Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana kwa wasilisho lenu, napongeza ubunifu wa Waziri na timu yako kukutana na sisi Wabunge, napongeza kwa sababu mawazo yetu/yangu yamezingatiwa, pamoja na kwamba siyo yote ambayo bila shaka ni kutokana na ufinyu/ukomo wa bajeti. Nawashukuru sana kwa kukubali wazo na ombi langu la kuitizama hospitali kongwe ya Mafinga ambayo inahudumia Halmashauri tano za jirani kwa maana ya Mufindi DC, Mbalari, Mlimba, Iringa DC na sehemu ya Makambako. Hospitali hii pia iko kando ya barabara ya TANZAM 1 ambayo ndio corridor kuu kuelekea nchi za ukanda wa SADC kwa maana ya Malawi, Zambia, DRC na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza kututengea shilingi milioni 900 kwa ajili ya hospitali hii na nawaahidi mimi na Madiwani wenzangu kwa ushirikiano na CMT tutasimamia kwa ukaribu kuhakikisha kuwa lengo linatimia kwa viwango na kwa wakati. Ombi langu fedha iletwe kwa wakati na utekelezaji uwe kwa force account.
Kuhusu TARURA, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri na walau bajeti imeongezeka Mafinga kutoka around 900 million mpaka around 2.3 billion. Hii ni hatua kubwa, hata hivyo zipo changamoto hasa ya wakandarasi. Nitatoa mfano, Mkandarasi Rahda Investment wa Mbeya anayejenga barabara ya kuelekea katika Kituo cha Afya cha Ihongole, ndugu zangu sijui niseme nini, barabara hii mkandarasi alikuwa atukabidhi barabara tarehe 4 Machi, 2023 lakini mpaka nawasilisha mchango wangu huu, kazi haijafika hata 20%. Mkandarasi huyu ameitwa kwa DC, amekamatwa na TAKUKURU, wenzetu wa Chama cha Mapinduzi wamepiga kelele weeeee hakuna kinachoendelea, ilifika wakati wananchi waliandamana wakaamua kuondosha mawe ambayo mkandarasi aliyamwaga, kusambaza na kuondoka zake, siku moja kabla ya kikao cha Road Board akarejea site, in short anatufanyia mchezo, mkiwa wakali anaonekana siku mbili, siku ya tatu anaondoka, kwa ufupi ametugombanisha na wananchi na Mbunge, wananchi na Serikali, wananchi na chama, sote tunaonekana ametuweka mfukoni.
Mheshimiwa Spika, ninaomba sana, namna mtakayoona inafaa kuchukua hatua sio tu kwa kumuondoa lakini kwa kutafuta namna ambayo itatuondolea hii aibu, nawaomba. Kuna jitihada zimefanyika kwamba labda kazi hii afanye mwingine kwa internal arrangement, hii ni kwa sababu kiushauri wanasema kuvunja mkataba italeta more complications, naomba na naona aibu kuwasilisha jambo la ujenzi wa barabara ya kilometa moja kwenu.
Mheshimiwa Spika, nina ushauri kwamba pamoja na kuwa fedha haitoshi, lakini hii ambayo inatengwa walau inasaidia kupunguza kadhia ya barabara, hata hivyo nilichojifunza, inaonekana kazi ni nyingi kuliko uwezo wa wakandarasi au uwepo wa mitambo. Kwa sababu hiyo mkandarasi anashika kazi nyingi kwa sababu zipo, lakini anakuwa hana vifaa, ninashauri tuchukue hatua za makusudi na kuona uwezekano wa kuwasaidia kwa kuwajengea uwezo ama kuwadhamini kupata mkopo wa mitambo au TARURA kila kanda kuwa na mitambo ambayo itakuwa inakodishwa kwa wakandarasi na baadae wanakatwa katika malipo yao. Huu ni ushauri ambao wataalam wanaweza kudadavua na kuona the best practice ambayo inaweza ikawa sehemu ya suluhisho la kukabiliana na wakandarasi ambao hawatekelezi kazi kwa wakati na kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu TACTIC, kwanza naendelea kushauri tuendelee na vikao kati ya Wabunge wa miji 45, pili ninashauri kwa kuwa mradi huu utasaidia pia kujenga miradi ambayo itakuwa sehemu ya chanzo cha mapato, hii Tier 2 na 3 zingeunganishwa ili utekelezaji wake 2024/24. Kuchelewa kuanza utekelezaji kwa jambo ambalo ni mkopo wa WB ambayo nafahamu ina vigezo vingi vya kufuatwa lakini naamini majadiliano yakifanyika tunaweza kutekeleza tier hizi 2 na 3 kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, pia naomba kuwasilisha mchango wangu wa maandishi katika maeneo mahususi; kwanza naomba tusome huu ujumbe kuhusu madai ya huyu mwalimu; "Pole na majukumu Mheshimiwa, mimi ni Mwalimu Pascal Canisio wa Mnyigumba Sekondari. Ninaidai Serikali shilingi 2,770,000 (mishahara ya miezi mitatu), ni miaka mitatu sasa na jina langu linaonekana liko kwenye mfumo. Ninaomba msaada niweze kulipwa mapema ili nitatue matatizo yangu. check no. 11178565."
Nimemshauri awasiliane na Afisa Utumishi wa Halmashauri, majibu yake; "Wanasisitiza Serikali inalipa taratibu kulingana na bajeti, Mheshimiwa. Tatizo wapo watu wamedai baada ya mimi na wamelipwa."
Mheshimiwa Spika, naomba tumsaidie ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, maombi maalum; tuliwasilisha maombi ya Shule ya JJ Mungai kupewa fedha za ukarabati mkubwa. Tunashukuru shule ya A-Level ya Changarawe sasa imekaa vizuri. Shule ya JJ Mungai ni kati ya shule ambazo zilikuwa shule za wananchi chini ya MET - Mufindi Education Trust ambazo zilijengwa kwa nguvu ya wananchi na baadae zikachukuliwa na Serikali. Toka wakati huo na hasa baada ya kuanzisha kidato cha sita, hatujawahi kupata usaidizi kutoka Serikalini, tumewasilisha andiko fupi kuelezea hali halisi ya shule na tumetaja maeneo yanayopaswa kufanyiwa ukarabati.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya; kama ambavyo nimeeleza mara kadhaa, na ninashukuru mmetusikia na kututengea fedha shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa hospitali kongwe ya Mafinga. Hata hivyo Kata ya Upendo tumeanzisha ujenzi wa kituo cha afya na tayari tumeshajenga OPD na hivi karibuni tutaanza kutoa huduma za wagonjwa wa nje. Hivyo ombi letu kutokana na ukuaji wa ongezeko la watu na uchumi wa mazao ya misitu, uhitaji wa huduma katika kata hii ni muhimu sana, baada ya Kata ya Boma, Kata ya Upendo ni ya pili kwa idadi ya watu katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, ina watu 25,000 hivyo Serikali ikishirikiana nasi tutaendeleza ujenzi wa Kituo cha Afya Upendo tutasaidia sana kuboresha huduma.
Mheshimiwa Spika, kuhusu TACTIC; bado nashauri, Tier 2 na Tier 3 ziunganishwe ili utekelezaji wake uende kwa pamoja na kwa haraka. Mradi huu pamoja na kuboresha miundombinu, itasaidia hizi Halmashauri kuwa na vyanzo vya mapato, kwa mfano Mafinga moja ya miradi ambayo tumeainisha ni stendi ya malori ambayo tayari kwa mapato ya ndani tumeweka fence wire na tayari malori ya safari ndefu maarufu kama transit yana- park na kidogo tunapata mapato. Mradi mwingine ni stendi ya mabasi Mafinga ipo kando ya TANZAM 1, highway ya kwenda nchi za SADC, aidha, kutokana na kuimarika kwa sekta ya mazao ya misitu, Mji wa Mafinga unakua kwa kasi kama kitovu cha biashara katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hivyo mradi huu utakuwa viable na hautakuwa white elephant kama ambavyo imejitokeza katika baadhi ya maeneo.
Mwisho, nawapongeza sana utaratibu wa kutujulisha wajumbe kuhusu fedha zilizopelekwa katika Halmashauri zetu, ninaomba uwe ni utaratibu wa mara zote. Tupo Wabunge wa aina nyingi, tupo ambao tunafanya kazi kwa ukaribu na CMT/Mkurugenzi, hivyo kujua kila kinachoendelea, lakini wapo Wabunge ambao hata fedha za Mfuko wa Jimbo zikiingia anasikia kupitia group letu la whatsapp. Kwa hiyo, kwa kutoa taarifa mnatusaidia sana.
Mheshimiwa Spika, angalizo; pamoja na miongozo ya wapi fedha zikatumike, nashauri, pale ambapo kutakuwa na maboresho kwa maana ya baadhi ya Halmashauri kuwa na maombi mbadala, basi pawepo utaratibu wa kuyapokea ikiwa tu maombi hayo yatapata baraka za Kamati ya Fedha ya Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu hapa turuhusu flexibility lakini kwa kuweka mechanism ambayo baadae haitakuwa vurugu kwamba sasa kila mtu anataka kubadilisha kutoka shule A na kwenda shule B au C.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.