Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa nafasi hii ya uhai. Pia shukrani zangu zimuendee Rais Samia Suluhu Hassan kwa kweli kwa kutusaidia katika miradi ya maendeleo kwenye Jimbo la Mbulu Vijijini na sisi kule tumeanza kufanya kazi vizuri sana kwa slogan ile ya kazi iendelee.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, sisi tumeanza kupata slogan baada ya kazi iendelee sisi tumesema pale kwa pamoja tunaijenga Mbulu. Sasa nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba pamoja na slogan hii ya kufanya maendeleo tunayo matatizo ambayo nataka niyaseme.

Mheshimiwa Spika, hospitali yetu ya wilaya ni kati ya hospitali 67 zilizoanza kujengwa mwanzoni kabisa. Pamoja na ile flow ya kugawanywa kwa fedha za kujenga na kumalizia hospitali hiyo, kwa bahati mbaya tumerukwa kwa milioni 500. Kwa hiyo hospitali ile haijaanza kazi na kama imeanza kazi labda jana, maana yake ni kwamba haiwezi kuendelea. Tunaomba Waziri atupatie fedha, shilingi milioni 500 ambayo ipo katika flow ile ya kupatiwa hizi hospitali.

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, Kituo cha Maretadu Waziri ametoa milioni 200, tunahitaji milioni 300, naomba Waziri atuongezee ili tuweze kumaliza kile kituo. Kituo cha Haydom ambako sasa wametupatia fedha, kwa bahati mbaya sana tumejenga wodi ya wazazi lakini haina theater (chumba cha upasuaji). Kwa hiyo bahati mbaya sana ikitokea mama mjamzito anakwenda kujifungua na ikashindikana maana yake ni kwamba operation haifanyiki kabisa na Mheshimiwa Waziri ni mama, aangalie hilo.

Mheshimiwa Spika, lingine, kuna vituo vya afya vitatu vimejengwa na wananchi na viko kwenye hatua mbalimbali; Vituo vya Masieda, Gembak na Labay; naomba Waziri atufikirie katika hilo kwenye bajeti yake. Najua kwenye Wizara yake Mheshimiwa Waziri hajaweka hiyo, lakini naamini yeye ni mama na kwa ajili hiyo atatusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi, alikuwepo Mheshimiwa Bashungwa kabla ya Mheshimiwa Waziri na alikuwa Waziri kwenye ofisi hiyo, ametoa ahadi na leo bahati nzuri yuko mbele yangu ananisikia vizuri sana hapa, kuna ahadi ya kujengewa mabweni kwenye Shule hizi ya Getanyamba, Masieda, Labay na Maga na ametuahidi pia maabara ambayo nina uhakika Mheshimiwa Waziri ananisikia, lakini yeye amepelekwa Ulinzi na Waziri sasa yuko hapo, naomba atusaidie kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi kuna tatizo la ukuaji wa maeneo yetu ya utawala, hasa kata, vijiji na vitongoji. Leo hii najua tumesomeshwa sana habari ya mgawanyo huu. Ombi langu ni kwamba TAMISEMI waangalie namna gani waruhusu vijiji na kata ambazo ni kubwa ili walau ziweze kugawanyika, vinginevyo kwa sasa hivi havitawaliki. Kwa hiyo hilo ni ombi kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, lingine kubwa ni huu mgawanyo wa ajira mpya. Kwa sababu muda ni kidogo ningetoa vielelezo jinsi ambavyo ajira mpya zinatutesa kule majimboni. Walimu wetu wengi sana wanajitolea katika shule zetu nyingi na wameona kama slogan hiyo itawasaidia kupata ajira. Walio wengi wanajitolea. Nimwombe Mheshimiwa Waziri aangalie sana, huu mgawanyo utakaotokea aangalie kwenye majimbo au halmashauri ili wanapoajiriwa, basi tuone kwamba maeneo yote yapatikane hizo nafasi kwa uwiano.

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi Serikali imeacha sasa kuajiri maendeleo ya jamii na sekta hii kama imeachwa sana. Ombi langu, wakiacha kuajiri maendeleo ya jamii ni wazi kwamba miradi yetu itakuwa na shida kwa sababu wananchi watashindwa kuelimisha na matatizo ya kijamii yatakuwa mengi. Wafungue dirisha hilo.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameachia dirisha hili la Walimu, waone basi kwenye sekta nyingine za maendeleo ya jamii na nyingine ambazo kimsingi zinasaidia ajira hizi.

Mheshimiwa Spika, ombi lingine, wameshachukua yale madaraka ya kule vijijini. Watendaji wa Kata sasa hivi wanaajiriwa toka Central Government (Serikali Kuu); warudishe kule kwenye halmashauri zile ajira ili ziweze kufanyiwa kazi kule wilayani.

Mheshimiwa Spika, hizi za watendaji wa kata, ni kweli Sekretarieti ya Ajira imepewa uwezo huo wa kuajiri na kusimamia kule katika maeneo yetu, lakini nataka nikwambie, unaweza ukapata nafasi 20 za kuajiri katika halmashauri yako, lakini utashangaa katika wanaokwenda kuajiriwa, najua ni nchi nzima, sina ubaguzi, lakini utashangaa kwenye eneo hilo hata mtu mmoja anaweza asitokee kwenye ajira 20. Sasa ombi langu; wawape nafasi Baraza la Madiwani nalo lione kama inaweza kutia input kule ili walau tuwe na ajira ambazo zinakuwa sawa.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo naona lazima nitoe kama tahadhari; hata wanapokwenda kuajiri sasa hivi hii ya Walimu, waone hata yale majina wanayoletewa wayahakikishe, je, yanatoka kweli huko katika maeneo yetu na hawa wanaojitolea ndio hawa kweli wanaojitolea? Isije ikawa afisa fulani akafanya ujanjaujanja ukashangaa tumefikia mahali wanaajiriwa watu wengine ambao pia hawakuwa wamejitolea.

Mheshimiwa Spika, ombi langu; amejitolea mtu, kafanya kazi kwa miaka kadhaa, naomba aajiriwe. Tena waanze kwa kutumia chronological order, kwamba 2015 aajiriwe, kwenda 2016 waajiriwe, kwa kuendelea namna hiyo. Siyo unashangaa 2015 mtu ameshamaliza chuo lakini anaajiriwa wa 2022; itakuwa ajabu. Tunataka kujua, je, hizo ajira, kama wamesoma chuo kimoja, wanakaa eneo moja, kwa nini wa 2020 aajiriwe na wa 2015 asiajiriwe?

Mheshimiwa Spika, naona umewasha mic, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nikupongeze wewe, Mungu akubariki sana maana wewe ni kichwa. Ahsante sana. (Makofi)