Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Moja kwa moja kwanza, nimuombe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aendelee kukubariki.
Mheshimiwa Spika, nataka kwanza nimpongeze Wakili, Mheshimiwa Angellah Kairuki, kwa kuja na hotuba nzuri sana ambayo inabeba na kuakisi maono ya Mheshimiwa Rais. Maono ambayo anataka maendeleo ya haraka. Hiyo katika hii miaka mwili ametuonesha, hivyo, mwaka huu wa tatu ambao tunakwenda nao sasa hivi Mheshimiwa Kairuki anaomba zaidi ya trilioni tisa katika bajeti yake. Naliomba Bunge hili liridhie kwa haraka sana ili tuweze kumpa nyenzo Mheshimiwa Waziri akafanyie kazi.
Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie masuala yanayohusiana na kupata hayo maendeleo ya haraka, kwamba lazima tufanye kazi kwa bidii sana. Hapa napenda ninukuu maneno ya CAG Mstaafu, Alhaj Mussa Assad katika mchango wangu. Yeye alikuwa anazungumzia mambo gani muhimu ya kuyafanya ili tuweze kupata maendeleo ya haraka na akasisitiza katika kufanya kazi kwa bidii. Anasema siku zako mbili zisiwe zinafanana. Maana yake unachokifanya leo, kesho kifanye bora zaidi. Hili ndilo tunaloliona kwa Mheshimiwa Rais, kwamba kila siku yeye analokuja na jambo lake moja, siku ya pili linakuwa ni jambo zuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa natazama nione hata wasaidizi wake, yasiwe ni masuala ya kila siku sawasawa na siku nyingine. Tunataka maendeleo ya haraka na kwa kutaka maendeleo ya haraka maana yake ni kwamba kila siku tunachokifanya tunakiboresha kuliko jana yake.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni quantum of work, kwamba tuwe na muda mwingi sana wa kufanya kazi. Siyo kila siku tunafanya kazi kwa kipindi kilekile tu, kwamba kuna kazi nyingine hazisubiri muda. Ndiyo maana unaweza ukashangaa viongozi wetu hawa, mfano Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, hata Mheshimiwa Angellah, unaweza ukazungumza naye saa 8.00 za usiku anaku-text, kwa maana huyo mtu anafanya kazi hata saa 8.00 za usiku. Hao ndio viongozi tunaowataka na hata kule chini kwenye halmashauri tukutane na viongozi wa sampuli hiyo. Siyo kiongozi ikifika saa fulani, saa 8.00, saa 9.00 anafunga mafaili anaondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, excellence. Kazi ambayo unaifanya lazima ujipime wewe, inakuwa bora kiasi gani, siyo bora kazi, kazi bora. Ndiyo viongozi tunaowataka. Sasa hayo unayakuta kwa Mheshimiwa Rais. Kila siku na kila Mbunge hapa akisimama anampongeza Mheshimiwa Rais, tunayataka haya yarudi kule chini, viongozi wa chini wamfanye Rais kama role model wao.
Mheshimiwa Spika, hili nalizungumza najaribu kuliangalia sana pale kwangu Kinondoni. Pale Kinondoni wakati nimepokea fedha za mwaka jana za Mfuko wa Jimbo. Mfuko wa Jimbo ule tukasema tukajenge eneo ambalo litatoa huduma za mama na mtoto, jengo la huduma ya mama na mtoto.
Mheshimiwa Spika, pale kulikuwa na eneo la wazi, watu wakilitumia kama soko. Wananchi wale nikishirikiana na Mheshimiwa Diwani wa pale ambaye anaitwa Mheshimiwa Mgana, tukaenda tukazungumza na wananchi wa pale kwamba ndugu zangu tunataka tujenge jengo kwa minajili ya kuwahudumia akinamama na watoto, tumepata fedha katika Mfuko wa Jimbo. Wananchi wale wakakubali kuhama eneo lile ili tuweze kujenga.
Mheshimiwa Spika, yote haya yanafanyika tukiwa na Viongozi wa Manispaa ya Kinondoni, wanaridhia. Baada ya kuridhia hata fedha zikahamishwa kutoka katika Mfuko wa Manispaa kupelekwa kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kata. Ajabu, baada ya muda kuna kiongozi, sitaki nimtaje kwa sababu hayuko hapa na hawezi akajitetea, lakini nitamwambia Waziri ni nani, anakwenda kule anafanya juhudi jengo lile lisijengwe. Kigogo ni eneo ambalo watu wengi sana pale ni maskini, hali zao ni za chini. Tunapowapelekea huduma kama zile tunawasaidia, lakini huyu mtu anaamua kudhoofisha juhudi za Mbunge, nasikia anataka kugombea Ubunge, nashangaa! Hugombei Ubunge kwa kuwaumiza wananchi. Kama unataka kushindana na Tarimba Abbas, come to me, usiwachezee watu. Wale watu wana matumaini yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hebu angalia lingine, Tandaleā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Haya, Mheshimiwa Tarimba, kengele ya pili imegonga, muda wetu umekwisha.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, lakini mfano mmoja unatosha, nawaomba tuipitishe hoja hii kwa nguvu sana. Ahsante sana. (Makofi)