Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, kupitia njia ya maandishi naomba kuchangia bajeti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Wizara hii ni muhimu katika ujenzi wa Taifa hili, lakini zaidi ya jukumu hili ni shughuli za Wizara hii zinawagusa Watanzania walio wengi na hasa walioko vijijini. Pamoja na majukumu ya Wizara hii ambayo kwa miaka miwili hii yametekelezwa kwa ufanisi wa kiwango cha juu nashauri na kuomba yafuatayo: -

Kwanza, Wilaya ya Muleba ina kata 43, tarafa tano na vijiji 166. Eneo hili ni nchi kavu na maji ya ziwa kwa uwiano wa asilimia 30 kwa 70 mtawalia. Tuna shule za msingi 250 zenye wanafunzi 158,000 wakifundishwa na walimu 2,287. Tunazo sekondari 70 zenye wanafunzi 47,890 kwa walimu 755. Katika shule tajwa hapo juu, shule 15 za msingi na moja ya sekondari ziko visiwani (square kilometer 7,600) eneo ambalo usimamizi na utendaji katika maeneo hayo ni mgumu na hatarishi. Tunaomba yafuatayo kwa ajili ya Wilaya ya Muleba: -

i. Sekta ya elimu hasa msingi Wilaya Muleba iongezwe toka shilingi milioni tisa mpaka milioni 17 kwa uwiano wa eneo, wingi wa shule, wanafunzi, walimu hudumiwa, lakini ugumu wa kukagua maeneo yote hasa visiwani.

ii. Shule ya sekondari ya Bumbiile ambayo iko visiwani iwe shule ya bweni ya Serikali. Hali ya visiwani ni ngumu sana, wanafunzi hutoka visiwa jirani kuja shule lakini visiwa vingine viko mbali mwanafunzi kumudu kwenda na kurudi. Hata wale wanaokwenda na kurudi kwa kutumia mitumbwi ni kutegemea huruma ya wavuvi na kuangalia hali ya hewa, ikichafuka ziwa halipitiki.

iii. Kwa wingi wa shule, msambao wa vijiji na kata tunaomba tuongezewe walimu kwa shule za msingi na sekondari.

Pili, Wilaya ya Muleba kwa kupitia TARURA imefunguka kwani maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki sasa yana barabara za uhakika. Pamoja na kazi nzuri hjyo tayari tulishaleta maombi maalum kwa ajili ya kujenga barabara ya kufungua Kata ya Rutoro na barabara ya Kimeya mpaka Burigi kwa kadirio la shilingi bilioni 4.9. Tunaomba nyongeza ya bajeti hiyo tusaidiwe kufungua maeneo hayo hali ambayo pamoja na kuchochea maendeleo italeta ustawi kwa wananchi.

Tatu, Wilaya ya Muleba ilianzishwa miaka ya 1970 lakini mpaka sasa haina hospitali ya wilaya. Tulipewa shilingi milioni 500 likajengwa jengo la OPD tangu hapo hakuna nyongeza ya pesa mwaka jana hata mwaka huu kwa ajili ya kuendeleza ujenzi hospitali hiyo.

Nne, kwa Jimbo la Muleba Kaskazini tunashukuru uboreshaji wa vituo vya afya vya Kamachumu na Izigo ili kufikia viwango vya vituo vya afya. Tunaomba sana uboreshaji huo uendelee ili vituo hivyo vifikie viwango vya kitaifa vya vituo vya afya. Kituo cha afya kilichoko kisiwa Bumbiile kinachojengwa kwa vyanzo vya ndani kimekwama yaani hakijakamilika. Mbali na utaratibu huo nilioueleza jimbo la Muleba Kaskazini halijawai kujengewa kituo cha afya katika utaratibu huu tunaouona kwa majimbo mengine nchini. Kupitia bajeti hii niombe tupate kituo cha afya Kata ya Ngenge eneo ambalo litahudumia Kata za Bulungula, Rutoro, Mushabago, Nyakatanga, Nsheshe na Ngenge yenyewe. Maeneo haya kwa pamoja hayana kituo cha afya na kadirio la watu ni zaidi ya 80,000.

Mheshimiwa Spika, tano, Jimbo la Muleba Kaskazini wananchi wake wanao utamaduni wa kushiriki maendeleo kwa kujenga shule na zahanati. Kutokana na mrundikano wa wanafunzi katika baadhi ya shule hasa ya msingi na kutokana na hizo shule kuwa na vyumba vichache au vyumba vilivyochakaa wananchi wameanzisha shule mpya ili kurekebisha mapungufu hayo. Tatizo kwa jimbo la Muleba Kaskazini ni kuwa miradi hiyo iliyobuniwa na wananchi haisaidiwi na Serikali na hata tathimini ya maeneo yenye uhitaji inapofanyika hawa walioanza wanaachwa bila kusaidiwa. Mfano; mosi, kutokana na shule ya Ruzinga Kata ya Ibuga yenye wanafunzi takribani 700 kuwa na vyumba vichache na vilivyochakaa, Kijiji cha Rwanda walianzisha shule mpya ya Bwanika ili kupunguza matatizo ya shule mama na kupunguza umbali kwa watu wa upande wa Busingo. Jengo la vyumba vinne na ofisi liko usawa wa kuezeka. Naomba wananchi hawa wasaidiwe.

Pili, kutokana na shule ya Biija Kata ya Nyakatanga yenye wanafunzi takribani 750 kuwa na vyumba vichache lakini kutokana na wanafunzi wake kutoka maeneo ya mbali na shule, eneo la Mulole kuna mradi wa ujenzi wa shule mpya sasa iko usawa wa lenta yenye vyumba vitano na ofisi. Ushauri wangu ni kuwa tathimini ya wahitaji iwaangalie wananchi hawa kwa kupima miradi hii miwili.

Tatu, kutokana na shule ya msingi Nyakatanga yenye wanafunzi 900 kuwa na vyumba vichache tena vidogo kwa size ya mkoloni na kutokana na baadhi wa wanafunzi kutoka mbali sana takribani kilometa 10, wananchi wanajenga shule eneo la Kalengo. Mpaka sasa wamekusanya vionwa na saruji wanayo. Hawa nao tathimini iwaangalie upya.

Nne, kutokana na shule ya msingi Ngenge Kata ya Ngenge yenye wanafunzi 1,000 na zaidi wengi wakitoka mbali shule ya Kalimalimo ilianzishwa sasa iko darasa la nne na wananchi wanajenga vyumba vitatu na ofisi, lakini ipo shule moja ya Kihya inajengwa umbali wa kilometa 13 na wananchi wanapambana kujenga ili kupunguza umbali lakini na tatizo la vyumba shule mama ya Ngenge. Naomba miradi hii mipya wananchi wasaidiwe.

Mheshimiwa Spika, tano, kutokana na wanafunzi kuwa wengi katika shule ya msingi Kata Bumbiile wanafunzi 700, lakini wanafunzi hutoka mbali, shule mpya Kisha imeanzishwa kupunguza tatizo hilo na lile la vyumba. Kuna vyumba viwili tu, wananchi wanapambana kujenga vyumba vinne kwa kukusanya vionwa kwa sababu vyumba hivyo viwili tayari kuna wanafuzi wengi sana. Hawa nao waangaliwe.

Sita, tatizo kama la Bumbiile liko shule ya Mushenyi Kijiji cha Buhaya, Kata ya Kagoma, nao waangaliwe; na saba, kutokana na kuwa na sehemu kubwa Wilaya kuwa ni ziwa (70%), kunahitajika boti salama na ziendazo kasi. Hii itasaidia sekta za afya, elimu, maendeleo na usalama. Tulishaleta mapendekezo na maombi tusaidiwe

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.