Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, Wizara ijielekeze katika kujenga uwezo wa kutimiza wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa kadri ya kiwango cha matarajio yaliyo wengi. Wizara hii ya TAMISEMI ni miongoni mwa Wizara kubwa, muhimu na mtambuka, lakini inakumbwa na changamoto ya kiutendaji.

Kwanza, Wizara inakabiliwa na ufinyu wa nguvu kazi, eneo muhimu katika kutekeleza majukumu; watendaji hawatoshi kwa idadi na yao na ubora na pia watendaji hawatoshi kiuweledi (professionalism). Aidha, majukumu muhimu yanatekelezwa na watendaji wasio na sifa za elimu na uelewa wa kazi husika (elimu na uelewa duni) mfano Halmashauri ya Mtama na Nanyamba, kazi za engineer zinatekelezwa na fundi wa cheti na kusababisha utekelezaji duni wa miradi ya hospitali kwenye maeneo hayo.

Pia watendaji kukosa maadili ya kazi hivyo hivyo kusababisha ubadhirifu mkubwa mahala pa kazi (upotevu wa pesa na mali).

Mheshimiwa Spika, pia watendaji wenye sifa kukaidi taratibu za kazi na maelekezo kutoka kwenye mamlaka zinazowatuma (Wizara yao) kwa mfano Masasi DC engineer alishindwa kutoa mchanganuo wa miradi aliyotekeleza baada ya kuamua kutozingatia BOQ iliyokuwa imuongoze kwenye utekelezaji wa vipengele vya mradi mkuu wa ujenzi wa A-Level ya Mpeta. Utaratibu aliouchukua baada ya kuachana na BOQ ulipelekea kupelea (deficit) ya shilingi 345,000,000; asilimia 34.5 zaidi ya pesa iliyokusudiwa kukamilisha mradi huo. Mradi ulipewa bilioni moja zikatumika zote hazikutosha.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya kiutendaji pia inajionesha kwenye mifumo; mifumo ni mingi lakini pia haisomani hivyo taarifa kuchelewa ama kuwa zisizo na uhalisia (potofu).

Mheshimiwa Spika, taarifa zinazotolewa kwa Wabunge kuhusu miradi na masuala ya ufuatiliaji zinachelewa, hongera Waziri kwa kuliona hilo naona ameanza kulifanyia kazi jambo hili.

Kuhusu mfumo wa udhibiti mahali pa kazi (internal control system) licha ya umuhimu wake umekuwa dhaifu kiasi cha kudhania kuma haupo. Shida kubwa inajionesha kwenye ukaguzi wa ndani. Eneo hili lingekuwa linafanya kazi zake vema, changamoto nyingi za ubadhirifu wa fedha zingepungua kama sio kwisha. Shida kubwa ya ubadhirifu inayoripotiwa mara kwa mara inatokana na ukosefu wa maadili uliokithiri.

Mheshimiwa Spika, kuhusu shida ya ajira kwa vijana; wahitimu wa vyuo (walimu) hasa wa sayansi waliohitimu miaka ya 2016, 2017 na 2018 wametuma maombi lakini mpaka sasa hawajapata kazi, wanaendelea kutuma mambo. Nashauri ajira zitolewe kwa kuzingatia majimbo ili kila jimbo lipate, hali ilivyo sasa inaonesha upendeleo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.