake ndiyo ifanye kazi zingine ikiwa ni pamoja na posho za Madiwani, kuendesha vikao na kadhalika. Kwa sababu OC ambayo ingekwenda kule kusimamia posho za Madiwani na vikao haziendi kwa wakati. Kwa hiyo, inalazimu Halmashauri zitumie pesa ambazo zingeweza
kwenda kwa akinamama na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunataka kweli wanawake na vijana wapate pesa ni lazima Halmashauri zetu tuziongezee pesa, hii asilimia 10 tuliyowapa ni ndogo, tukumbuke kwamba Halmashauri zinalipa mchango wa ALAT-Taifa, Halmashauri zinalipa mchango wa ALAT-Mkoa, Halmashauri zinalipa loans board, asilimia 10 ile ndiyo inafanya hiyo kazi, katika hali hii unatekeleza vipi hili agizo, ni vigumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakwenda kuwalaumu Waheshimiwa Wabunge hapa, Madiwani kule, tutawalaumu Wenyeviti wa Halmashauri, tutawalaumu Wakurugenzi lakini uhalisia haitekelezeki. Hao Madiwani ndiyo wanaosimamia hizi pesa ambazo tunazipeleka kwao, kikao hakifanyiki kwa sababu hawana pesa watasimamia vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, asilimia 10 iliyobaki haiwezi kumudu kuyafanya haya ambayo tunataka yafanyike, mazingira ni magumu sana tumewatengenezea hao watu.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana tuheshimu bajeti, hapa tunajadili bajeti na hatimaye itapita. Naomba sana mambo yatakayopitishwa hapa yafanyike hayo hayo yasiongezeke njiani wala yasipungue njiani. Tuna uzoefu wa kutosha kwamba, mara baada ya bajeti yanatokea maagizo mengine ambayo Halmashauri sasa yanawachanganya. Ni kweli maagizo yanakuwa na lengo zuri kwa mfano, tutengeneze madawati kwa watoto wetu ni jambo jema,
lakini halipo kwenye bajeti! Tunawaambia tujenge maabara ni jambo jema, lakini haikuwa kwenye bajeti. Kwa hiyo, kwa sababu haipo kwenye bajeti kinachotokea hao Waheshimiwa Madiwani na Wakurugenzi wanakwenda kuharibu mipango mingine ambayo ilipangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaambia kwamba, wao watenge asilimia 10 ya mikopo ya akinamama na vijana maana tunalalamika sana Waheshimiwa Wabunge, mikopo, mikopo, Wakurugenzi hawatengi, watatengaje wakati wameambiwa wapeleke madawati na wamepewa deadline watafanya lini!
Wameambiwa maabara tarehe fulani iishe, pale kinachoendelea mipango mingine baadaye, kipaumbele ni madawati na mabaara.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kama tunaruhusu watu waendelee kupewa maagizo nje ya bajeti, tukubaliane kwamba na asilimia 10 inaharibika tusilaumu, tunyamaze, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, kama tumekubaliana na hii bajeti twendeni tuiheshimu. Kule Nanyumbu tunao Viongozi wa Jadi tunaita Mamwenye, wengine mnaita Machifu, wengine mnawaita Watemi. Mamwenye kwa mila yetu anaposimikwa na kufanyiwa sherehe, mtu wa kwanza kwenda kumuamkia ni Baba Mzazi na Mama Mzazi wa
yule Kiongozi. Hii ni massage kwa watu wengine kwamba, huyu anapaswa kuheshimiwa kuanzia leo. Sasa, kama kweli tunataka bajeti iheshimiwe mtu wa kwanza kuheshi
mu bajeti ni Serikali. Naomba sana Serikali tuheshimu
tutakayoyapitisha hapa ili ikatekelezwe kule kwa ufanisi ambao tumeutaka na
hapo tutakuwa tumetenda jambo jema.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huo nashukuru sana na
naunga mkono hoja.
(Makofi)