Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Pia namshukuru Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Pwani kwa kunipigia kura na kunifanya kuwa Mbunge katika Bunge lako. Niungane na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano kwa kuanza kazi vizuri, nina kila sababu ya kumpongeza kwa matukio yafuatayo machache:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa usimamizi mzuri wa makusanyo ya mapato ambayo naamini yatatekeleza mpango wa maendeleo unaokuja na bajeti hizi ambazo zinaendelea. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa fly over na naipongeza Serikali ya Japan ilikuwepo, napongeza kwa uzinduzi wa mradi wa Kinyerezi I pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi kinyerezi II. Pia nampongeza sana Rais Museven kwa kukubali bomba la mafuta kupitia Bandari ya Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nayapongeza haya nikiamini kabisa viongozi wa Mataifa mbalimbali ya nje yana imani na Mheshimiwa Rais wetu, hawana tatizo na kuona kwamba mpaka sasa instruments hazijatoka, kwa sababu wanaamini wao ni kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia napongeza fursa ambayo Serikali ya China imeonesha kutaka kutu-support katika ujenzi wa reli ya standard gauge. Naipongeza kwa sababu China wanataka kutoa hela nyingi lakini hawajapata kuuliza instrument ya Waziri wa Mawasiliano wala ya Waziri wa Ujenzi, naamini wao wanaamini hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na pongezi hizo, naomba nijielekeze kwenye bajeti. Nampongeza Waziri wa TAMISEMI, pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora na Naibu Waziri wameanza kazi vizuri, wanashughulikia masuala ya mishahara hewa vizuri na wanapambana. Nikipitia hotuba ya Waziri wa TAMISEMI pamoja na mikakati ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana, naomba nijielekeze zaidi kwenye sekta ya afya. Katika kujielekeza sekta ya afya nimeona kupitia bajeti hii mkakati wa Serikali wa ujenzi wa vituo vipya vya afya, ujenzi wa zahanati, ukarabati wa hospitali za wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali iangalie sera, Wizara ya Afya nadhani ingekuwa vizuri kama ingepewa jukumu pia la usimamizi wa vituo hivi kwa sababu wao wanasimamia sera. Inapokuwa TAMISEMI na wao wana mambo mengi, lakini changamoto kubwa zipo kwenye maeneo ya vituo vya afya, ziko kwenye maeneo ya hospitali za wilaya na ziko kwenye zahanati. Kwa kuwa TAMISEMI wanaendelea kusimamia, lakini kwa kuwa haihusiani na masuala ya sera, usimamizi kidogo unakuwa hafifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijielekeza zaidi katika ujenzi huo wa zahanati na ukarabati nimeona bajeti ya mwaka 2014/2015 takribani bilioni 263 zilitumika, lakini mwaka 2016/2017 zimetengwa bilioni 27. Naona hiki kiwango ni kidogo nikiangalia changamoto ambazo zinatukabili na nazielekezea changamoto hizo kwenye hospitali yetu ya Wilaya ya Mkuranga ambayo haina X-Ray; kituo chetu cha afya cha Kibiti katika Wilaya mpya hakifanyiwa upanuzi wa jengo la wazazi; kwenye kituo chetu cha afya Mkoani Kibaha changamoto kubwa ni jengo la upasuaji, pia hata kituo cha afya Maneromango, vifaa vya upasuaji vipo, lakini jengo halipo. Nashauri katika kifungu hiki angalau kingeongezwa zaidi ili tuweze kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona wakati nikipitia hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani katika ukurasa wa tatu, nanukuu:
“Kambi Rasmi ya Upinzani inawataka Wabunge wa CCM waache kufanya ushabiki Bungeni”.
Pia katika ukurasa huo huo nanukuu kwamba:
“Vyombo vya Habari vya Umma na Binafsi virushe moja kwa moja mijadala ili wananchi wajue fedha zao zinavyogawanywa katika Halmashauri zao na wajue ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Ibara ya 89 imeipa Bunge wajibu wa kutunga Kanuni za Uendeshaji wa Bunge hili, Kanuni za Kudumu za Bunge, Kifungu 116 zimempa mamlaka Spika kuunda Kamati, pia zimeipa mamlaka Kamati zenyewe kuchagua Wenyeviti wao wa Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Usimamizi wa pesa za Halmashauri (LAAC) na Kamati ya Hesabu ya Serikali (PAC), kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ambazo zinatokana na Katiba zinatakiwa ziongozwe na Wapinzani. Leo wanapoituhumu Serikali kuvunja Katiba, kuvunja taratibu mbalimbali, wao hawajitazami mpaka leo Wenyeviti wa Kamati hizo hawajachaguliwa, leo wanaposema Bunge lioneshwe live lakini wao hawajatimiza wajibu wao zaidi ya miezi minne, Kamati hazijapata Viongozi kutoka Kambi ya Upinzani na mamlaka hiyo ni ya Spika.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekeni Kiongozi unajipangia utaratibu kuteua Wajumbe wa Kamati hukupewa mamlaka hiyo! Ni mamlaka ya Spika kuwapanga Wabunge kwenye Kamati zao kwa vigezo vyao na Kanuni tumetunga wenyewe za Bunge hili. Nilidhani wangetoa ushauri kwamba Kamati zinazoongozwa zipewe mamlaka zenyewe. (Makofi)
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Taarifa!
Taarifa....
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa siipokei, kwa kuwa hakujielekeza kwenye Kanuni yoyote na mimi nimesema kama ana ushahidi wa Party Caucus kukutana ili kuchagua viongozi, walichaguliwa ndani ya Kamati husika, hiyo taarifa yake siyo sahihi naomba watimize wajibu wao kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, CAG (Controller and Accounting General) amewasilisha ripoti yake, lakini najua kwa nini hawajachagua mpaka sasa hivi, wamepima maji wameona yana kina kirefu. Mheshimiwa Aeshi endelea na kazi, chapa kazi PAC, umegundua mambo, LAAC nayo endeleeni, chagueni Makamu Mwenyekiti aendelee na kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze pia kwenye ukurasa wa mwisho wa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wanaelezea masuala ya vifungu vya Sheria ya Bajeti, kwa kuwa kitabu hiki kinatumika na Wabunge wote na ni upotoshaji, sasa nataka nijielekeze kwenye Public Finance Act hiyo, Kifungu 19 naomba wanavyo-quote Sheria za Fedha wamalizie wasi-quote nusunusu. Kifungu cha 19 kinasema; “If at the close of account for any financial year it is found that moneys have been expended:-
(a) on any expenditure vote in excess of the amount appropriated for it by an Appropriation Act;
(b) for a purpose for which no moneys have been voted and approaprated.
(c) the amount of excess expended or not appropriated as the case may be shall be included in a statement of expenditure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mwaka wa fedha wa Serikali haujakwisha msiwahishe shughuli, mnapo-quote Sheria mbalimbali za Fedha mmalizie, mme-quote Public Finance Act 18 (a) na 14, kwa nini hamku-quote 19 ambayo ndiyo imetoa mamlaka mwisho wa mwaka wa fedha kama kuna pesa zimetumika za ziada ambazo hazikutengwa ziwasilishwe ndani ya Bunge katika taarifa maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha haujakwisha lakini kama pia pesa zilitumika zaidi na naomba kwenye masuala ya barabara, nimeona kwenye kitabu cha TAMISEMI mpango wa ujenzi wa barabara, namwomba tu Waziri wa Fedha mwaka wa fedha wa Serikali ukiisha awasilishe statement, tuipitishe kwa sababu yamefanyika mambo ya heri na mamlaka hiyo anayo, kwa hiyo hakuna uvunjaji wowote wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba niwazungumzie Wabunge Wanawake namna ambavyo hawashiriki vikao vya Kamati vya Fedha Halmashauri za Wilaya. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, Ibara ya 66, imetaja aina za Wabunge wakiwemo Wabunge Wanawake. Wabunge wote wana haki sawa, inashangaza kwamba Wizara ya TAMISEMI Katibu Mkuu anatoa mwongozo wa kuwatoa Wabunge Wanawake ambao wanasimamia maslahi ya wanawake, maslahi mapana na changamoto mbalimbali katika Kamati za Fedha, kama leo wanapoleta milioni hizo hamsini, asilimia 10 ya Vijana na Wanawake, mambo ya sekta ya afya, mambo ya kilimo, Mbunge Mwanamke na yeye ana mchango mkubwa kwenye Kamati ya Fedha ambayo inakutana kila mwezi, Wabunge wana uwezo wa kuchangia hoja na kujenga hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya TAMISEMI tumelisemea kila siku, huu ni mwongozo tu, mtoe mwongozo kuwa Wabunge Wanawake na Madiwani Wanawake, tusibaguliwe na wala tusinyanyaswe, kwa sababu pia Katiba imekataza sheria yoyote inayoonesha ubaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono Bajeti na naunga mkono kwamba hakuna uvunjaji wowote wa Kanuni wala wa Katiba, wanaposhutumu na wao wajitazame, wajisahihishe, kidole kimoja kinawatazama. Ahsante sana.