Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba kwanza nichukue nafasi hii kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Nachingwea kwa imani kubwa ambayo wameionesha kwangu ili niweze kuwawakilisha katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda naomba nijielekeze katika kuchangia Mpango huu, kwanza, kwa kuwapongeza watu wa Wizara wakisaidiwa au wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa namna ambavyo wamewasilisha Mpango huu ambao umekuwa na mwelekeo wa kutaka kuisaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kabla ya yote, nomba niunge mkono wale ambao wametangulia kusema kwamba hatuwezi kutekeleza Mpango huu kama hatuwezi kujielekeza katika kufanya makusanyo mazuri katika kodi, lakini pia katika kupata fedha kutoka vyanzo mbalimbali ambavyo vitatuwezesha kutimiza malengo ambayo tumejiwekea. Mengi yameshasemwa lakini Mipango mingi imeshapangwa kwa kipindi cha nyuma ambacho sisi tumekuwa nje ya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ubunifu wa ukusanyaji wa mapato yetu. Nimeupitia Mpango huu vizuri sana, yako maeneo ambayo nafikiri wenzetu wa Wizara wakisaidiana na wadau mbalimbali wanatakiwa kuendelea sasa kujifunza kutoka katika maeneo mbalimbali ili tuweze kukusanya kodi kwa uhakika tuweze kutimiza malengo ya Mpango wetu. Pia Mheshimiwa Waziri nikuombe tuendelee kutumia wataalam wetu mbalimbali hata walio nje ya Wizara ili waweze nao pia kutoa mawazo ambayo yatasaidia katika kukamilisha Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo ambayo ningependa nijielekeze kama ambavyo malengo ya Mpango wetu yanavyozungumza. Kuna eneo la viwanda na Serikali ya Awamu ya Tano imejielekeza katika kuimarisha viwanda. Kwa sisi ambao tumetoka Mikoa ya Kusini kwa maana ya Lindi na Mtwara, tumekuwa ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya biashara; tuna korosho, tuna ufuta na sasa hivi tuna mbaazi. Hatuwezi kujadili kujenga uchumi mkubwa wa nchi yetu kama hatuwezi kujadili namna ya kuwaimarisha na kuwaendeleza wananchi katika ngazi ya chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wilaya ya Nachingwea inavyo viwanda vikubwa viwili ambavyo vimebinafsishwa. Tuna Kiwanda cha Korosho pale Nachingwea na tuna kiwanda cha kukamua mafuta, vyote wamepewa wawekezaji na viwanda hivi vimeshindwa kuendelezwa. Naomba Mheshimiwa Waziri, tunamwomba Rais wetu katika ari hii aliyoanza nayo, hivi viwanda nafikiri kuna kila sababu ya kwenda kuviangalia na tuweze kuvirudisha ili viweze kwanza kutoa ajira kwa wananchi wanaozunguka maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tuweze kuimarisha upatikanaji wa huduma ili tuweze kuandaa mazao yetu wenyewe katika maeneo haya ya kuanzia ngazi za chini. kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunapojadili viwanda viko viwanda ambavyo tayari hatuhitaji kufanya kazi kubwa ili tuweze kuviendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulichangia, ni suala zima la miundombinu, Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Mtwara kwa kutoa hizi malighafi ambazo nimezizungumza ambazo tunahitaji kujenga viwanda bado tumekuwa na changamoto kubwa sana ya mawasiliano na hasa katika eneo la barabara. Leo tunajadili Mkoa kama wa Lindi bado hatujafikia hatua ya kuweza kuunganisha kupata mawasiliano ya uhakika. Bado tuna tatizo la barabara sasa hatuwezi kufikiria kufanya mambo makubwa wakati bado wananchi wetu wanaendelea kupata shida ya usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo barabara ambazo toka nimepata akili mpaka leo bado zinazungumzwa na bado hazijafanyiwa kazi. Tuna barabara ya Nanganga - Nachingwea, tuna barabara ya Masasi – Nachingwea, bado tunahitaji barabara hizi zijengwe kwa kiwango cha lami. Pia tunahitaji tujengewe barabara ya kutoka Nachingwea kwenda Liwale na haya ndiyo maeneo ambayo yanazalisha kwa sehemu kubwa mazao ya biashara ambayo nimeyataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji pia barabara ya kutoka Nachingwea - Ruangwa na barabara zile zinazounganisha Mkoa wa Lindi pamoja na Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma. Haya yote ni maeneo ya kiuchumi ambayo kwenye Mpango huu lazima tujielekeze kwenye bajeti yetu tuone maeneo haya yanapata huduma muhimu ili tuweze kufikia malengo ambayo tumejiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa pia kuchangia, ambalo pia nimepitia katika huu Mpango ni eneo la nishati na madini. Tunayo changamoto, naomba niungane na wenzangu kumpongeza Waziri ambaye anashughulika na eneo hili Profesa Muhongo, iko kazi kubwa naomba nikiri kwamba imefanyika na inaendelea kufanyika, lakini bado tunazo changamoto ambazo tungependa kushauri Serikali yetu iongeze jitihada. Leo maeneo mengi ya vijiji vyetu yanapata umeme, lakini tungependa speed iongezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Muhongo, wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara ndiyo sasa hivi wanatoa gesi ambayo tunaitumia Tanzania nzima. Ni vizuri sasa mipango hii ambayo tunakwenda kuipanga, tuanze kunufaika watu wa maeneo haya ili wananchi wetu waweze kujikwamua na kupata uchumi ambao tunaukusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulisemea ni katika upande wa madini. Mkoa wa Lindi na Mtwara bado ziko fursa nyingine ambazo ningependa kuishauri Serikali ijielekeze kufanya utafiti. Sasa hivi Wilaya kwa mfano ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi sehemu kubwa ina madini. Madini ambayo bado hayajatumika, madini ambayo bado Serikali haijatambua kwamba yanaweza yakakuza uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo madini maeneo ya Nditi, Kilimarondo na Marambo, haya ni maeneo ambayo nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa heshima na taadhima, aelekeza wataalam wake waje tutawapa ushirikiano ili waweze kufanya utafiti wa kutosha tuweze kupata madini mengi zaidi ambayo yatalisaidia Taifa letu na pia yatasaidia wananchi wanaozunguka maeneo haya, kwa maana ya kuwapatia ajira na kukuza kipato cha Mtanzania wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuchangia ni eneo la elimu. Nimepitia vizuri huu Mpango, naomba niwapongeze kwa kazi kubwa ambayo imefanyika. Naomba nimpongeze kwa upekee kabisa Rais wetu mpendwa aliyepita Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Iko kazi kubwa ameifanya ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inatakiwa kuiendeleza. Leo hii nimezunguka ndani ya Jimbo langu Kata zote 32, changamoto kubwa ambayo tunakutana nayo ni ukosefu na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuliona hili Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alianzisha kwa makusudi jitihada za ujenzi wa maabara. Maabara hizi sasa hivi zimesimama, hazina msukumo; nilifikiri lengo lake lilikuwa ni zuri. Sasa kupitia Mpango huu naomba kwenye bajeti tunayokwenda kuipitisha, maabara hizi sasa tuzitoe mikononi mwa wananchi kwa sababu wamechangia nguvu zao kwa sehemu kubwa, badala yake Serikali ichukue kwa maana iliahidi itatoa vifaa, itamalizia majengo haya ambayo tayari tumeshayajenga ili tuweze kuzungusha tupate Walimu ambao watakwenda kufundisha kwenye shule zetu na tutapata wasomi wazuri wa masomo ya sayansi ambayo watasaidia katika kada nyingi ambazo tumekuwa na tatizo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili niliona ni pendekezo ambalo nalo pia ningependa kulizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la afya. Bado kwenye Mpango hatujaeleza ni namna gani Serikali imejipanga kusaidia kuona namna gani tunajenga vyuo vingi zaidi ili tupate wataalam. Leo hii hospitali zetu, zahanati zetu zina matatizo makubwa ya wataalam. Hii tutaipatia majibu kwa kutengeneza mkakati wa kusomesha wasomi wengi zaidi ambao watakwenda kuisaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia, ni eneo hili la uchumi kwa maana ya Mawaziri wetu ambao wamechaguliwa na Mheshimiwa Rais wetu, msaidieni Rais wetu, Rais wetu ameanza vizuri anafanya kazi nzuri. Naomba niwasihi Mawaziri wetu fanyeni kazi, sisi tuko nyuma yenu, tunaahidi kuwapa ushirikiano, lengo letu ni kuwakwamua Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe katika eneo la kilimo, naomba nitoe pongezi pia kwa Serikali kwa kazi kubwa inayofanya. Ipo changamoto ambayo nimeiona, ambayo ningependa kuishauri Serikali yangu. Kuna eneo la umwagiliaji, utengenezaji wa miundombinu, pesa nyingi inatengwa kwenda huko, lakini miradi mingi inahujumiwa huko chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba watu wa Kanda, kaka yangu Mwigulu yupo hapa ndani, namwomba afuatilie hili eneo. Pesa nyingi inapotea, miradi mingi ya umwagiliaji haifanyi kazi, nenda Nachingwea, upo mradi mkubwa pale Matekwe ambao ungeweza kunufaisha Watanzania, pesa yote imepotea, hakuna mradi uliokamilika. Nimewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, miradi mingi ya umwagiliaji ni hewa, pesa ukienda inasimamiwa na watu wa Kanda. Naomba Mheshimiwa Waziri fuatilia hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la pembejeo, nimekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Pembejeo, pesa nyingi ya pembejeo Mheshimiwa Waziri inapotea katika eneo hili. Malengo ya Serikali ni mazuri, lakini pesa hii hakuna mtu wa kumwamini sasa hivi. Naomba Serikali kupitia Wizara Fedha, kupitia Wizara ya Kilimo ifuatilie kwa karibu eneo hili. Tulete mapendekezo mazuri yatakayosaidia ili wananchi wetu kweli wanufaike kwa kupata pembejeo kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, naomba nishukuru, lakini pia naomba niunge mkono hoja juu ya Mapendekezo ya Mpango huu ambao lengo lake ni kuwasaidia Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)